Thursday, August 13, 2020

TAMKO KWA WANAHABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2020

Dar es Salaam Agost 12, 2020. Wakati macho na masikio ya Watanzania yakiisubiri kwa hamu Oktoba 28 ambayo ni siku ya uchaguzi mkuu nchini, Chama cha Wanahabari Wanawake

Tanzania (TAMWA) Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) pamoja na Global Peace Foundation (GPF) inavitaka vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi, kuondoa changamoto zote zinazochagiza ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

Uchaguzi Mkuu unafanyika wakati ambapo kati ya wagombea 16 waliochukua fomu kugombea urais, wapo wanawake wawili mpaka sasa ambao ni Queen Cathbert Sendinga wa Chama cha ADC, na Cecilia Augustino wa Demokrasia Makini walioteuliwa na vyama vyao kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi huo. Kadhalika, wapo wanawake watano wanaowania umakamu wa Rais, katika mchakato huu wa uchaguzi.

Lakini TAMWA, WiLDAF  na GPF  taasisi ambazo malengo yake ni kuwepo kwa jamii yenye amani, inayoheshimu haki za binadamu kwa mtazamo wa kijinsia, na amani zimeona ni vyema kuikumbusha jamii, wadau wa masuala ya siasa na ya jinsia  kuzifanyia kazi changamoto zinazochangia ushiriki duni wa wanawake katika siasa.

 TAMWA WiLDAF  na GPF  chini ya ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake Afrika, (AWDF) kupitia mradi wa ‘Wanawake Sasa’ imeendesha midahalo mbalimbali ya wanawake kutoka  vyama vya siasa ,wakiwamo wanawake wanasiasa, viongozi wa dini na kubaini kuwa bado kuna changamoto  zinazopelekea ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa.

Midahalo tuliyofanya  katika  kanda za Dodoma, Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam, iliibua changamoto zinazowakabili wanawake katika siasa ikiwamo lugha dhalilishi  zinazowavunja moyo wanawake  wanaogombea au walio katika nafasi za uongozi pamoja na familia zao kuwania nafasi mbali mbali za uongozi.

“Wanawake wanaogombea nafasi za uongozi, hukutana na changamoto  ya lugha dhalilishi wakati wa kampeni, na hata wakati wa utendaji wao wa kazi ili tu kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma. Kama tunataka uchaguzi wa haki na wa kidemokrasia, ni muhimu kwa tume ya uchaguzi na vyombo vya usalama kupiga marufuku na kutoa adhabu kali kwa wanasiasa watakaotoa lugha hizi dhidi ya wanawake,” Rose Reuben, Mkurugenzi TAMWA.

Katika midahalo hiyo, TAMWA , WiLDAF  na GPF  tumebaini kuwepo kwa rushwa ya kifedha katika shughuli za kawaida za siasa na hasa wakati wa chaguzi mbali mbali za ndani ya vyama, serikali za mitaa na uchaguzi mkuu. Hii ni pamoja na tabia za wajumbe wanaotegemewa kupiga kura kuwa na hulka ya kudai au kujenga mazingira ya kupewa “kitu kidogo” ili waweze kutoa ushirikiano kwa mgombea. Hii inaathiri  wanawake ambao wengi wao hawana kipato cha kutosha hasa wanawake vijana.

Pia tumebaini uwepo wa vitendo vya kuomba au kutengeneza mazingira ya rushwa ya ngono kwa baadhi ya wanaume wenye dhamana za kusimamia michakato ya chaguzi au mamlaka ndani ya vyama vya siasa.Changamoto hiyo husababisha wanawake kudhalilishwa na kuharibiwa ndoto zao za kisiasa na wakati mwingine familia au wenzi wao kuwazuia kushiriki katika siasa.

Hayo na mengine mengi, yanachangia wanawake, kuvunjika moyo na hivyo kutoshiriki shughuli za siasa au kukosa nafasi za uongozi pale wanapokuwa na msimamo wa kutotoa rushwa.

Katika hili tunapenda kutoa rai kwa wanawake wenzetu kukataa kabisa kudhalilishwa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa ya fedha au ngono na pia tunashauri jumuiya za wanawake ndani ya vyama vya sisasa kuvunja ukimya na kuhakikisha hoja za rushwa katika siasa inazungumzwa katika kila vikao vya jumuiya na vikao vingine muhimu.

Pia tunaviomba vyama vya siasa viweke utaratibu madhubuti na wa siri wa kutoa taarifa za vitendo hivi na kuwe na kamati huru ndani ya vyama zisizofungamana na yeyote zitakazoratibu upokeaji, ufuatiliaji na utoaji adhabu kwa wale ambao bado wanaendekeza vitendo hivi vya kuwadhalilisha wanawake.   

Changamoto nyingine zilizoibuliwa katika midahalo hiyo,  ni Ilani za vyama vya siasa ambazo hazitoi nafasi kwa wanawake kuwa viongozi na kupata nafasi ya kugombea katika majimbo. Tumebaini wanawake wengi wanashindwa kushiriki uchaguzi kwa kutopata baraka hii kuanzia ndani ya vyama.

Kadhalika tunapenda kuwaasa wanawake kuepuka kugawanywa na zile kauli kuwa, ‘hawapendani’ badala yake waendelee kushirikiana na kupeana fursa mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii.

“Kauli hizi za kuwa ‘wanawake hatupendani’ si za kweli bali zimekuwa zikitumika katika jamii kuwagawa wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi,” Reuben

Tunatarajia kuwa serikali, wadau wa siasa, vyombo vya usalama vitazingatia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DK John   Pombe Magufuli ya kuwepo kwa mazingira wezeshi kwa wanawake katika uchaguzi mkuu na katika nafasi za uongozi na maamuzi. Pia tunampongeza kwa kuendelea kumchagua Mama Samia Suluhu kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu ujao.

Tungependa kumalizia kwa kusisitiza kauli zilizotolewa na Rais, viongozi wa vyama mbali mbali na tume ya taifa ya uchaguzi kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa ni  huru, haki na wa amani.

Tunawakumbusha wagombea wote kuhakikisha kuwa hawatoi kauli zozote za uvunjifu wa Amani, kuchochea vurugu, kuwagawa watu kwa dini au makabila yao au matusi na udhalilishaji wa kijinsia kwa wagombea wengine.

Wakati huo, TAMWA, WiLDAF na GPF  inaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendelea kuhimiza uchaguzi huru, wa haki na usawa na kutengenezwa kwa mazingira sawa ya ushindani kwa wagombea wote.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ubariki Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2020.

No comments :

Post a Comment