Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan
Abbasi,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati
akitangaza siri 10 za Tanzania kung’ara na kuingia Uchumi wa kati miaka
mitano kabla ya kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.
TANZANIA YAINGIA KUNDI LA NCHI ZA KIPATO CHA KATI
…………………………………………………………………………………
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Benki ya Dunia imeitaja Tanzania
kuwa miongoni mwa nchi 50 duniani za uchumi wa kipato cha kati, ikiwa ni
ya
pili baada ya Kenya katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,
baada ya ukuaji wa uchumi unaosukuma pato la mwananchi kukua (Per capita
GNI) mwaka 2020.
Tanzania imeingia kwenye uchumi wa
kati miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
2025, jambo ambalo ni la kujivunia.
Akizungumza katika Mkutano na
waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan
Abbasi alisema kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025 katika
ukurasa wa pili, kipengele 1.2 “Uchumi wa kipato cha kati umehusishwa na
kuwa na nchi ambayo umaskini unapungua, uchumi imara unaojengwa na
kuimarika kwa uzalishaji viwandani unaimarika na wananchi wanapata
maendeleo”.
Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa
uchumi wa kipato cha kati umegawanyika katika madaraja mawili daraja la
chini ambapo ni kuanzia dola za Kimarekani 1036 hadi 4045 na daraja la
juu ni dola 4046 hadi 12,535 na mwaka huu Tanzania imepanda daraja kuwa
uchumi wa kipato cha kati daraja la chini, pamoja na nchi za Algeria na
Benin.
Aidha, Dkt. Abbasi alifafanua siri
10 zilizoisaidia Tanzania kutajwa kufikia daraja la uchumi wa kipato
cha kati na Benki ya Dunia hapo Julai 1, 2020 kuwa ni nchi yenye amani
na utulivu, na hivyo ni msingi muhimu nyuma ya mafanikio ya nchi ya
Tanzania kuingia katika uchumi wa kipato cha kati kwani bila amani
hakuna kufanyakazi, hakuna kuzalisha na hakuna kuongeza kipato. Na hivyo
viongozi, wanahabari na wananchi kwa ujumla wamesisitizwa kuwekeza
akili zao katika kuimarisha amani iliyopo na kukataa chokochoko zozote
zile zinazoweza kuharibu misingi ya maendeleo.
Siri ya pili ni mipango thabiti
ya maendeleo, ambapo Dkt. Abbasi alisema kuwa moja ya kanuni muhimu ya
kuendelea ni kuwa na mipango inayokuwekea malengo makubwa (Olympic targets).
Serikali itaendelea kuweka mipango mbalimbali ya maendeleo ya muda
mrefu na mfupi, akitolea mfano mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo moja ya malengo ni kufikia
uchumi wa kati.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi siri ya
tatu ni utekelezaji usioyumba, katika miaka 59 ya Uhuru na mitano ya
Awamu ya Tano Serikali imejitahidi kusimamia eneo hilo kwa kuhakikisha
mipango inayowekwa inatekelezwa kwa kina (3feet implementation).
Siri nyingine ni maamuzi magumu,
“Moja ya mafanikio ya Serikali ya Tanzania kwa Awamu zote na sasa
tumeimarisha katika Awamu ya Tano ni wakati fulani Serikali kufanya
uamuzi mgumu ambao wakati fulani ulionekana kuwa ni ndoto lakini baadaye
ukaleta mafanikio makubwa kwa jamii, tumepambana na wala rushwa na
wahujumu uchumi, tumewekeza katika miundombinu mikubwa, tumekataa pia
baadhi ya nadharia za kimagharibi kwenye utendaji wetu na utungaji wetu
wa sera za maendeleo” alisema Dkt. Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi alitaja siri
nyingine kuwa ni azma ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi,
kutekeleza miiko ya uongozi, kuwekeza kwenye miradi inayochechemsha
uchumi, maendeleo ya vitu na sekta binafsi yenye tija.
No comments :
Post a Comment