Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza na viongozi
pamoja na wananchi wa mkoa wa Kigoma waliojitokeza kushuhudia uzinduzi
rasmi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma jana.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza
kushuhudia uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma uliofanywa na
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akikagua moja ya majalada la ardhi
katika ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma alipokwenda kuizindua rasmi. Kulia
ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga na
wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Kigoma Chediel
Mrutu.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimkabidhi hati ya ardhi mmoja wa
wananchi wa mkoa wa Kigoma wakati wa uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi
mkoani humo jana. Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali
Mstaafu Emanuel Maganga.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na
wananchi wa mkoa wa Kigoma waliokabidhiwa hati za ardhi wakati wa
uzinduzi rasmi wa ofisi ya ardhi mkoani humo jana. Wa nne kushoto ni
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimsikiliza mkazi wa
Kigoma aliyewasilisha malalamiko kwake wakati wa uzinduzi rasmi wa ofisi
ya ardhi mkoani humo jana. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA
ARDHI)
******************************
Na Munir Shemweta, WANMM KIGOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Maafisa Mipango Miji nchini
kuzisaidia wilaya kuhakikisha maeneo yote ya vijiji yanayochipukia kuwa
miji anapelekewa ili ayatangaze kuwa maeneo ya Mipango Miji.
Lukuvi alisema hayo jana wakati
akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi
wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini. Tayari ofisi za ardhi
kwenye mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Iringa, Njombe, Songwe,
Rukwa, Katavi zimezinduliwa.
Alisema, wizara yake kwa sasa ina
mpango wa kupima kila kipande cha ardhi nchi nzima sambamba na
kuhakikisha maeneo yanapangwa ili kuepuka ujenzi holela.
‘’Maeneo yote ambayo vijiji
vinachipukia nileteeni nitangaze kuwa maeneo ya mipango miji na maafisa
mipango miji mzisaidie wilaya katika hili’’ alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, baada
ya maeneo hayo ya vijiji vinavyochipukia kutangazwa maeneo ya mipango
miji wananchi wake hawatapewa tena hati za kimila na badala yake
watapata hati za miaka 99 kama wanavyopata watu wanaoishi mijini.
Alisema, mpango wa kuyatangaza
maeneo hayo ya vijiji inavyochipukia siyo lazima uanzie wizarani bali
Maafisa Mipango Miji katika halmashauri za wilaya wanatakiwa kuyawahi
mapema ili kuepuka ujenzi holela.
Akizungumzia utendaji kazi katika
ofisi za ardhi za mikoa, Waziri Lukuvi alisema, ofisi hizo zimekamilikia
kutokana na kuwa na wataalamu wa fani zote kama vile Upimaji, Uthamini,
Mipango Miji pamoja na Usaji wa Hati na kubainisha kuwa vifaa vya
kisasa vya upimaji navyo vimepelekwa kwenye ofisi hizo na sasa mwananchi
halazimiki kufika Wizarani kwa kuwa huduma zote zinapatikana ofisi za
mikoa.
Kuhusu upungufu wa watumishi wa
sekta ya ardhi kwenye halmashauri za wilaya, Lukuvi alisema kuwa, baada
ya kupeleka watumishi ngazi ya mkoa, zoezi linalofuata ni kuwapanga upya
watumishi katika ngazi ya halmashauri kwa kuzingatia wataalam wa fani
zote.
Akigeukia suala la utoaji hati
miliki za ardhi nchini, Lukuvi ameagiza wananchi wote waliopimiwa ardhi
kwenye mkoa wa Kigoma kwenda ofisi za halmashauri za wilaya kuomba
kutengenezewa hati na kubainisha kuwa, atakayeshindwa baada ya siku
tisini atapelekewa hati ya malipo na kudaiwa kuanzia tarehe aliyopimiwa
kiwanja chake.
‘’kama hukwenda kujisalimisha
kudai hati ya eneo lako lililowekewa mawe basi baada ya siku tisini
utaletewa bili na utadaiwa kuanzia siku ambayo kiwanja chako kiliwekewa
mawe, kama yaliwekwa mwaka 1986 basi utaanza kudaiwa kuanzia hapo’’
alisema Lukuvi
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi
Msaidizi mkoa wa Kigoma Chediel Mrutu, mkoa huo una wamiliki wa viwanja
14,746 ambao hawajachukua hati zao pamoja na kukamilika taratibu zote za
umilikishwaji ikiwemo kuwekewa alama jambo linaloikosesha serikali
mapato sambamba na wamiliki wake kukosa fursa za kiuchumi zinazotokana
na kuwa na hati miliki
‘’Usipokuwa na hati ya kiwanja
hukopesheki, ongezeni thamani ya mitaji yenu na ardhi isiyopimwa inaitwa
mitaji mifu na unapopima ardhi yako na kumilikishwa unakuwa na kinga ya
kisheria ‘’ alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa
Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga aliielezea ardhi kama
msingi wa haki na dhuluma yoyote inayofanyika inaweza kuleta vita kwa
kuwa ardhi ina rasilimali mbalimbali. Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali
Mstaafu Maganga, uanziushwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Kigoma
utawezesha wana kigoma kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo
kusafiri hadi Tabora kuifuta huduma kwenye ofisi ya kanda.
Mapema Kamishna Msaidizi wa Ardhi
Uratibu na Usimamizi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Wilson Luge alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa unaenda
sambamba na usambazaji vifaa vya kisasa kwenye ofisi hizo ili kuongeza
kasi ya upangaji, upimaji na umilikshaji ambapo alibainisha kuwa ardhi
inaweza kutumika kama sehemu ya mwananchi kujiongezea kipato.
No comments :
Post a Comment