Friday, July 10, 2020

HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM YAMPITISHA DKT.HUSSEIN MWINYI KUGOMBEA URAIS ZANZIBAR



HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha kwa kauli moja jina la Dkt.Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Chama hicho katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Akitangaza matokeo ya kura ambazo zimepigwa na wajumbe wa mkutano huo uliofanyika leo Jijini Dodoma, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amesema kuwa Dkt.Mwinyi amepata kura kura 129 sawa na asilimia 78.65, Shamsi Vuai Nohodha kura 16 pamoja na Dkt.Khalid Salum Mohamed aliyepata kura 19 sawa na asilimia 12.58.

Baada ya Spika Ndugai ambaye alitangaza matokeo hayo kwa niaba ya wasimamizi wenzake, wajumbe wa mkutano huo kwa pamoja walianza kushangilia kwa kupiga makofi.

Mwenyekiti wa CCM Taifa ,Rais Dkt.John Magufuli akizungumza baada ya Dkt.Mwinyi jina lake kuibuka kidedea kwenye matokeo ya kura hizo, amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar Dkt.Mwinyi ndiye anayekwenda kupeperusha bendera ya Chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

" Bila kulazimishwa na mtu, bila kushurutishwa na kwa kumtanguliza Mungu wetu kwa ajili ya kufanikisha ushindi wa Zanzibar, kwa kauli moja wajumbe wa mkutano huu wamepitisha jina la Dk.Hussein Mwinyi.Tunakwenda kumtetea, Dkt.husein Mwinyi ndiye atakuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar.

"Najua wengine wengine hawajasikia, najua wengine hawakusikia, kwamba Dk.Husein Mwinyi aliyeongoza kwa kupata asilimia 78.75 katika kura zote zilizopigwa bila kuharibika hata kura moja ndio amechaguliwa na kikao hiki kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang'anyiro cha Urais wa Zanzibara,"amesema Dkt.Magufuli.

No comments :

Post a Comment