Wataalam wa afya wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwapima wananchi waliotembelea banda la
JKCI lililopo ukumbi wa Karume shinikizo la damu (BP) pamoja na kutoa
ushauri wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule akimpima kiwango cha sukari mwilini
mwananchi aliyetembelea banda la JKCI JKCI lililopo ukumbi wa Karume
wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia akimweleza
kuhusu ugonjwa wa kutanuka kwa moyo mwananchi aliyetembelea banda la
JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam.
Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwahudumia wananchi waliotembelea banda
la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam. Katika maonesho hayo Taasisi hiyo inatoa huduma za upimaji na
ushauri wa magonjwa ya moyo
Daktari
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Winnie Masakuya akimuelezea
mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo namna ambavyo mishipa
inayopeleka damu kwenye moyo inavyoweza kuziba kutokana na kuganda kwa
mafuta katika mishipa hiyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Ipyana Mwailafu kiwango cha sukari mwilini
mwananchi aliyetembelea banda la JKCI lililopo ukumbi wa Karume wakati
wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Picha na JKCI
……………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeombwa kuwafikia wananchi wengi zaidi
hasa
wanaoishi maeneo ya vijijini ili waweze kupata huduma za upimaji,
ushauri na matibabu ya moyo kama wanazozitoa kwa wananchi wanaoishi
mjini.
Ombi
hilo limetolewa na baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Taasisi
hiyo lililopo ukumbi wa Karume kwa ajili ya kufanya vipimo na kupata
ushauri wa magojwa ya moyo wakati wa maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Wananchi
hao walisema watu wengi wanaoishi maeneo ya mjini wanapata nafasi ya
kupima afya zao mara kwa mara hii ni kutokana na taasisi mbalimbali za
afya kufanya upimaji wa bila malipo tofauti na ilivyo kwa wanachi
wanaoishi vijijini.
“Leo
hii nimetembelea katika maonesho haya nimepata bahati ya kupima afya na
kupata ushauri wa mtaalamu wa lishe ambao utanisaidia kula chakula bora
ambacho hakitaniletea madhara katika mwili wangu”, alisema Patricia
Chikojo ambaye ni mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani.
Patricia
aliwashauri wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa ya jirani
kutembelea banda la Taasisi hiyo lililoko katika ukumbi wa Karume ili
waweze kupata huduma mbalimbali za upimaji wa magonjwa ya moyo
zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi hiyo.
“Wito
wangu kwa wananchi watembelee maonesho hayo na kwenda kupima magonjwa
mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa moyo kwa kufanya hivyo watatambua hali zao
kuliko kusubiri waumwe ambapo wanaweza kugundulika kuwa na magonjwa
makubwa ambayo matibabu yake yakawa ya gharama au magonjwa hayo
yakashindwa kutibika kutokana na kuchelewa kugundulika”, alisema
Patricia.
Kwa
upande wake Cyril Kessi ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam alifurahia
huduma aliyoipata ya upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo pia alipata
muda wa kupima vipimo mbalimbali ikiwemo urefu, uzito, damu, kuangalia
jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO) na umeme wa moyo (ECG).
“Huduma
niliyoipata ni nzuri, kuna vipimo nimepima bure na vingine nimelipia
gharama kidogo ukilinganisha na kama ningekwenda Hospitali kupima. Pia
nimepata muda wa kutosha wa kuzungumza na daktari ambaye amenieleza kwa
kina kuhusu magonjwa ya moyo”, alisema Kessi.
Akizugumzia kuhusu maonesho hayo Mkuu wa kitengo cha Utafiti na Mafunzo wa Taasisi hiyo Dkt. Naiz Majani alisema katika
maonesho hayo wanatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo
bila malipo yoyote, upimaji wa magonjwa ya Moyo vikiwepo vipimo vya
damu, ECHO na ECG.
Ushauri wa kiafya kuhusiana na
magonjwa ya moyo, elimu ya lishe bora, kuelezea kwa kina huduma
zinazotolewa na Taasisi hiyo na kutoa Rufaa ya moja kwa moja kwa
wagonjwa watakaokutwa na matatizo ya Moyo yanayohitaji kupewa rufaa.
Dkt. Naiz ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema asilimia
kubwa ya watu waliowapima walikuwa wanatumia dawa za shinikizo la damu
(BP) lakini baada ya kuona hali zao ziko vizuri wameacha kutumia dawa
kitu ambacho siyo sawa kwani mgonjwa wa shinikizo la damu akianza
kutumia dawa hatakiwi kuziacha katika maisha yake yote.
“Tumewaanzishia dawa
wagonjwa tuliowakuta wameacha kutumia dawa za shinikizo la damu pia
tumewaeleza madhara ya kuacha kutumia dawa hizo hii ikiwa ni pamoja na
moyo kutanuka na kushindwa kufanya kazi , kupofuka kwa macho, figo
kuacha kufanya kazi, kiharusi na vifo vya ghafla”, alisema Dkt. Naiz.
Aliwashauri
wazazi wanaokwenda kupima afya zao katika banda hilo kwenda kupima na
familia zao wakiwemo watoto kwani tafiti zinaonesha kuwa kati ya watoto
100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja anatatizo la moyo.
No comments :
Post a Comment