Waziri wa Nishati Dkt Medard
Kalemani (kushoto) akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania,
Frederic Clavier (kulia) pamoja na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Norway hapa
nchini. Kikao hicho kilichojadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya
nishati, kilifanyika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe kutoka Balozi za Ufaransa
na Norway nchini Tanzania, wakiwa katika kikao na Waziri wa Nishati Dkt
Medard Kalemani na Ujumbe wake (hawako pichani). Kikao hicho
kilichojadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati,
kilifanyika Ofisi ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Viongozi na Wataalamu
kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO), wakiwa katika kikao cha Waziri mwenye
dhamana, Dkt Medard Kalemani na Ujumbe kutoka Balozi za Ufaransa na
Norway nchini Tanzania (hawako pichani). Kikao hicho kilichojadili
masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati, kilifanyika Ofisi ndogo
za Wizara, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati Dkt Medard
Kalemani (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Ufaransa
nchini Tanzania, Frederic Clavier (kushoto) na Bjorn Midthun, ambaye ni
Afisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa Norway hapa nchini. Waziri alifanya
kikao na Ujumbe husika, Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam,
kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta ya nishati.
………………………………………………………………………………………..
Veronica Simba – Dar es Salaam
Serikali ya
Tanzania imezishukuru nchi za Ufaransa na Norway kwa mchango wake...
mkubwa
walioutoa na wanaoendelea kuutoa katika kuwezesha utekelezaji wa miradi
ya umeme vijijini.
Waziri wa Nishati
Dkt Medard Kalemani alitoa shukrani hizo jijini Dar es Salaam, Agosti
27, 2020 wakati wa kikao baina yake na Balozi wa Ufaransa hapa nchini,
Frederic Clavier pamoja na Bjorn Midthun, ambaye ni Afisa Mwandamizi
kutoka Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.
“Mmefanya kazi
nzuri sana katika kutuwezesha kutekeleza miradi ya umeme vijijini.
Ushirikiano wenu umetuwezesha kufikia hatua hii tuliyopo leo. Kwa niaba
ya Serikali, ninawashukuru sana,” alisisitiza Waziri.
Akidadavua hatua
iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Dkt Kalemani
alisema hadi sasa zaidi ya vijiji 9,512 ambavyo ni zaidi ya asilimia 85
ya vijiji vyote 12,268 vilivyopo nchini, vimeshafikiwa na umeme.
Aidha, aliueleza
Ujumbe huo kutoka Ufaransa na Norway kuwa vitongoji takribani 25,000
vimekwishafikishiwa umeme kati ya 64,339 vilivyopo nchini hivyo
ameziomba nchi hizo kuendelea kutoa mchango wao katika kuwezesha
kutekeleza kazi iliyobaki ya kupeleka umeme kwa vijiji na vitongoji
vilivyosalia nchini.
Alisema umeme ni
injini ya uchumi huku akipambanua kuwa pasipo umeme wa uhakika,
haiwezekani kwa nchi yoyote kuwa na maendeleo ya kiuchumi.
Aliongeza kuwa
jitihada za makusudi zinazoendelea kufanywa na Serikali hususani katika
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, pamoja na mambo mengine,
ndizo zimeiwezesha Tanzania, kuingia katika uchumi wa kati.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti katika kikao hicho, Balozi Clavier pamoja na Bwana
Midthun, walimhakikishia Waziri Kalemani kuwa Serikali za nchi zao
zitaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha miradi mbalimbali
ya umeme.
Pamoja na kueleza
utayari wa kuendelea kuisaidia Tanzania, Viongozi hao walisisitiza
umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika kutekeleza miradi husika
ambapo Waziri Kalemani amewahakikishia kuwa, ubora na uaminifu ni
masuala yanayopewa umuhimu wa hali ya juu.
Kikao hicho pia
kilihudhuriwa na Mwakilishi wa Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu,
Mhandisi Styden Rwebangira, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga na baadhi ya Maafisa Waandamizi
kutoka REA, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Balozi za Norway na
Ufaransa hapa nchini.
No comments :
Post a Comment