………………………………………………………………..
Na Mwandishi Wetu, Lindi.
Serikali Mkoani Lindi
kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC wameanzisha Dawati
maalum la uwekezaji ambapo masuala yote yanayohusu uwekezaji sasa
yanashughulikiwa kupitia katika dawati hilo ambalo lengo lake ni
kuwaweka karibu na kuwahudumia kwa upekee Wawekezaji wa Mkoa huo pamoja
na kutangaza fursa zilizopo.
Mkuu wa Wilaya ya
Lindi Mhe. Shaibu Ndemanga amesema uamuzi wa Serikali wa kuanzisha
dawati hilo Mkoani Lindi umekuja kufuatia kuwepo kwa fursa nyingi za
Uwekezaji ambapo kwa kushirikiana na TIC wameweza kuzitangaza.
Mhe. Ndemanga
aliyasema hayo wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi Mkoani Lindi, ambapo alisema
kufuatia Kongamano la Uwekezaji lililofanyika mwaka jana waliweza
kubaini masuala kadhaa ambayo yatasaidia kuongeza Wawekezaji.
“ Hapa Lindi
tumeanzisha Dawati la Uwekezaji ambalo linatuweka karibu sisi na
Wawekezaji wetu. Pia Ofisi ya TIC katika Kanda ya Kusini inafanya kazi
nzuri ya kuhamasisha uwekezaji hivyo kwa kushirikiana nao tumepanga
mambo makubwa na tutafanikiwa sana” alisema Mhe. Ndemanga.
Alisema Wawekezaji
wengi wanafika Mkoani humo ambapo sasa kupitia dawati hilo wataweza kuwa
karibu na kuwahudumia ipasavyo ambapo pia alizitaja baadhi ya Taasisi
zilizoonesha nia ya kuwekeza ikiwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaama
(UDSM) wanaotaka kujenga Chuo cha Utafiti wa Mazao, Chuo cha
Usafirishaji na Chuo Kikuu cha Kiisilamu cha Morogoro; ambavyo vyote
vimepata maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo husika.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania-TIC Dkt. Maduhu Kazi alisema hatua ya
Mkoa wa Lindi ya kutenga maeneo yenye miundombinu ya uwekezaji pamoja na
kuwa na kuanzisha Dawati la Uwekezaji ni ya kupongezwa na kuiomba Mikoa
mingine kuiga mfano wao.
“Mkoa wa Lindi
mnafanya kazi nzuri kwa kutenga maeneo, kuweka miundombinu na kuanzisha
Dawati la Uwekezaji, mmerahisisha kazi hizi kwa sababu sisi wote nia
yetu ni moja katika mbinu za kuvutia uwekezaji” Alisema Dkt. Kazi.
Aidha aliuomba Mkoa
huo kuwa na taarifa za maendeleo ya miradi na kufuatilia endapo
Mwekezaji aliyeweka nia ya kuwekeza na hajawekeza, ili kujua ni
changamoto gani alizokumbana nazo ili zisiweze kujirudia ambapo pia
aliwashauri kufuatilia kwa karibu miradi iliyo mbioni kuanza ili iweze
kuendelea na hivyo kukuza uchumi wa Mkoa na Nchi kwa ujumla.
No comments :
Post a Comment