Mtaalamu wa Mifumo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel
Maendaenda (kulia) akitoa maelezo ya Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG)
kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba, alipotembelea
Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya
Nyakabindi Mkoani Simiyu. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Benny Mwaipaja.
Watoto wakiwa wanasoma machapisho mbalimbali yanayohusu Mifumo ya
Fedha, yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya
Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Furaha Alphad na Ilham Khalid (wa kanza na wa pili kulia) ambao ni
wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Dutwa Mkoani Simiyu,
wakisikiliza kwa makini maelezo kuhusu Sekta Fedha kutoka kwa Mtaalamu
wa Huduma Ndogo za Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Joseph
Msumule (wa pili kushoto) walipotembelea Banda la Wizara hiyo katika
Maonesho ya Nanenane Kitaifa, katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani
Simiyu.
Wanafunzi wa Sekondari ya Kidinda Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu,
wakisikiliza Maelezo Mtumishi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Bi.
Grace Masawe, kuhusu masuala mbalimbali ya Chuo zikiwemo sifa za
kujiunga na Chuo hicho, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, katika
Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Katibu
Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba (kushoto), akizungumza
jambo na watumishi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) alipotembelea
Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane
Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
(Picha na Peter Haule, WFM)
*********************************
Na. Peter Haule, WFM, Simiyu
Katibu Tawala wa
Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Tutuba, ameishauri Wizara ya Fedha na
Mipango na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuratibu kwa karibu vikundi
vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VIKOBA ili kutoa elimu na
ufahamu kabla ya mwananchi kujiunga au kukopeshwa fedha ili kuwa na
uhakika na usalama wa fedha.
Rai hiyo
imetolewa na Bw. Tutuba, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na
Mipango wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa
katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
“Kuna vikundi
vinavyowaambia wananchi kuwa vinatoza riba ya asilimia tano, kumbe
asilimia hiyo ni kwa mwezi na sio kwa mwaka ukifanya hesabu utagundua
riba kwa mwaka ni asilimia 60 ilihali kuna benki zinazotoa mikopo kwa
riba ya asilimia 18 kwa mwaka, hivyo lengo la huduma ndogo za fedha
kumsaidia mwananchi kurahisisha shughuli za kiuchumi halifikiwi”,
alieleza Bw. Tutuba.
Bw. Tutuba
alisema kuwa, kuna vikundi wananchi wanaunganishwa bila kuwa na ufahamu
wa kutosha hivyo kuchangishwa fedha lakini akienda kudai maslahi yake
anaambiwa fedha hazipo, jambo ambalo taasisi zinazodhibiti vikundi hivyo
zinabidi kufuatilia kwa karibu kwa kutoa elimu toshelevu ili mwananchi
aweze kufanya maamuzi sahihi.
Pia alisema kuwa
kwa ngazi ya Halmashauri anashauri fedha zinazotolewa kama mikopo kwa
vikundi vya Wanawake, Vijana na Wlemavu, zitolewe kwa mfumo wa kibenki
utakaosaidia ufuatiliaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa urahisi kwa
kuwa na uelewa wa maana ya mikopo.
Alisema kuwa kuna
vikundi ambavyo vinaanzishwa kwa mtazamo wa kutafuta fedha bila kuwa na
wazo au biashara yenye tija kwa kikundi na eneo alipo hivyo dhana ya
kuwakomboa wananchi kupitia mikopo hiyo kutofikiwa.
“Wale
wanaokopeshwa wakipata fedha katika mifumo ya kibenki watapata elimu
inayotakiwa, watarejesha fedha kwa uhakika, watafuatiliwa lakini hata
dhamana sio lazima ziwe za ajabu zaidi ya muhtasari wa Kijiji kutambua
biashara yake”, aliongeza Bw. Tutuba.
Alisema
ikiwezekana ianzishwe Benki katika Serikali za Mitaa itakayosaidia kutoa
fursa kwa watu kutoa wazo la mradia au biashara na litakapodhibitishwa
lina tija katika uchumi wa Kijiji au Kata linaweza kudhaminiwa na
Serikali ya Kijiji ili watu waweze kurejesha fedha.
Alifafanua kuwa
Benki hiyo itawahudumia wananchi kwenye maeneo yao badala ya kuwaacha
wananchi kwenda kurubuniwa kwenye vikundi vyenye dhamira ovu.
Kwa upande wake
Mtaalamu wa Masuala ya Sekta Ndogo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Joseph Msumule, alisema kuwa Sheria mpya ya huduma ndogo za
fedha imeanzishwa ili kurahisisha utoaji wa huduma hiyo lakini kudhibiti
wafanyabiashara wenye nia ovu kwa wananchi, pia sheria imeweka kiwango
cha mtaji kwa wakopeshaji ili kusajiliwa, lengo likiwa ni kusaidia
vikundi vya kuweka na kukopa kuwa na uwezo wa kutoa huduma wakati
inahitajika.
No comments :
Post a Comment