Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ambaye pia ni Mjumbe wa TASAF, alipokuwa
akifungua warsha hiyo kwa viongozi ngazi ya Halmashauri.
………………………………………………………………………..
Na. Mwandishi wetu- DODOMA
Serikali
imewataka wawezeshaji wa ngazi ya Halmashauri watakaoshiriki zoezi la
kuhakiki kaya maskini kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini kufanya
kazi hiyo kwa weledi na kuhakikisha matumizi ya teknolojia yanakuwa na
manufaa kwa kazi waliyokabidhiwa.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji hao, Mjumbe wa Mfuko huo,
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, anayeshughulikia
masuala ya Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema matumizi ya vishkwambi
iwe chachu ya kubadili utendaji wa kazi zao wakati wa kuwasajili watu
wanaostahili kuingia katika mpango huo.
“Leo mnapokea
mafunzo na kuwezeshwa ili baada ya hapa mkawaeleweshe wananchi kusudi
zuri la serikali na nia njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
juu yao, kwamba mkono wake haujawaacha unawagusa mahali walipo.”
Amesema Gwajima na kuongeza,
“Hatutaki
kusikia tena kaya zisizo na sifa au hewa katika ardhi ya Tanzania, huku
Afisa mwenye dhamana ya usimamizi akiwa amekaa ofisini, ili hali
amezungukwa na kaya hewa, hilo haliwezekani” amekemea Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima
amesema watakaoshindwa kuzingatia itabidi watoe maelezo ya kina kwa
namna gani walisimamia na kutenda majukumu waliyopewa, na kama mtu
ataonekana ni sehemu ya kusababisha tatizo, basi gharama yake itakwenda
kwa aliyevunja sheria, taratibu na kanuni.
Katika jitihada
ya kuona mpango huo unakwenda vizuri wataalam wasimamizi wa kaya maskini
ngazi ya Halmashauri wamepatiwa vishkwambi, ili viweze kuwarahisishia
shughuli za utendaji, ambavyo vitatumika kuwabaini walengwa wenye sifa
na wasio na sifa.
“Ifahamike kwamba
wananchi wengi katika maeneo yao wanafahamiana, hivyo hata kubaini nani
alifanya tofauti kwa kuingiza mtu asiyehusika itakuwa rahisi kwa
kutumia vishkwambi hivi kwa maana itajulikana wazi mtaalamu
aliyeidhinisha sifa za mlengwa husika anayedaiwa kuwa ni hewa. Kwa
mantiki hii vishkwambi vikawe ndio chachu ya maboresho,” alisema Dkt.
Gwajima.
Amewataka
watalam hao kuwatumia vyema, Watendaji Vijiji na Mitaa ili kufanikiwa
katika kutekeleza majukumu yao kwani wao ndio wanaoishi na jamii kwa
karibu.
Mjumbe huyo
wa TASAF, Dkt. Gwajima, amesema atashangazwa sana na wakuu wa Idara
ambao ni mahiri katika kuelezea mafanikio na kutambua takwimu za maeneo
yao ya kazi halafu washindwe kutambua walengwa wa mpango wa kunusuru
kaya maskini kwenye eneo lake analosimamia mfano, wewe ni Afisa Mifugo
ujue idadi ya mifugo yote ushindwe kujua idadi ya mifugo inayomilikiwa
ba walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini” alisema Dkt. Gwajima.
“Mathalani wewe
ni mkuu wa idara ya Afya, Kilimo, Ustawi wa Jamii, Mwanasheria, nk.
unakwenda kufanya shughuli zako lakini suala la TASAF umeliweka pembeni
na halitoki kwenye taarifa zako hilo litakuwa ni tatizo” Amesema Dkt.
Gwajima.
Mafunzo hayo
kwa wataalam hao katika mpango wa TASAF kipindi cha pili cha awamu ya
tatu yamefanyika katika Shule ya Sekondari Umonga jijini Dodoma.
No comments :
Post a Comment