Friday, July 10, 2020

TAKUKURU IRINGA WAREJESHA MAMILIONI YA MWALIMU MSTAAFU



Mkuu wa Takukru Mkoa wa Iringa Mweri Kilimali kulia akiwa na mwalimu Msuri Chuma aliyetaka kudhulimiwa kiasi cha milioni 19 kutokana na mikopo umiza.
……………………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE,IRINGA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Iringa imefanikiwa kurejesha kiasi
cha sh. Milioni 19,460,000 kwa mwalimu Mstaafu Msuri Chuma kutoka kwenye kampuni ya mikopo ya Magere Credit Company Limited na Dicta Financial service Company Limited baada ya kufanya oparesheni endelevu juu ya wanaojihusisha na mikopo umiza.
Akizungumza na wanahabari wakati wakati wa kutoa taarifa ya Takukuru mkoa wa Iringa kwa kipindi cha kuanzia Mwezi April hadi Juni mwaka huu, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Mweli Kilimali jana ofisini kwake, alisema kuwa fedha hizo zimerejeshwa baada ya kubaini riba kubwa ya marejesho aliyotakiwa kufanya mwalimu huyo kwa taasisi hizo.
Akizungumzia hali hiyo, Kilimali alisema kuwa mnamo mwezi Desemba mwaka 2019 Mwalimu Msuri Chuma alikopa fedha kiasi cha sh. Milioni 11,900,000 kutoka kwa Magere Credit Company Limited inayomilikiwa na  Juma George Magere kwa ajili ya kwenda kulipia ada za watoto wake watano pamoja na yatima wawili wanaosoma sekondari na vyuoni.
Alisema kuwa mara baada ya kukopa fedha hizo alitakiwa kurejesha sh. Milioni 31,425,000 yakiwa na riba ya asilimia 264 ambapo kati ya fedha hizo alikuwa amefanikiwa kurejesha milioni 1.065,000 na hivyo kusalia rejesho la milioni 30,360,000 kwa dhamana ya kuacha vyeti vya elimu,kadi mbili za benki pamoja nywila (password).
Kilimali alisema kuwa mara baada ya kupata taarifa hizo na kufanyiwa kazi walibaini mapungufu ya utozaji wa riba kinyume na utaratibu za utozaji wa riba za mikopo na jambo ambalo wahusika wa mikopo hiyo walikiri mapungufu hayo.
Alisema kuwa kutokana na mapungufu hayo walimtoza mkopaji riba stahiki ambapo katika mkopo wa sh. Milioni 11.9 alirejesha sh milioni 14 badala ya sh milioni 30.3 na mkopo wa milioni 1 alirejesha sh. Miloni 1.4 badala y ash. Milioni 4.5 hivyo alitakiwa kufanya marejesho ya jumla y ash. Milioni 34.8 lakini baada ya takukuru mkoa wa iringa kufanyia kazi alirejesha sh. Milioni 15.4 hivyo kuokoa milioni  19.4.
“Takukuru mkoa wa Iringa inatoa wito kwa wananchi wanaoojihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa sheria na taratibu za mikopo kuacha vitendo hivyo mara moja na kuwataka wananchi wanapobaini vitendo hivyo  wanatakiwa kutoa taarifa ili hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika”
Aidha alisema kuwa katika kipindi tajwa imeweza kufanya kazi mbalimbali za udhibiti na kufanikiwa kudhibiti na kuokoa mali na fedha kutokana na oparesheni mbalimbali na katika oparesheji hizo wadaiwa sugu na chunguzi za ubadhirifu wa fedha za vyama vya akiba na mikopo (saccos) takukuru imeokoa sh. Bilioni 1.2 na kuendelea na uchunguzi wa tuhuma za madeni hayo yenye jumla ya sh. Bilioni 3.7.
Aidha Kilimali alisema kuwa katika kipindi hicho Takukuru mkoa wa Iringa imefanikiwa  kupokea malalamiko 68 ambapo baadhi ya walalamikaji walishauriwa na taarifa nyingine zilihamishiwa idara zingine na zile zinazohusu sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007 ziko kwenye hatua mbalimbali za uchunguzi ambapo mashtaka 16 yamefikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Mwalimu Msuri Chuma, aliwashukuru takukuru kwa kuweza kumsaidia kwani alikwisha poteza matumaini ya kulipa fedha hizo kutokana na riba kubwa na kuongeza kuwa baada ya kugundua hilo alianza kutafuta njia mbalimbali na kufikisha changamoto hiyo takukuru ambapo walianza uchunguzi.
Alisema kuwa alikopa kiasi cha milioni 11 kwa ajili ya ada ya watoto wake ambapo alitakiwa kulipa kwa kipindi cha miezi 6 na miezi hiyo ikipita  basi riba inaongezeka hadi kufikia kiasi cha milioni 35 hali iliyomlazimu kutoa taarifa takukuru kwamsaada zaidi na kuwataka jamii kuepuka kukopa kwenye mikopo umiza.

No comments :

Post a Comment