Sunday, August 16, 2020

MABULA AWABANA WADAIWA KODI YA PANGO LA ARDHI JIJI LA MWANZA ‘WATEME’ BILIONI 2.2

 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimuonesha Ramani ya Mkoa wa Mwanza Mkuu wa mkoa huo  John Mongela alipomkabidhi ramani hiyo akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza mwishoni mwa wiki. Wizara ya Ardhi kupitia Idara yake ya Upimaji na Ramani ndiyo yenye jukumu la kuandaa ramani ya Tanzania pamoja na zile za Mikoa. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Wadaiwa wa kodi ya Pango la Ardhi katika halmashauri ya Jiji la Mwanza mwishoni mwa wiki akiwa katika ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza.Kulia ni Kamishna Msaidzi wa Ardhi mkoa wa Mwanza Makwasa Biswalo na kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba. Sehemu ya Wadaiwa wa kodi ya Pango la Ardhi katika halmashauri ya Jiji la Mwanza waliokutana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kuangalia namna bora ya kulipa madeni wanayodaiwa mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Mwanza.Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kuhusiana na mradi wa ujenzi wa ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania katika eneo la Mkolani wilaya ya Nyamagana kutoka kwa Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Mwanza Fadhili wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki. Mradi huo unajengwa na NHC. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI).

*********************************

Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewabana

wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi katika jiji la Mwanza na kuwataka kila mmoja kueleza ni muda gani watalipa deni wanalodaiwa.

Jiji la Mwanza lina wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi123 wanaodaiwa takriban bilioni 2.2 na Naibu Waziri Mabula alikutana na wanaodaiwa kuanzia shilingi  milioni 3 ambapo kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa ardhi mkoa wa Mwanza Makwasa Biswalo jiji la Mwanza linatakiwa kukusanya Bilioni 6 ya kodi ya pango la ardhi .

Hata hivyo, takriban wadaiwa wote aliokutana Dkt Mabula waliahidi kulipa madeni yao huku baadhi wakiomba kulipa kwa awamu ambapo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi  aliwataka kuandika barua ikieleza  azma hiyo na muda watakaokamilisha malipo.

Akiwa katika ziara yake ya kikazi katika jiji Mwanza mwishoni mwa wiki Dkt Mabula aliwatahadharisha wamiliki wanaodaiwa kodi ya pango la ardhi  kutosubiri kushitakiwa katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya na kubainisha kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha makusanyo yanapatikana ili kusaidia shughuli za kimaendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati.

Alisema,  baada ya kikao chake na wadaiwa wa kodi ya ardhi wale wote watakaokaidi watapelekewa ilani ili wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba na Wilaya alikokuelezea kuwa, maamuzi  yake yatakuwa ni kulipa ama mali kunadiwa kufidia deni.

” kumiliki ardhi kumesisitizwa lakini pia kila mmiliki ajue wajibu wake wa kujua kulipa kodi na sisi tumeona badala ya kutumia sheria ya kuwafikisha mahakamani tuwaite tuwasikilize na kuwapa hamasa kulipa ili kumuwezesha mhe Rais kufanya shughuli za kimaendeleo ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati” alisema Dkt Mabula

Aidha, Naibu Waziri Mabula ambaye alizitembelea pia halmashauri za wilaya za Misungwi na Kwimba katika mkoa wa Mwanza alilitaka jiji la Mwanza na halmashauri nyingine nchini kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kulipa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa na serikali kwa shughuli za umma.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula kuna baadhi ya  maeneo ambayo  halmashauri imeyachukua kwa ajili ya shughuli za umma lakini wamiliki wake hawajalipwa fidia na kusisitiza kuwa ni vizuri halmashauri zikatenda fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kulipa fidia kwenye  maeneo hayo.

Pia Naibu Waziri wa Ardhi alizitaka halmashauri nchini zenye mipango kabambe kuacha kutoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo bila kuzingatia mipango hiyo na kutolea mfano wa halmashauri ya jiji la Mwanza na Ilemela kuwa pamoja na kuwepo mpango unaoelekeza aina ipi ya ujenzi hufanyika bila kuzingatia na kusisitiza utoaji vibali vya ujenzi  uzingatia mpango kabambe.

No comments :

Post a Comment