Waziri
wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akizungumza
jambo wakati akitizama mtambo wa kutengeneza kamba katika kiwanda cha
Katani cha Kisangara kinachomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji
kilichopo wilayani Mwanga,wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa wilaya ya
Mwanga ,Thomas Apson akifuatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
ya Mwanga ,Zefrin Lubuva na kulia ni George Mwamakula -Meneja.
Waziri
wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akitizama bidhaa
inayotumika kutengeneza magunia inayotokana na zao la Katani
alipotembelea kiwanda cha Katani cha Kisangara wilayani Mwanga
kinachomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji,wengine katika picha
kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga ,Zefrin
Lubuva na kushoto mwa waziri kairuki ni George Mwamakula -Meneja.
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akizungumza jambo na uongozi wa kiwanda hicho.
Baadhi
ya wafanyakazi wa kiwanda cha Katani cha Kisangara wakiendelea na
shughuli za ukusanyaji wa bidhaa inayotumika kutenegeneza kamba na
magunia.
Na Dixo Busagaga ,Mwanga
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki, amewataka
wananchi, kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya,
kwa ajili ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu, kuwekeza katika
tasnia ya Mkonge, ambayo imeonekana kuwa na chachu kubwa ya maendeleo.
Kairuki,
alitoa rai hiyo , mara baada ya kutembelea Shamba la Mkonge la
Kisangara,lililoko chini ya Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL) Wilaya
ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, na kupewa taarifa ya uwepo wa upungufu wa
mashine kwa ajili ya kuchakata zao hilo, ambapo alisema ni fursa kubwa
kwa wananchi katika kujipatia kipato
Alisema
wananchi wanaweza wakajiunga katika vikundi kama ambavyo imekuwa
ikielekezwa na Halmashauri, na kupewa mkopo, ambao watauwekeza katika
ununuzi wa Mashine ya kuchakatia Mkonge,ijulikanayo kwa jina maarufu
kama Corona na kuweza kupiga hatua kimaendeleo.
“Nimeelezwa
kuwa, kuna upungufu wa mashine za kuchakata Mkonge,hivyo wakati
mwingine mkonge upo ila hakuna mashine ya kuchakata, Sasa viongozi wa
Halmashauri na hata Mkoa, tuendelee kuwahamasisha wananchi wawekeze
katika tasnia ya zao la mkonge, ambako kumeonekana kuwa na fursa nzuri”
alisema Kairuki na kuongeza kuwa,
“Tunaweza
pia kutumia fursa ile ya mikopo ya wanawake,Vijana na watu wenye
ulemavu,kuona ni namna gani kikundi cha pamoja au vikundi vya ushirika
vinaweza kuwekeza katika Corona (Mashine ya kuchakatia Mkonge) wananchi
wachangamkie fursa hii,ili kumaliza tatizo la upungufu wa mashine hizi”
Aidha
alitumia pia nafasi hiyo, kuwataka Viongozi wa Halmashauri,kutoa elimu
kwa wananchi na kuelezea fursa zilizopo katika Mkonge,ili kupanua wigo
wa uwekezaji katika kilimo hicho, kwa kuwa mahitaji ya Mkonge bado ni
makubwa nchini na hata duniani.
“Mahitaji
ya Mkonge bado ni makubwa, hivyo tuendelee kuhamasisha wananchi na
kuwapa elimu ili wale wenye maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho, waweze
kuwekeza huko,lakini pia tunaendelea kukaribisha wawekezaji wengine,
kuingia katika uchakataji wa zao hili, kwani kwa sasa Vipo viwanda zaidi
ya 11 vikubwa na vya kati vya kuchakata mkonge,na viwanda vidogo zaidi
ya 70 kwa ajili ya uchakataji wa zao hili”alisema.
Awali
akizungumza Meneja wa kituo cha uwekezaji Kanda ya Kaskazini, Daudi
Riganda, aliutaka uongozi wa shamba hilo la Mkonge, kuongeza uzalishaji,
na kuwekeza zaidi katika zao hilo, ili kuweza kutengeneza faida.
“Bado
hatujaridhika na namna ambavyo muwekezaji ameweza kutumia fursa ya
uwekezaji katika kilimo hiki cha mkonge,ikilinganishwa na rasilimali ya
Ardhi aliyo nayo na hali ya hali ya hewa iliyopo,hivyo
ningeshauri,wawekezaji watakaopewa nafasi ya kuwekeza katika kilimo cha
Mkonge, waongeze uzalishaji na kuwekeza kwa tija zaidi”alisema.
Mkuu
wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson,alisema kwa sasa wanajipanga kutoa
elimu na kuhamasisha wananchi, kujiingiza katika Kilimo cha Mkonge,ili
kuweza kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa zilizopo nhini.
“Kuna
haja ya sisi kama Wilaya, kukaa na Idara ya Kilimo na Biashara,kuona ni
namna gani tunahamasisha wananchi, kwani changamoto yetu ni kuwapata
watu ambao wataitumia mikopo na kuirejesha kwa wakati,sasa tunakwenda
kuhamasisha Kilimo na kutoa fursa kwa wananchi, kwani kufanikiwa kwetu
kama viongozi ni kuona tunaboresha maisha ya viongozi tunao
waongoza”alisema
No comments :
Post a Comment