Monday, August 17, 2020

BILIONI 100 KUPELEKA UMEME PEMBEZONI MWA MIJI

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika Shule ya Sekondari Moivaro, wilayani Arusha, Agosti 16, 2020. Wa pili kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji.Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, akiwahamasisha wananchi wa Mtaa wa Bondeni Kati, Kata ya Terrat, wilayani Arusha, kulipia shilingi 27,000 tu ili waunganishiwe umeme. Waziri alikuwa katika ziara ya kazi wilayani Arusha, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Agosti 16, 2020.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji akizungumza, wakati wa hafla fupi ya kuwasha umeme katika Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat. Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia-Meza Kuu) ndiye aliwasha rasmi umeme katika Shule hiyo akiwa katika ziara ya kazi, Agosti 16, 2020.

***************************************

Veronica Simba – Arusha

Serikali imetenga shilingi bilioni 103.8 kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo yaliyo

pembezoni mwa majiji, mikoa, manispaa na miji, nchi nzima.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, amebainisha hayo kwa nyakati tofauti leo, Agosti 16, 2020 alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani Arusha.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuwasha umeme katika Shule ya Sekondari Moivaro na baadaye Shule ya Sekondari Nyahiri Terrat, Dkt Kalemani amesema kuwa Serikali inaendelea kuwaunganishia umeme wananchi wa maeneo ya aina hiyo nchini kote kwa gharama ya shilingi 27,000 tu kama ilivyo kwa vijijini.

Amesema, Mpango huo wa Serikali ni kutokana na uhalisia kuwa maeneo hayo kwa kiasi kikubwa, yanashabihiana na yaliyoko vijijini, ambapo asilimia kubwa ya wakazi wake wana kipato kidogo.

“Tulikaa tukaona maeneo haya yaliachwa muda mrefu bila kuwa na miundombinu ya umeme. Tukaona tuwapunguzie gharama kutoka mlivyokuwa mnalipa zamani shilingi 177,000 na katika baadhi ya maeneo 380,000 hadi shilingi 27,000 tu.”

Akizungumzia Wilaya ya Arusha, Waziri Kalemani amesema kuna mitaa takribani 26 iliyo pembezoni mwa Mji na kwamba Serikali ilianza kuipeleka umeme kutoka mwaka 2018.

Amempongeza Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Arusha, Mhandisi Herin Muhina, kwa kazi nzuri anayoifanya na kumwagiza atumie muda wa miezi mitatu kuanzia hivi sasa, kukamilisha kazi ya kupeleka umeme katika mitaa yote iliyo pembezoni mwa Mji, ambayo haijafikiwa na huduma hiyo.

Aidha, Waziri amekiri kufurahishwa na Uongozi wa Shule ya Sekondari Moivaro kuona umuhimu wa kulipia gharama za kuunganishiwa umeme na kupata huduma hiyo, ikiwa na mwaka mmoja tu tangu ianzishwe.

Ametoa rai kwa viongozi wengine katika maeneo mbalimbali nchini, kuiga mfano huo kwa kuhakikisha taasisi zote za umma zinapewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ili kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi.

Kuhusu suala la wananchi kulipia nguzo ili waunganishiwe umeme, Dkt Kalemani ameendelea kusisitiza msimamo wa Serikali kuwa ni marufuku kwa kitendo hicho na ametoa tahadhari kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maagizo hayo, atachukuliwa hatua kali.

Amesisitiza wananchi kuendelea kulipia huduma ya umeme pasipo kusubiri nguzo akisema hilo siyo jukumu lao. “Wewe lipia kisha udai umeme,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri amegawa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wao kwa Taifa kupitia kazi wanayoifanya katika kuhabarisha na kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali, yakiwemo ya sekta ya nishati.

Aidha, amegawa vifaa hivyo kwa shule alizoziwashia umeme pamoja na walimu wake huku akielekeza kuwa vitumike kuwaunganishia umeme wa gharama nafuu ambao haulazimu kutandaza mfumo wa nyaya katika jengo husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kenan Kihongoji, amempongeza Waziri Kalemani kwa uchapakazi wake hususan katika kuhakikisha wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kote, wanapata huduma ya umeme.

“Uchapakazi wako unadhihirisha kwa vitendo kuwa unamuunga mkono Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa John Magufuli katika kuwatumikia Watanzania ili kuhakikisha wanajipatia maendeleo ya kiuchumi.”

Katika ziara hiyo, Waziri aliambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga na wataalamu wengine mbalimbali kutoka wizarani na taasisi hizo.

No comments :

Post a Comment