Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Samwel Laizer (kulia)
akipokea vifaa maalumu vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona
kwa shule mbalimbali Wilaya humo kutoka kwa Meneja wa Uchechemzi na
Kampeni kutoka Save The Children Nuria Mshare (katikati) kushoto ni
Meneja wa mradi wa ulinzi kwa mtoto Jesca Ndana, leo jijini Dar es
Salaam.
Muonekano wa vifaa mbalimbali vya kujikinga na maambukizi ya virusi
vya Corona vilivyotolewa na Shirika la Save The Children kwa Manispaa ya
Kinondoni vikielekezwa kuwafikia wanafunzi katika mashule mbalimbali
ikiwa ni sehemu ya kupambana na kujikinga zaidi na kuenea kwa virusi
hivyo, leo jijini Dar es Salaam.
Meneja wa mradi wa ulinzi kwa mtoto Jesca Ndana (wapili kushoto)
akitoa maelezo kwa Mganga mkuu wa Manispaa ya Kinondoni Dkt. Samwel
Laizer juu ya namna wanavyozihudumia shule 10 za Mkoa wa Dar es Salaam
katika kuhakikisha mtoto analindwa na kupata mahitaji ya msingi, leo
jijini Dar es Salaam.
Na Leandra Gabriel, Globu ya Jamii
SHIRIKA
la Save The Children leo Julai 9 limekabidhi vifaa maalumu vya
kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona yakiwemo matanki, sabuni za
kunawia na taulo za kike kwa Manispaa ya Wilaya ya Kinondoni huku
vifaa hivyo vikielekezwa kuwafikia wanafunzi katika mashule mbalimbali
ikiwa ni sehemu mchango wa Shirika hilo kwa Serikali katika kupambana na
kuenea kwa virusi vya vya Corona hasa kwa wakati huu ambao shule
zimefunguliwa na watoto wanaendelea na masomo.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam mara baada ya
kupokea vifaa hivyo Mganga mkuu wa Manispaa ya Kinondoni kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Dkt. Samwel Laizer amesema kuwa Save The
Children wamekua wadau na washirika bora katika kulinda na kutetea
watoto pamoja na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
"Mmekua mkifanya kazi kwa ukaribu zaidi na Serikali katika kutatua
changamoto mbalimbali, ni mfano mzuri wa kuigwa na nina imani vifaa hivi
vitawafikia walengwa"ameeleza Laizer.
Dkt.Laizer amesema kuwa baada ya watoto kurejea mashuleni bado
wanatakiwa kuwa salama kiafya ili waweze kusoma kwa uhuru na kufaulu
masomo yao.
" Mchango huu ni hatua ya kwanza katika kufanikisha ndoto za watoto
wetu, wanafunzi watanawa kwa kutumia vifaa hivi na kuingia madarasani
wakiwa salama zaidi na kusoma kwa uhuru zaidi" ameeleza.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika hilo Meneja wa Uchechemuzi na
Kampeni kutoka shirika hilo Nuria Mshare amesema kuwa wamekabidhi
matanki 20, sabuni za kunawia 500 pamoja na taulo za kike 1000 kwa
Manispaa ya Kinondoni ili ziwafikie na kuwasaidia watoto ambao wamerudi
shule.
Amesema kuwa lengo kutoa mchango huo ni kutokana na ufanyaji kazi kwa
ukaribu zaidi wa Serikali na shirika hilo katika kuhakikisha mtoto
analindwa hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya Corona
vilivyoathiri duniani kote.
"Tulivyoona wanafunzi wanarudi shule kuendelea na masomo yao tukaona
ni muhimu kuisaidia Serikali katika kuhakikisha watoto wanakua salama
kiafya kwa kuhakikisha wananawa na kupata elimu ya afya sambamba na
kupata elimu bora zaidi" ameeleza.
Shirika lisilo la kiserikali limekuwa likifanya kazi na shule
zipatazo 10 katika Mkoa wa Dar es Salaam na wamekuwa wakishirikiana kwa
karibu zaidi na Serikali katika kuhakikisha watoto wanabaki salama
pamoja na kupata mahitaji yote ya msingi ikiwemo elimu na afya.
No comments :
Post a Comment