Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akilihutubia Taifa kwenye Sherehe ya Uzinduzi wa Maonesho ya Sikukuu ya
Wakulima Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu
leo ambapo ujumbe wa mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi Chagua Kiongozi Bora 2020.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akizindua Muongozo wa Kitaifa wa Uongezaji wa Virutubisho katika
matumizi ya mazao ya Chakula wakati wa Uzinduzi wa Maonesho ya Sikukuu
ya Wakulima Nanenane Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani
Simiyu leo ambapo ujumbe wa mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi Chagua Kiongozi Bora 2020.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akimkabidhi Muongozo wa Kitaifa wa Uongezaji wa Virutubisho katika
matumizi ya mazao ya Chakula Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima mara
baada ya kuuzindua Muongozo huo leo katika uzinduzi wa Sherehe ya
Sikukuu ya Wakulima Nanenane kitaifa iliyofanyika katika Viwanja vya
Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akizindua Jengo la Kituo cha Elimu kwa Wakulima Kanda ya Ziwa Mashariki
wakati wa Uzinduzi wa Sikukuu ya Wakulima Nanenane iliyofanyika leo
Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu. ambapo ujumbe wa
mwaka huu Nanenane kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua
Kiongozi Bora 2020.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akimsikiliza Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Mlingano
Dkt. Catherine Senkoro alipokuwa akimuelezea kuhusu Utafiti wa mazao ya
aina mbalimbali ya Kilimo alipotembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa
Kilimo TARI katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi
Mkoani Simiyu.Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akizungumza na Baadhi ya watumishi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI
Mlingano alipotembelea Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI katika
Viwanja vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akiangalia baadhi ya Mazao ya aina mbalimbali ikiwemo Vitunguu maji,
Nyanya na Viazi Mviringo alipotembelea mabanda maonesho katika Viwanja
vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akiangalia baadhi ya Bidhaa za aina mbalimbali ya Kilimo ikiwemo
alipotembelea mabanda maonesho katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane
vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo kulia Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet
Hasunga.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akiangalia mazalio ya Samaki alipotembelea Banda ya JKT katika Viwanja
vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akiangali Ng’ombe wa Maziwa kwenye mabanda ya maonesho katika Viwanja
vya Maonesho ya Nanenane vya Nyakabindi Mkoani Simiyu leo. (Picha na
Ofisi ya Makamu wa Rais)
………………………………………………………………………………………..
HOTUBA YA
MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA WAKATI WA UZINDUZI WA MAONESHO YA KILIMO NA SHEREHE ZA
WAKULIMA NANE NANE
TAREHE 01 AGOSTI, 2020 KATIKA
VIWANJA VYA NYAKABINDI – MKOANI SIMIYU
Mheshimiwa Japhet N. Hasunga, Waziri wa Kilimo;
Mheshimiwa Luhaga Mpina, Waziri wa Mifugo na Uvuvi;
Waheshimiwa Mawaziri wote mliopo;
Mheshimiwa Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa;
Waheshimiwa Manaibu Waziri;
Ndugu Gerald M. Kusaya, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo;
Ndugu Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu mliopo;
Makatibu Tawala wa Mikoa;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Waheshimiwa Wabunge;
Wadau wa Maendeleo;
Wakurugenzi wa Mamalaka za Serikali za Mitaa;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi wa Dini;
Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wanaushirika;
Ndugu Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Ndugu Wananchi
Mabibi na Mabwana;
Asalaam Aleikum Bwana Asifiwe; Mwadila wa Baba na Wamayo/Iminza/ Ise Simiyu Ise!
Nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutufikisha Simiyu salama
salimini na kuweza kujumuika nanyi leo. Kama mnavyofahamu, juzi
tumemaliza siku saba za maombolezo ya mpendwa wetu, Mzee wetu, Kiongozi
wetu na Rais wetu Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin William
Mkapa ambaye alitutoka usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 23 Julai 2020.
Naomba tusimame kwa dakika moja ili tumuombee Kiongozi wetu. Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina.
Nichukue
fursa hii kumshukuru Mkuu wa Mkoa Simiyu – Mkoa Mwenyeji, Mheshimiwa
Mtaka akishirikiana na Wakuu wa Mikoa jirani ya Mara na Shinyanga pamoja
na Kamati ya Maandalizi, kwa maandalizi mazuri ya Maonesho ya 28 ya
Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane zinazofanyika ngazi ya Kitaifa
katika viwanja vya Nyakabindi hapa Simiyu.
Kwa wananchi
wa Simiyu nawashukuru sana kwa mapokezi mazuri na ukarimu wenu ambao
mmekuwa mkinionesha mara kwa mara ninapotembelea Mkoani kwenu. Hii ni
mara yangu ya pili kushiriki maonesho haya na nimeshafanya ziara pia
Mkoani hapa. Hakika ukarimu wenu kwangu hauelezeki. Mungu awabariki
sana. Hongereni pia kwa kuweza kumudu kwa ufanisi mkubwa uenyeji wa
maadhimisho haya kwa miaka mitatu mfululizo.
Kabla ya
kuendelea mbele na hotuba yangu niruhusuni niwape salamu kutoka kwa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Mheshimiwa Rais anawasalimu sana na anawatakia mafanikio
katika maadhimisho haya ya Sherehe za Wakulima Nane Nane 2020. Aidha,
Mheshimiwa Rais anawapongeza na kuwashukuru sana wakulima, wavuvi na
wafugaji wote kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuzalisha mazao
yanayotuhakikishia uhakika na usalama wa chakula, kipato na kukuza
ajira.
Nitoe
shukrani za pekee kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi,
Wizara za Kisekta, Wakuu wa Mikoa ya Kanda hii ya Ziwa Mashariki kwa
kazi kubwa ya maandalizi ya maonesho haya. Aidha, nichukue fursa hii
kuwapongeza wadau wote wa Maonesho haya kwa kujitokeza kwa wingi na
ubunifu wa kipekee katika Maonesho haya.
Natambua
changamoto za ugonjwa wa Korona ilivyoathiri maandalizi ya maadhimisho
kwa mwaka huu. Lakini hakika mmejitahidi sana ikizingatiwa muda mchache
wa maandalizi tangu pale Taifa letu tulipojiridhisha kupungua kwa
maambukizi ya COVID-19.
Kwa namna ya
pekee napenda kutambua uwepo wa wananchi wote kutoka mikoa mbalimbali
mliojitokeza kwa wingi wenu kutembelea mabanda ya Wakala, Taasisi za
Umma na Sekta Binafsi wakiwemo Wajasiriamali waliojitolea kuunga mkono
na kutambua juhudi hizi za Serikali. Waswahili husema shughuli ni watu
na kwa kadamnasi hii ya watu ninayoiona mbele yangu basi sina shaka
kusema kuwa shughuli yetu imefana.
Ndugu Wananchi, sote
tunafahamu umuhimu wa maadhimisho haya ambayo hufanyika kila mwaka kwa
lengo la kuwatambua Wadau Wakuu wa Sekta ya Kilimo ambao ni Wakulima,
Wafugaji, Wavuvi, Wanaushirika, Wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo,
uvuvi na maliasili kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kuendeleza
uchumi wa nchi yetu.
Maonesho haya
hutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wanaushirika kuona na
kujifunza matumizi ya teknolojia bora za kilimo, ufugaji na uvuvi kwa
ajili ya kuongeza tija na uzalishaji kwa uhakika wa chakula, kukidhi
mahitaji ya viwanda na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ninayo
taarifa kuwa pamoja na kuadhimishwa Kitaifa katika Kanda ya Ziwa
Mashariki hapa Mkoani Simiyu, Maonesho haya yanafanyika pia Kikanda
kwenye Kanda nyingine Saba (7) za maonesho ambazo ni Kanda ya Mashariki
(Morogoro), Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Magharibi (Tabora),
Kanda ya Kusini (Lindi), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini (Mbeya) na Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza). Lengo la kuwa na
mtawanyiko huo wa maonesho ni kuhakikisha kuwa wadau wengi wa sekta za
kilimo wanapata fursa ya kujifunza teknolojia kulingana na ikolojia ya
Kanda husika.
Ndugu Wananchi, nimepata
fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali na kujionea shughuli mbalimbali
zinazohusiana na ujasiriamali, uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi, ushirika, usindikaji wa mazao na utafiti wa kilimo na mifugo.
Nimefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Wizara za Kisekta na wadau
mbali mbali (Taasisi za utafiti, mabenki na sekta binafsi). Natambua
umuhimu wa ushiriki wenu kwenye maadhimisho haya kwa kuwa nyie ndio
chachu ya kukuza kilimo chetu kwa kushirikiana na Serikali katika
kutekeleza maeneo ya kipaumbele ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye
kilimo. Maeneo hayo ni
- Uimarishaji wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo;
- Udhibiti wa visumbufu;
iii. Matumizi ya zana bora za kilimo na huduma za ugani;
- Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji;
- Ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mazao ya kilimo;
- Utafutaji wa masoko; na
vii. Kufanya utafiti wa kilimo na kuzalisha teknolojia.
Aidha,
nimefarijika kuona muamko wa wananchi katika Kanda hii, pamoja na
mabadiliko ya ubunifu ya maonesho ya mwaka huu ikiwemo uwepo wa vituo
maalum vya kutoa habari na elimu kwa wazalishaji; maeneo/vyumba maalum
vilivyotengwa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo kuhusu kilimo
biashara, ufugaji, fursa za masoko, majadiliano baina ya wadau wa Sekta
ya Umma na Binafsi.
Huu ni
ubunifu mzuri na endeleeni kuukuza na kuundeleza. Ni imani yangu kuwa
wananchi watajifunza na kupata elimu na teknolojia mbalimbali katika
maonesho haya ya Nane Nane.
Nawapongeza sana washiriki wote.
Ndugu Wananchi, sote
tunatambua kuwa Sekta ya kilimo imeendelea kuwa ni mhimili muhimu
katika maendeleo ya uchumi wa taifa letu. Katika kipindi cha miaka
mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia bei za Mwaka
2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Shilingi trilioni 25.2 Mwaka
2015 hadi Shilingi trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile,
sekta hiyo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka
2018 na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa na hata kuchangia
upatikanaji wa malighafi za viwanda kwa wastani wa asilimia 65. Aidha,
kati ya mwaka 2015 hadi 2019 sekta ya kilimo imeendelea kukua kwa
wastani wa asilimia 5.2. Ukuaji huu wa Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
unahitaji usimamizi madhubuti katika Nyanja za kiutaalam, kisera na
kiutendaji.
Maadhimisho
ya Nane Nane ya mwaka huu yanaadhimishwa na kaulimbiu inayosema, “Kwa
Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora
2020.” Kaulimbiu hii inaendana na wakati huu tulionao tunapojipanga
kuelekea katika Uchaguzi Mkuu, wa Rais, Wabunge na Madiwani mwezi Oktoba
2020. Kaulimbiu hii inatoa hamasa kwa wananchi kuchagua viongozi bora
2020 watakaokuwa chachu ya kuleta mapinduzi katika Sekta za Uzalishaji
na kuinua uchumi na ustawi wa wakulima, wafugaji na wavuvi.
Ni dhahiri
kuwa maendeleo katika sekta mbalimbali hayawezi kupatikana iwapo hatuna
viongozi bora wenye kuweza kuweka na kusimamia sera na mipango madhubuti
itakayohakikisha kuwa wakulima wanawekewa mazingira rafiki na wezeshi
ya kufanya kilimo ikiwemo uhakika wa masoko kwa bidhaa zao.
Ni vyema kila
mmoja wetu kwa nafasi yake kuhakikisha kuwa tunachagua viongozi ambao
wataweka maslahi mapana ya taifa mbele na sio matumbo yao.
Ndugu Wananchi, nyote
ni mashahidi wa kazi na hatua mbalimbali tulizochukua katika awamu ya
tano ikiwa ni pamoja na kusimama bega kwa bega na wakulima katika
mnyororo mzima wa uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo.
Kupitia Ilani
ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015-2020 tumetekeleza ahadi
tulizozitoa kwa wakulima kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo
Awamu ya Pili (ASDP II) na kuwezesha kilimo kuchangia katika uchumi na
maendeleo ya Taifa letu, hususan katika maeneo ya:
- a)Usalama wa chakula na lishe,
- b)Ajira,
- c)Upatikanaji wa malighafi za viwanda
- d)Kuchangia katika kupunguza umaskini na kuongeza kipato cha wakulima.
Si lengo
langu kudurusu hotuba za Waziri wa Kilimo na Mawaziri wenzie wa Ufugaji
na Biashara walizozitoa wakati wa bajeti ya mwaka 2020/2021; ila
niruhusuni nigusie kwa uchache baadhi ya maeneo yaliyopata mafanikio
makubwa katika awamu ya tano ambayo ni:
- Usalama wa chakula na lishe; hivyo kupelekea nchi kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 121 na kuwa na wastani wa ziada ya takribani tani milioni mbili;
- Ongezeko la uzalishaji wa mazao makuu ya biashara yakiwemo pamba, kahawa, chai, pareto, tumbaku, korosho, mkonge na miwa kutoka tani 796,502 mwaka 2015/2016 hadi tani 1,148,126 mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 44.1. Aidha, kutokana na zao la korosho wakulima katika mkoa wa Lindi, Mtwara na Ruvuma hadi sasa wameshalipwa na Serikali zaidi ya shilingi bilioni 800.
- Upatikanaji wa pembejeo za kilimo; Tumeimarisha mfumo wa upatikanaji wa mbolea kwa kuanzishwa mfumo wa ununuzi wa pamoja (Bulk Procurement System-BPS) ambao umewezesha kuongeza upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,482 mwaka 2015/16 hadi tani 604,978 mwaka 2019/20. Vilevile tumefanya maboresho ya mifumo ya biashara ikiwemo ya usajili, uzalishaji na uagizaji wa pembejeo za uzalishaji wa mazao.
- Upatikanaji wa Mbegu bora umeongezeka kutoka tani 36,614.28 mwaka 2015/2016 hadi tani 76,725.52 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 110. Aidha, uzalishaji wa ndani wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20,604.97 mwaka 2015/2016 hadi tani 69,173.17 mwaka 2019/2020. Uzalishaji huo umepunguza uagizaji wa mbegu kutoka nje ya nchi kutoka tani 2,216,009.31 mwaka 2015/2016 hadi tani 7,552.35 mwaka 2019/2020 sawa na punguzo la asilimia 53.
- Maboresho ya kisera ya kodi na tozo; Tumefuta ushuru, tozo na ada chechefu 105 kati ya mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020 ambazo zimesaidia kumuondolea mkulima kero, adha, na kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea uzalishaji na uwekezaji katika Sekta ya kilimo.
- Upatikanaji wa Masoko; Tumeimairisha masoko ya mazao ya kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Serikali imeimarisha mfumo wa stakabadhi za ghala kwa kuhakikisha mazao yanauzwa kwa mfumo huo kupitia vyama vya ushirika ili kuwapatia wakulima masoko ya uhakika na bei zenye tija.
- Kuanzishwa kwa Bima ya Mazao na Kanzidata za wakulima; mfumo wa usajili wa wakulima na uanzishwaji wa Bima ya Mazao umeanzishwa kwa lengo la kumsaidia mkulima kujikinga na athari za majanga ya asili na mabadiliko ya tabianchi. Hadi kufikia Julai, 2020 jumla ya wakulima 1,325,799 wamesajiliwa kupitia mfumo maalum wa kusajili wakulima (Farmers Registration System-FRS). Nitoe wito kwa wakulima na wasimamizi kuendelea na zoezi hili muhimu lenye lengo la kuwatambua wakulima wote nchini ili kuwa na takwimu sahihi kwa ajili ya maamuzi sahihi kwa sekta ya kilimo.
- Upatikanaji wa viuatilifu; umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza upotevu wa mazao wakati wa kuvuna na baada ya kuvuna; Wizara, kupitia TPRI imesajili viuatilifu vipya 66.
- Ongezeko la matumizi ya zana bora za kilimo; matrekta makubwa na matrekta ya mkono yanayomilikiwa na wakulima yameongezeka kutoka 14,200 na 6,348 mwaka 2015 hadi 19,604 na 8,883 mwaka 2019 hii imesaidia kuzalisha zaidi na kurahisisha kilimo.
- Ongezeko la viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo; viwanda 145 vya usindikaji wa mazao ya mifugo vimejengwa vikijumuisha viwanda 33 vya nyama, viwanda 99 vya maziwa na viwanda 13 vya kusindika ngozi. Katika kipindi cha miaka minne jumla ya viwanda vipya 199 vya kuchakata mazao vimeanzishwa vikiwemo vya kubangua korosho, viwanda vya chai, viwanda vikubwa na viwanda vidogo vya kuchakata mkonge, kusindika matunda na mboga mboga.
- Maboresho katika sekta ya Mifugo na Uvuvi; Yamehakikisha kusimamia mpango wa matumizi bora wa ardhi kwa kuhakikisha ufugaji na uvuvi endelevu na unaohimili mabadiliko ya Tabianchi. Maboresho haya yameongeza uzalishaji wenye tija. Kwa upande wa Sekta ya Mifugo ilichangia asilimia 7.4 katika mwaka 2019/2020, katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2018/2019. Pia, Sekta ya Mifugo imekua kwa asilimia 5 kwa mwaka 2019/2020 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019. Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 katika pato la Taifa na imetoa ajira kwa Watanzania milioni 4.5. Vilevile, imechagia takriban asilimia 30 ya protini katika lishe inayotokana na wanyama.
- Utoaji wa mikopo; Serikali imeanzisha Dawati la Sekta binafsi linaloratibu wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi wanaohitaji huduma za mikopo, dhamana na bima. Kutokana na uwepo wa dawati hilo, katika mwaka 2019/2020 TADB iliidhinisha jumla ya Shilingi bilioni 26.1 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wazalishaji wa mifugo na wasindikaji wa nyama, wazalishaji na wasindikaji wa maziwa na wavuvi na wakuzaji viumbe maji. Aidha, benki ya TPB imefungua dirisha maalum la mikopo kwa wavuvi, na Shirika la Bima la Taifa (NIC) limeanzisha huduma ya bima ya mifugo itakayochochea ongezeko la mikopo.
Mbali na
hatua tajwa hapo juu, vilevile tumefanya maboresho kwenye utafiti,
huduma za ugani na mafunzo; uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti
Upotevu wa Mazao baada ya Mavuno, ongezeko la uzalishaji wa mazao ya
bustani; kuimarika kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko; kuimarika
kwa ushirika; kuimarika kwa kilimo cha umwagiliaji; ongezeko la ushiriki
wa vijana katika kilimo; matumizi bora ya ardhi; kuhuisha mifumo na
sera za kilimo.
Ndugu Wananchi, pamoja
na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita,
Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi bado inakabiliwa na changamoto
zifuatazo:-
- Upungufu wa masoko ya uhakika kwa mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kuyumba kwa bei za mazao.
- Mabadiliko ya tabianchi yamechangia kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa ya mimea na mifugo na hivyo kuchangia uzalishaji kuwa mdogo.
- Upungufu wa wataalamu katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
- Upungufu wa vitendea kazi kwa Maafisa Ugani hasa katika ngazi za chini kama vile usafiri, kompyuta.
- Baadhi ya viongozi wa Vyama vya Ushirika kutokuwa waadilifu na hivyo kupelekea ufanisi mdogo katika Sekta ya Ushirika.
- Matumizi duni ya pembejeo na zana kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Ndugu Wananchi, katika kutatua changamoto hizi Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi imejipanga kutekeleza mambo yafuatayo:-
- Kuendelea kuimarisha mifumo ya masoko kwa kuhakikisha inajenga miundombinu wezeshi na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ndani na nje ya nchi.
- Kuwajengea uwezo wananchi kuhusiana na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuhimiza matumizi ya zana za kilimo hifadhi ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
- Kuendelea kuajiri na kuwapatia vitendea kazi wataalamu kulingana na bajeti ya kila mwaka na kuwatambua watoa huduma binafsi za ugani.
- Kuhamasisha uanzishaji wa vituo vya kutoa huduma za zana za Kilimo (Agri-Mechanization hub) pamoja na uwezeshaji wa utengenezaji wa boti za uvuvi za kisasa kwa gharama nafuu. Kupitia utaratibu huu wakulima, wafugaji na wavuvi watapata huduma kwa ukaribu zaidi na hivyo kuongeza matumizi ya zana za Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
- Kuhamasisha wananchi kuchagua viongozi waadilifu na pia Serikali inaendelea kuwachukulia hatua viongozi wala rushwa, wabadhirifu na wasiozingatia maadili ya kazi. Hivyo kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu nawahimiza kuchagua viongozi waadilifu na waliotayari kuwatumikia wananchi bila kuzingatia maslahi yao binafsi.
Ndugu Wananchi, napenda
kutoa maelekezo ya kuzingatiwa wakati tunatekeleza shughuli za kilimo,
mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuwa na kilimo endelevu kinacholinda
mazingira yetu kama ifuatavyo: –
- Matokeo ya Tafiti
Watafiti wetu
wanafanya kazi nzuri sana na kupata mbegu bora zinazokinzana na magonjwa
pamoja na mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo,
matokeo ya tafiti hizo zilizo nyingi haziwafikii walengwa. Nitoe rai
kwa watafiti wote nchini kutoa matokeo ya tafiti zenu kwa Maafisa Ugani
na wadau wengine ili wakulima wetu wanufaike na matokeo hayo.
- Kilimo cha umwagiliaji
Kilimo cha
umwagiliaji ni muhimu sana na kinakabiliwa na changamoto ya mabadiliko
ya tabianchi. Kilimo hiki huwezesha eneo husika kulimwa mara mbili au
zaidi kwa mwaka. Hivi sasa eneo la umwagiliaji linalotumika
linakadiriwa kuwa Hekta 475,052 tu, hii ni kutokana na gharama kubwa
inayohitajika katika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa sekta binafsi itahakikisha kuwa miundombinu ya
umwagiliaji inajengwa na kusimamiwa vizuri. Aidha, naiagiza Wizara ya
Kilimo ambayo ndiyo inayoisimamia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutumia
fursa hii kutoa elimu ya utunzaji na uendeshaji endelevu wa miundombinu
ya umwagiliaji. (Nisisitize kuwa tuwaze Unyunyiziaji badala ya
umwagiliaji).
- Mifugo
Kadri mifugo
inavyoongezeka inahitaji eneo kubwa la malisho na maji ya kutosha. Kwa
bahati mbaya sana, ardhi haiongezeki. Hali hii, kwa namna moja ama
nyingine inaibua migogoro kati ya wakulima na wafugaji kutokana na ardhi
kutokidhi mahitaji ya pande zote mbili, wakulima na wafugaji. Kupitia
maonesho haya, Serikali inawaelekeza wataalam wa mifugo kutumia vizuri
nafasi hii, kutoa elimu bora ya utunzaji wa mifugo pamoja na malisho
kulingana na hali halisi ya maeneo tuliyonayo. Ni vyema mkatoa elimu ya
jinsi wafugaji wetu wanavyoweza kufanya ufugaji endelevu kwa kuvuna
mifugo yao na kujiongezea kipato.
- Uvuvi
Vitendo vya
baadhi ya wavuvi wanaovua samaki bila kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizowekwa, vilipelekea kupungua kwa samaki katika Maziwa
yetu, wote ni mashahidi jinsi tulivyokuwa na upungufu wa mavuno ya
samaki kutoka Ziwa Viktoria. Serikali imeboresha Kanuni za Uvuvi za
Mwaka 2009 ambayo imeelekeza zana za kutumia na aina ya uvuvi ili
kujenga uvuvi endelevu. Wizara ya Uvuvi muendelee kusimamia na
kudhibiti Uvuvi haramu kulingana na Sheria na taratibu zilizopo.
- Upandaji wa miti
Bado wananchi
wanafanya vitendo viovu vya ukataji miti kiholela hususan kwenye maeneo
ya hifadhi. Wizara yenye dhamana ya misitu na hifadhi isimamie na
kuwakuchukulia hatua wote wanaoendelea na kilimo kwenye hifadhi za
misitu. Agizo la kupanda miti 1.5m kwa kila Wilaya ni agizo halali
lililoelekezwa na Ilani yetu ya CCM ya mwaka 2015 katika Ibara 193 (a),
hivyo nikumbushe kila Mkoa, Wilaya na Halmashauri zetu kutekeleza agizo
la kupanda miti na kuhakikisha inamea.
- Kutunza vyanzo vya maji kwa kutofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji.
Ndugu Wananchi, Serikali
imeandaa utaratibu kwenye viwanja hivi vya Nyakabindi wa kuwakutanisha
wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na wakulima ili kujadili changamoto
na mafanikio katika shughuli zao. Natoa wito kwa wananchi wote
mnaoshiriki kwenye maonesho kushiriki kwenye majadiliano hayo.
Aidha, kila
Wizara na Taasisi za Umma na Binafsi ziwe mstari wa mbele kutafuta na
kuwakutanisha wadau wa sekta husika na kujadili ufumbuzi wa changamoto
zilizopo katika sekta husika. Suala la masoko, mifumo ya upatikanaji
mitaji, maeneo ya uwekezaji, miundombinu ya usafirishaji, uchukuzi na
uhifadhi viwe mojawapo ya maeneo ya kipaumbele katika majadiliano yenu.
Suala hili lifanyike katika viwanja vya maonesho kote nchini na wananchi
jitokezeni kwa wingi kutumia fursa hii. Vitengo na Idara za mawasiliano
zihusike katika kuhabarisha umma maonesho na elimu inayotolewa katika
viwanja hivi ili wadau wengi waweze kufikiwa.
Ndugu Wananchi, kabla
sijahitimisha hotuba yangu napenda kuzungumzia kidogo kuhusu Uchaguzi
Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.
Nawasihi wananchi mjitokeze kwa wingi kwenye mikutano ya kampeni
kuwasikiliza wagombea na sera zao ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi
siku ya kupiga kura.
Nayasema haya kwa
kuzingatia kuwa Maonesho ya Kilimo Nane Nane mwaka huu kaulimbiu yake
imelenga kuwakumbusha wakulima, wafugaji na wavuvi kote nchini kuchagua
Viongozi Bora. Serikali yenu imeweka mazingira wezeshi kwa wagombea wote
kufanya shughuli za siasa kwa amani na utulivu.
Niwaombe viongozi
wote wa vyama vya siasa kufanya kampeni zenu kwa kuzingatia taratibu
zinazotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Serikali haitosita kuchukua
hatua kali za kisheria kwa wote watakaoendesha kampeni zinazolenga
kujenga chuki na kuvuruga amani iliyopo. Napenda kuwasihi wananchi wote
kufika kwenye viwanja vya maonesho ya Nane Nane kote nchini kwa lengo
la kujifunza kanuni bora za uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na
uvuvi.
Baada ya kusema haya, nitamke rasmi kuwa Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane mwaka 2020 yamefunguliwa rasmi.
Mungu Ibariki Tanzania;
Mungu Wabariki Wakulima,
Wafugaji na Wavuvi
No comments :
Post a Comment