*********************************
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wilayani Dodoma mjini wameshauriwa kutouza ardhi kiholela badala yake kupata
msaada wa kisheria kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Mwalimu Josephat Maganga alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Mtumba jijini Dodoma jana katika ziara yake ya kujitambulisha, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mwalimu Maganga alisema “ndugu zangu wapendwa wana Mtumba pamoja na mitaa yetu yote minne, Vikonje ‘A’, Vikonje ‘B’, Majengo na Mtumba, hii ardhi tunayoiona kama wanavyosema zamani haikuwa na thamani. Lakini tumekuja kugundua kwamba ina thamani kubwa. Wananchi tunaongezeka, tunakuwa wengi lakini ardhi ipo hivyo hivyo. Hii ardhi ni kitu cha thamani, ina thamani kiuchumi, tunalima kwenye ardhi hii tunapata chakula, tunajenga kwenye ardhi hii nyumba zetu na tunaishi, tumezaliwa kwenye ardhi hii na inawezekana na nikweli kabisa kwamba hata kufa tutazikwa kwenye ardhi hii”.
Alisema kuwa ardhi ni kitu cha thamani na yanapofanyika maamuzi ya ardhi wanaoyafanya wahakikishe wanafanya mamauzi sahihi. Aidha, aliwataka Wenyeviti wa Mitaa na watendaji kuwa makini na uuzaji ardhi. “Ndugu zangu naomba tuwe makini na uuzaji holela wa ardhi, tuwe makini sana. Hata kama mwananchi wa kawaida anataka kuuza eneo lake, sheria zinaturuhusu kuhoji, kwa sababu anaweza akauza ardhi hapa, mkastukia anakuja mtu anatengeneza mambo ya baruti hapa, ukimuuliza anasema anapasua miamba hapa halafu anasababisha matatizo. Tutahitaji kujua huyo mtu ni nani? anatoka wapi na kwanini aje anunue ardhi kubwa hapa. Kuna wakati mwingine wanakuja watu wataalam kuwazidi hata nyie wenyewe. Niwaombe kabla ya kufanya maamuzi shirikisheni, Halmashauri ya Jiji lazima itatoa msaada wa kisheria” alisema Mwalimu Maganga.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga shilingi milioni 210 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliotwaliwa maneo yao. “Nafurahi kuona hawa wananchi 34 wanapata fidia zao shilingi milioni 210. Niipongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga fedha hizo ambazo nimetaarifiwa zitalipwa mwezi huu” alisema Mwalimu Maganga.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akijibu swali la mwananchi wa Kata ya Mtumba, Jackson Seganje aliyetaka kujua alipo ya fidia kwa wananchi 34 ambao hawakuwepo katika uthamini uliopita wa eneo la Mtumba, alisema kuwa malipo hayo yatalipwa mwisho wa mwezi Agosti mwaka huu.
Mafuru ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mipango miji, Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, ni kweli kuna wananchi 34 ambao kwenye eneo tulilotwaa hawakuwepo wakati wa zoezi la uthamini. Eneo ambalo tulitwaa tulirudia mara nne zoezi la uthamini. Hii ni kwa sababu mnaweza kufanya zoezi hilo lakini bahati mbaya wachache wasiwepo wakati wa utekelezaji zoezi hilo, kuna kitu kinaitwa ‘supplementary valuation’ kwamba watakapokuwa wale watu tutawafanyia kitabu cha pili ili wa kwanza wanalipwa kwanza na wale wengine wanalipwa baadae. Sasa hawa waliobaki wananchi 34 ni wa awamu ya tano ambapo wanadai shilingi milioni 210” alisema Mafuru.
Mkuu huyo wa Idara alikiri kuwa wananchi hao walipaswa kulipwa mwaka wa fedha ulioisha ila taratibu hazikukamilika na kuahidi malipo hayo kufanyika kufikia mwisho wa mwezi Agosti, 2020. “Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nachoweza kukuahidi pamoja na wananchi hawa ni kwamba kabla ya mwezi huu Agosti kuisha fedha zao zitakuwa kwenye akaunti zao. Malipo haya ni kipaombele kwetu kwa sababu tulifunga nayo mwaka wa fedha uliopita” alisema Mafuru kwa kujiamini.
MWISHO
No comments :
Post a Comment