Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu akifungua Mkutano
wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya mtandao, kwaniaba ya Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango, katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu akifungua Mkutano
wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) kwa njia ya mtandao, kwaniaba ya Waziri wa
Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango, katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, akipitia nyaraka za Mkutano wa Kamati ya
Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika(SADC), uliofanyika kwa njia ya TEHAMA katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo nchi
wanachama 16 na Taasisi kadhaa zimeshiriki Mkutano huo. Kulia ni
Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu, kwaniaba ya Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.
Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania
kwenye Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania,
Prof. Florens Luoga (wa pili kulia walioketi mbele), akiwa na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto),
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Bw. Juma Hassan Reli (wa pili kulia nyuma), Naibu Katibu Mkuu
Wazara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaban (kulia mbele), na
Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Suleiman
Missango (kushoto), wakifuatilia mjadala wa mkutano huo, uliofanyika kwa
njia ya mtaondao kutokea Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius
Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akichambua nyaraka za Mkutano wa Kamati ya
Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC), uliofanyika kwa njia ya TEHAMA, katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Suleiman
Missango.
Baadhi ya Maafisa waandamizi wa
Tanzania wakishiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika kwa njia
ya TEHAMA, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere,
jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Ushirikiano wa Kikanda, Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Bi. Agnes Richard Kayola, akifuatilia kwa makini Mkutano wa
Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC), uliofanyika kwa njia ya Mtandao kutokea katika Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe.
Mussa Azzan Zungu, kwaniaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Isidor Mpango ukishiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha
na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika kwa njia ya mtandao, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
……………………………………………………..
Na Farida Ramadhani, Dar es Salaam
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) imezipongeza nchi za Tanzania na
Mauritius kwa kufanikiwa
kuingia katika uchumi wa kati na juu licha ya changamoto mbalimbali za
kiuchumi zilizoikumba Jumuiya hiyo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu
alipofungua Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa nchi
za SADC kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor
Mpango, uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Zungu alisema kuwa Tanzania
ilitangazwa na Benki ya Dunia kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati
na Mauritius imepanda daraja na kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha juu
kutokana na kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja.
“Kwa Tanzania pato la mtu mmoja
mmoja limeongezeka kutoka dola za Marekani 1,020 kwa mwaka 2018 na
kufikia dola za Marekani 1,080 kwa mwaka 2019 na Mauritius pato la mtu
mmoja mmoja limeongezeka hadi kufikia dola za Marekani 12,740 kwa mwaka
2019 kutoka na dola za Marekani 12,050 mwaka 2018”, alifafanua.
Mhe. Zungu alisema pamoja na nchi
kupanda daraja hakuna nchi mwanachama ambayo imeshuka daraja na
kuzishauri nchi wanachama kuyatumia mafanikio hayo kama chachu ya
kujitathmini na kuangalia uwezekano wa kuleta maendeleo zaidi ya
kiuchumi na kuchukua tahadhali ili chumi zisiweze kushuka hadhi.
Pamoja na mafanikio hayo,
alizisihi nchi wanachama kuendelea kuchukua hatua za kukabiliana na
janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona
(COVID-19) bila kuathiri shughuli za kiuchumi kwa kuwa ugonjwa huo ni
changamoto nyingine ya uchumi wa Jumuiya hiyo.
Alisema kuwa athari za ugonjwa
huo zinatajwa kusababisha chumi za nchi nyingi duniani kuporomoka
kutokana na kusimama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii
ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiri sekta ya huduma zinazochangia zaidi
ya robo ya ajira zote katika chumi za nchi wanachama wa SADC.
“Matokeo ya uchambuzi wa athari
za ugonjwa wa COVID-19 kwenye viashiria vya muunganiko wa uchumi mpana
kwa nchi za SADC yameonesha nchi wanachama zinatarajia kushuhudia ukuaji
mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti ya Serikali na
kuongezeka kwa madeni”,alisema Mhe. Zungu.
Mhe. Zungu amezishauri nchi
wanachama wa SADC kutafuta fedha kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu ili
kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijami ambazo ziliatharika
na COVID-19 pamoja na kupunguza mzigo wa madeni.
Aidha, aliipongeza Sekretarieti
ya SADC kupitia kamati zake ndogondogo kwa kazi wanayoifanya kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutafuta njia mbalimbali zenye
ubunifu katika kugharamia miradi ya maendeleo kwa kuangalia namna bora
ya uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda na Mfuko wa Kugharamia
Miradi ya Miundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme.
Alisema matokea ya kazi zao
yatatoa fursa kwa nchi wanachama kutoa maamuzi ambayo yatapelekea
kufikia malengo ya Jumuiya na kusaidia kuboresha mazingira ya kuvutia
uwekezaji.
Alisisitiza kuwa Mfuko wa
Kugharamia Miradi ya Miundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme
utasaidia kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ndani ya
Jumuiya kwa kuwa suala la upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika
ni sehemu muhimu itakayoiwezesha Jumuiya kufikia malengo yake ya uchumi
wa viwanda.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Zungu aliihakikishia Jumuiya hiyo kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania
unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2020 utakuwa huru, wa amani na
utulivu utakaozingatia misingi ya demokrasia huku akizipongeza nchi za
Botswana na Malawi kwa kufanya uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu.
No comments :
Post a Comment