Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni-
Daniel Chongolo akipokea msaada mabati 180 kutoka kwa Kaimu Meneja wa
Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam – Seka Urio.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Turiani wakipeleka madawati darasani baada ya hafla fupi ya makabidhiano na Benki ya NMB.
……………………………………………………………………..
Benki ya NMB, imekabidhi misaada
ya mabati 180, madawati 200, mashine sita za
kunawia mikono, viti na
meza 100, kwa ajili ya Shule za Msingi Oysterbay, Msasani, Tandale
Magharibi, Mzimuni na Kisauke pamoja na Sekondari ya Turiani. Huku
kituo cha Afya cha Mabwepande kikipata vitanda magodoro, vyote kwa
pamoja vikiwa na thamani ya jumla ya Sh. Mil. 36.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kuvibabidhi kwa Mkuu wa Wilaya – Daniel Chongolo, Kaimu Meneja wa Benk
ya NMB Kanda ya Dar es Salaam – Seka Urio alisema “Ingawa Serikali
inafanya makubwa, sisi kama wadau tunawajibu wa kuunga mkono juhudi hizi
za maendeleo kwa kusaidia jamii, kwani kupitia jamii hii hii, ndio
imeifanya benki yetu kuwa hapa ilipo, kubwa kuliko benki yoyote hapa
nchini huku tukiendelea kupokea tuzo ya benki bora kwa mara ya nane
mfululizo,”
Alibainisha kuwa, NMB itaendelea
kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo katika jamii
inayowanzunguka. “Kwa maana hiyo, NMB tumeamua kushirikiana na shule
hizo, ambazo kila shule inapata madawati 50 na viti vyake. Pia
tumechangia Shule ya Msingi Mzimuni mabati 150, huku Shule tano zikipata
mashine za kunawia mikono na maji tiririka ilikuzuia maambukizi ya
Covid-19,” aliongeza:
Kwa mwaka 2020, NMB imetenga zaidi
ya Sh. Bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo
kusaidia sekta ya afya na elimu, kiasi kinachoifanya kuwa benki ya
kwanza katika kuchangia maendeleo kuliko benki yoyote nchini.
Kwa upande wake, DC Chongolo
aliipongeza Benki ya NMB kwa moyo wa kuijali na kuithamini jamii na
kwamba misaada mbalimbali inayotoa katika sekta za afya na elimu,
inaacha alama njema katika mioyo ya wanafunzi, walimu na jamii kwa
ujumla na kuwa inasaidia harakati za Serikali katika kuboresha
miundombinu na kutatua changamoto.
Chongolo aliwaagiza watendaji
mbalimbali waliopo katika Wilaya ya Kinondoni, kuhakikisha wanatumia
huduma za NMB hasa za makusanyo ya kodi, ili kuchagiza pato la benki
hiyo na kukuza asilimia moja ya mapato yao yamwaka na kuzifikia taasisi
nyingi zaidi zenye uhitaji kupitia program ya Uwajibikaji kwa Jamii
(CSR).
No comments :
Post a Comment