Mwezeshaji
wa zoezi la uhakiki wa taarifa za kaya maskini kutoka mfuko wa
maendeleo ya jamii Tasaf wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mbwana Boma
kushoto, akipata taarifa kutoka kwa Awetu Kulangwa ambaye ni mmoja kati
ya walengwa wanaopokea ruzuku ya fedha kutoka Tasaf katika kijiji cha
Nakayaya Mashariki wakati wa zoezi la uhakiki wa taarifa za wanufaika wa
mpango huo ambapo jumla ya kaya 13,752 zimehakikiwa taarifa zao
wilayani Tunduru.
*******************************
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
WAKATI Mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma ukikamilisha zoezi la uhakiki kwa wanufaika wa mpango wa
kunusuru kaya maskini,baadhi ya Tunduru
walengwa wakiwemo walemavu wameiomba Serikali kuongeza kiwango cha fedha ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Wakizungumza wakati wa zoezi la uhakiki wa kaya maskini katika kipindi cha pili awamu ya tatu katika kijiji cha Nakayaya Mashariki walengwa hao walisema, kiwango kinachotolewa na Serikali kupitia Tasaf ni kidogo na hakitoshelezi kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
John Nchunda na Mohamed Thabit, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha inazotoa kama ruzuku ya kaya maskini kwa kuwa gharama za maisha kwa sasa zimepanda,kwa hiyo ni vizuri serikali ikaangalia suala hilo.
John Nchunda alisema, licha ya nia njema ya Serikali kuwasaidia watu maskini wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha,hata hivyo haina budi kuangalia upya tena kwa jicho la huruma kutokana na kupanda kwa gharama.
Naye Aidan Ndumbaro, ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka watu maskini juu ya suala la kutoa fedha za ruzuku ambazo tangu ilipoanza mpango huo zimesaidia sana kubadili hali zao za maisha.
Aidha, ameunga mkono mpango wa kuhakiki upya kaya maskini unaokwenda kuboresha taarifa za walengwa kwa sababu utamaliza tatizo la ubabaishaji uliokuwa unafanywa na baadhi ya watu wasiohusika kupokea fedha zinazotolewa na Serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii(Tasaf).
Alisema, zoezi la uhakiki litasaidia kupata walengwa husika na kuondoa malalamiko ya kuwepo kwa watu wanaojinufaisha kupitia mpango huo ambao hawana sifa na hawastahili kuendelea kupokea ruzuku.
Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf wilaya ya Tunduru Muhidin Shaibu alisema,lengo la uhakiki huo ni kuboresha taarifa za kaya maskini ili kubaini kama zinafanana na taarifa za awali za walengwa hao.
Alisema, katika zoezi hilo lililofanyika kwa kutumia vishikwambi(tablet)kupata taarifa za walengwa,wawezeshaji wamefanikiwa kuzifikia jumla ya kaya 13,751 zilizopo katika mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani Tunduru.
Alisema, katika zoezi la uhakiki wanaangalia taarifa za kaya ili kujiridhisha kama kuna zilizoongezeka ua kupungua,watoto wanaokwenda shule na wanaohudhuria kliniki ambao wanapata ruzuku ya Serikali.
Alisema,kabla ya kuanza kwa zoezi hilo wawezeshaji ambao ni watumishi wa Serikali walipewa mafunzo siku mbili ya kuwajengea uwezo namna ya kupata taarifa na kutumia vishikwambi na walifika katika vijiji 88 vyenye wanufaika kwa ajili ya kufanya uhakiki wa taarifa zao.
Shaibu alisema, zoezi hilo limefanyika kabla ya kuanza upya kutoa fedha za ruzuku kupitia utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa kunusuru kaya maskini katika wilaya hiyo.
Alisema, kimsingi uhakiki huo utasaidia kufanya marekebisho ya taarifa pamoja na kutambua usahihi wa taarifa za walengwa kama ziko sawa sawa kama zilizokusanywa katika awamu zilizopita.
Alisema, zoezi la uhakiki linalenga kupata taarifa sahihi za walengwa ambao wataendelea kupokea ruzuku na utamaliza baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa utambuzi wa kaya katika awamu zilizopita.
No comments :
Post a Comment