Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Benki
ya Maendeleo ya Kilimo, Japhet Justine (kulia) alipomkabidhi Mkuu wa
Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa hundi ya Sh. 9,050,846,030/= ikiwa ni
malipo ya madeni ya wakulima, waendesha maghala, wasafirishaji na
wapuliza madawa wa zao la korosho wilayani Tandahimba katika mkutano
aliouhutubia kwenye viwanja vya AMCOS ya Matogoro, Tandahimba, Julai
19, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imetoa sh. bilioni 20 za kulipa madeni ya
wakulima,
wasafirishaji, wapuliziaji dawa na waendesha maghala ya korosho.
“Rais
Magufuli ametoa fedha hizi kwa ajili ya Tandahimba, Masasi, Mtwara na
Kibiti kwa ajili ya waliokuwa wamelipwa nusu, waliolipwa kiasi na
wasiolipwa kabisa. Fedha hizi zitaanza kulipwa kesho asubuhi,” amesema.
Ametoa kauli
hiyo leo (Jumapili, Julai 19, 2020) wakati akizungumza na wanachama wa
Chama cha Msingi (AMCOS) cha Matogoro na wakazi wa Tandahimba mkoani
Mtwara alikoenda kuhamasisha maandalizi ya msimu wa ununuzi wa korosho.
Amesema
uhakiki uliofanywa kwa wakulima wa Kibiti, Rufiji, Mkuranga, Ruangwa,
Liwale, Lindi, Tunduru na wilaya zote za mkoa wa Mtwara ulibaini kuwa
wakulima na watoa huduma wote walikuwa wakidai zaidi ya sh. bilioni 23.
“Katika hao,
Tandahimba wanadai zaidi ya sh. bilioni 9, Masasi wanadai sh. bilioni
2.3 na Mtwara Vijijini wanadai sh. milioni 884. Nyingine ni za Pwani na
Lindi,” amefafanua.
Waziri Mkuu
amesema fedha hizo zimetokana na mfumo uliotengenezwa na wanunuzi ili
kumnyonya mkulima katika msimu wa 2018/2019 kwa kununua kilo ya korosho
kwa sh. 1,500 badala ya sh. 3,000 hali iliyolazimu Serikali kuingilia
kati na kuamua kuzinunua korosho zote.
Waziri Mkuu
alishuhudia Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo (TABD), Bw. Japhet
Justine akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Gelasius Byakanwa hundi
ya sh. 9,050, 846,030 ambaye pia aliikabidhi kwa viongozi wa Chama Kikuu
cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) na AMCOS ya Matogoro.
Awali,
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara, Bw. Yusuph Nanila alimuomba Waziri
Mkuu atoe majibu ya lini wakulima wa Tandahimba watalipwa fedha zao,
ambazo zimefikia zaidi ya sh. bilioni 9.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amevitaka Vyama Vikuu vya Ushirika na AMCOS waweke
kipaumbele cha kununua mashine ndogo ndogo za kubangulia korosho ili
waache mtindo wa kuuza korosho ghafi.
“Ukibangua
kilo tatu za korosho yenye maganda, unapata kilo moja ya korosho
zilizobanguliwa. Kilo moja ya korosho yenye maganda inauzwa sh. 2,400
kwa hiyo kilo tatu ni sh.7,200, lakini ukizibangua, kilo moja inauzwa
sh.25,000. Ninawasihi tuanzishe viwanda vidogo vya kubangua korosho ili
tupate fedha zaidi kwenye vyama vya msingi.”
“Matogoro
mnaweza kununua hata mashine 100 kutoka SIDO ili mzibangue hapahapa na
kuongeza pato la wakulima wenu. Tena mashine za viwanda vidogovidogo
zinatoa korosho nzuri zenye ubora sawa na zilizotoka kwenye mashine
kubwa,” aliongeza.
Kuhusu msimu
wa ununuzi wa korosho, Waziri Mkuu alisema msimu mpya unaanza Septemba
hadi Desemba na akawataka viongozi wa ushirika wasimamie ununuzi wa
korosho mapema.
Aliwataka
wakulima wa korosho wa wilaya hiyo wabadili mfumo wa kilimo cha zao hilo
kwa kuanza kupanda miche mipya ambayo inazaa kwa wingi na inachukua
muda mfupi kukomaa. “Pandeni miche mipya kwa sababu inazaa ndani ya
mwaka mmoja na nusu, ondoeni mikorosho iliyozeeka.”
Pia aliwataka
wanachama hao walime mazao mbadala kama chikichi na alizeti ambayo
yanakubali kwenye ardhi yao ili waongeze wigo wa sgughuli za kiuchumi
kwenye wilaya hiyo. “Michikichi inakubali sana kwenye ukanda wa pwani,
kwa hiyo jaribuni muone ukuaji wake.”
Kuhusu malipo
ya wasafirishaji, Waziri Mkuu alisema kati ya fedha zilizolipwa,
wasafirishaji wametengewa sh. bilioni 3.3. Alikuwa akijibu swali la
Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji wilayani Tandahimba, Bw. Maulid
Mussa ambaye alisema walisafirisha korosho kutoka kwa wakulima hadi
kwenye maghala na madai yao yaliyofikia sh. milioni 600 yamekuwa
yakiwanyima usingizi kwa muda mrefu.
Kuhusu bei
dira ya korosho, Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa vyama vya msingi
na vyama vikuu nchini kote wakae na kuandaa gharama ambazo mkulima
anakuwa amezitumia na gharama zitakazokubaliwa ndiyo iwe msingi wa bei
dira.
“Vyama vikuu
vifanye hiyo kazi kabla msimu haujaanza Septemba 2020. Mniletee ofisni
kwa maandishi ili tumshirikishe Waziri wa Kilimo na kisha tutangaze
kitaifa bei dira ni ipi,” amesema.
No comments :
Post a Comment