Tuesday, August 11, 2020

SIMA AELEKEZA WACHIMBAJI WADOGO KUSAJILIWA

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima

akiongea na Mkuu wa Wilaya ya Songwe Bw. Samuel Jeremia Opulukwa (wa pili
kushoto) wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za uhifadhi wa Mazingira katika
Wilaya hiyo. Kulia ni Prof Esnat Chaggu Mwenyekiti wa Bodi – Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC na Dkt. Samuel Gwamaka Mkurugenzi Mkuu
– NEMC.


Prof Esnat Chaggu Mwenyekiti wa Bodi – Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira NEMC akisisitiza jambo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua
shughuli za uhifadhi wa Mazingira katika Wilaya ya Songwe hii leo.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akitoa maelekezo kwa Bw Honest Mrema Meneja Mkuu wa Mgodi wa Shanta mara
baaada ya Naibu Waziri Sima kutembelea mgodi huo kukagua bwawa la kuhifadhi tope
sumu litokanalo na uchenjuaji wa dhahabu mgodini hapo.


Dkt. Samuel Gwamaka Mkurugenzi Mkuu, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira – NEMC akisalimiana na baadhi ya watumishi wa mgodi wa Shanta Gold
Wilayani Songwe akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua uzingatiaji wa Sheria ya
Mazingira ya Mwaka 2004.

……………………………………………

Na Lulu Mussa ,Songwe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima ameuagiza

uongozi wa Wilaya ya Songwe kuwabaini, kuwasajili na kuunda vikundi vya wachimbaji wadogo wasio rasmi ili waweze kutambulika na kufaidika na mikopo midogomidogo inayotolewa na Serikali hapa nchini.

Ameyasema hayo  leo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa
Songwe hususan Wilaya ya Songwe na kubaini changamoto ya wachimbaji wadogo wanaoharibu mazingira kutokana na uchimbaji holela.

“Ni lazima mchukue hatua za haraka za kuwatambua wachimbaji hawa kwa lengo lakuwasajili na kuanzisha kanzi data itakayosaidia katika zoezi la utoaji wa elimu ili kunusuru mazingira” Sima alisisitiza.

Waziri Sima amesisitiza kuwa ni vema pia Wilaya ya Songwe ikaanzisha vikundi vya mazingira na kuhamasisha matumizi ya Sheria ndogondogo katika maeneo yao.

Aidha akitoa taarifa ya hali ya Mazingira katika Wilaya hiyo Mkuu wa Wilaya ya Samuel Jeremia Opulukwa amesema Wilaya yake inakabiliwa na changamoto kubwa za uchomaji wa misitu unaohatarisha maisha ya viumbe hai na ikolojia ya eneo hilo.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka ametoa wito kwa watafiti wa madini katika eneo hilo kutoa taarifa rasmi katika ngazi ya Wilaya ili kuepuka uharibifu wa mazingira unaofanywa na watafiti hao kwa kuchimba kiholela kwa lengo la kutafuta dhahabu.

Pia, Naibu Waziri Sima ametembelea Mgodi wa Shanta na kuagiza uongozi wa mgodi huo kutoa elimu kwa jamii inayozunguka mgodi huo juu ya namna bora ya uchimbaji wa madini kwa njia bora na salama kwa mazingira.

“Kwa kuwa mgodi huu unatumia teknolojia ya kisasa zaidi, natoa rai kwa mgodi
kuhamisha teknolojia hii kwa wachimbaji wadogo wadogo ili wananchi pia wanufaike” Sima alisisitiza.

Mheshimiwa Mussa Sima yuko Mkoani Songwe kwa ziara ya kikazi na ametembelea Wilaya ya Songwe na kukagua usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ambapo kesho atawasili Mkoani Mbeya.

No comments :

Post a Comment