…………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia
Wizara ya Maji imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika
maeneo ya mijini na vijijini kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya
Maji kwa mujibu wa
Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002.
Sera ya Taifa ya
Maji ya mwaka 2002 inaelekeza kuwapatia wananchi waishio vijijini maji
safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao,
hatua inayolenga kuwaondelea changamoto mbalimbali ikiwemo maskini na
magonjwa yanayosababishwa na maji.
Wizara ya
Maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini kwa kujenga,
kupanua na kukarabati miradi ya maji, lengo ikiwa ni kufikia asilimia
85 ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya
vijijini ifikapo mwaka 2020.
Miradi ya Maji
Vijijini inatekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana
na wananchi pamoja na sekta binafsi ambapo katika kuwapunguzia wananchi
gharama, Serikali kwa kushirikiana na wadau inaandaa mifumo itakayofaa
kusimamia na kuendesha miradi ya maji ikiwa ni pamoja na kuviimarisha
Vyombo vya Watumiaji Maji.
Halmashauri ya
Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi inatekeleza miradi mbalimbali ya maji
katika vijiji mbalimbali vya Wilaya hiyo hatua inayolenga katika kutoa
huduma endelevu kwa wakazi waishio mijini na pembezoni mwa miji.
Wananchi
wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama kutoka katika vyanzo
vya Visima vifupi, Visima vya kati, Visima virefu ambavyo vimefungwa
pampu za mikono, miradi ya maji bomba ya maporomoko na miradi ya maji ya
kusukumwa na mitambo.
Tangu kuingia
madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hali ya upatikanaji wa huduma
ya maji vijijini imeongezeka kutoka 38.5% mwaka 2015 hadi kufikia 51.20%
kufikia mwezi Novemba, 2018 ikiwa ni ongezeko la 12.7% ambapo jumla
watu 64,498 waishio vijijini wanapata huduma ya maji.
Miongoni mwa
miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Maji wa Naunambe-Mpekenyera
unaosimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kushirikiana na
Kamati za Vijiji vya Naunambe na Mpekenyera katika kuhakikisha kuwa
Serikali inamtua mama ndoo kichwani na kumuondolea changamoto ya
kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.
Kufuatia juhudi
kubwa zilizofanywa na Serikali ya Wilaya ya Ruangwa mradi huo
ulikamilika mwezi Juni, 2018 na jumla wananchi 7,000 wameanza kupata
maji na salama na kiasi Tsh. Milioni 828 zimetumika kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali ikiwemo
mashine za kusafisha maji na miundombinu mbalimbali kwa ajili ya
kurahisisha upatikanaji wa maji kutoka katika vyanzo na kuwafikia
wananchi.
Akizungumza na
Timu ya Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) waliofanya ziara
Wilayani humo, hivi karibuni, Katibu wa Mradi huo, Selemani Nyamiri
anasema mradi huo ulianza kuibuliwa na wananchi mwaka 2010 kwa kaya
mbalimbali katika vijiji hivyo kuchangishana fedha kwa ajili ya
kuhakikisha mradi huo unatoa huduma endelevu ya maji katika vijiji hivyo
vyenye wakazi zaidi ya 10,000.
‘Maji yaliyokuwa
yakizalishwa katika chanzo cha Mpekenyeara yalikuwa yana chumvi sana,
pia yalipatikana katika vyanzo visivyo safi na salama hivyo ilitulazimu
kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya kutumia mafundi na
utaalamu wa ziada ili kuhakikisha kuwa maji yanarejea katika ubora
wake’’
Nyamiri anasema
kwa sasa kiwango cha chumvi katika maji hayo kimepungua na kufanya maji
hayo kuwa na ubora wa matumizi kwa binadamu, ambapo watumiaji
wanalazimika kuchangia gharama ya Tsh. 200 kwa kila ndoo, ikiwa ni fedha
zinazokusanywa na kamati hiyo kwa ajili ya kufanya matengenezo na
ukarabati wa miundombinu ya mradi.
Akifafanua zaidi
anasema wananchi wa vijiji hivyo wataendelea kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za maendeleo ya jamii
ikiwemo huduma ya maji ambapo wananchi wamekuwa na mwamko wa kusimamia
uhifadhi wa maeneo ya vyanzo vya maji ili kufanya vijiji vyote vinapata
maji ya uhakika.
Naye Mwenyekiti
wa Kijiji cha Naunambe Bi. Amina Abdalla aliipongeza Serikali ya Awamu
ya Tano kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kusimamia
utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa umeondoa kero kwa akina mama wa vijiji
hivyo waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya maji.
Bi. Rehema Mussa
Mkazi wa Kijiji cha Mpekenyera alisema kwa kipindi cha nyuma hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji hivyo haikuwa ya kuridhisha,
hususani wakati wa kipindi cha kiangazi na kuwalazimu wananchi wengi
kutembea umbali wa kilometa 3 kufuata huduma ya maji katika vyanzo
visivyo rasmi huku wakitembea na watoto migongoni.
‘Utekelezaji wa
mradi huu ni mkombozi mkubwa sana kwetu wananchi wa Naunambe na
Mpekenyera kwani kwa sasa shida ya maji imeisha, tunaipongeza Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli pamoja na
juhudi kubwa zinazofanywa na Mbunge wetu wa Ruangwa na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa’’ alisema Rehema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue alisema hali
ya upatikanaji wa maji katika Wilaya hiyo umefikia asilimia 55 huku
kukisaliwa na maeneo machache ambayo yanakosa huduma ya maji ambapo
Ofisi yake imekuwa ikiendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha
huduma ya maji inafikia walau asilimia 70 ifikapo mwishoni mwaka 2020.
‘Halmashauri ya
Ruangwa inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika vijiji
mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wa Naunambe-Mpekenyera wananchi
wanapata maji na wanafurahia huduma inayotolewa kwa mwaka 2019 pekee
tulipata miradi minne ikiwemo mradi wa maji Kitandi na tayari tumeanza
kufanya mawasiliano na Halmashauri ya Mtama kuhakikisha kuwa maji
yanafikishwa katika vijiji jirani ikiwemo vijiji vya Nangumbu A na B’’
alisema Chezue.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Maji Kata ya Mandawa Rashid Mshamu anasema mradi wa maji
mandawa unahuhudumia jumla ya vijiji 5 vya Nahanga, Chikundi, Mandawa
Chini, Mchichili na Mtondo unaogharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 1.7
zilizotolewa na Serikali, ambapo mradi huo unawanufaisha jumla ya watu
13,756.
Anaongeza kuwa
mradi huo ulioasisiwa mwaka 1975 ulikuwa na miundombinu chakavu na
kusababisha kero kubwa kwa wananchi hususani wazee, wanawake na watoto
ambapo walikuwa wanahangaika, ambapo Serikali iliamua kuufua mradi huo
katika bajeti ya mwaka 2014/15.
Anasema kuwa kwa
sasa mradi huo unaendelea vyema na huduma ya maji ni ya uhakika na
wananchi wa vijiji hivyo wanalazimika kuchangia kiasi cha Tsh. 50
inayopelekwa katika mfuko wa maji wa kijiji hicho na kutumika kwa ajili
ya ukarabati wa miundombinu ya mradi.
Miradi mingine ya
maji inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ni pamoja
na mradi wa maji Nanganga, mradi wa maji Likunja, mradi wa maji
Namahema, mradi wa maji Chenjele, ambapo katika maeneo yote hali ya
upatikanaji wa maji ni ya kurithisha.
Miradi mingine ni
pamoja na ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mibure, Namakuku na
Namahema ambao tayari umekamilika na jumla ya watu 6,133 wananufaika,
ambapo kiasi cha Tsh. Milioni 631,593,444.50 zimetumika.
Serikali
imewekeza katika miradi ya maji mikubwa na midogo ili kufikisha huduma
ya maji kwa wananchi, ambapo uwekezaji huo umeleta mabadiliko makubwa
katika sekta mbalimbali nchini na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Ili kuleta
matokeo tarajiwa utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini
unahusisha ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi na pia wadau
wa maendeleo kutokana na ukweli kuwa Serikali imeweka lengo la kufakisha
huduma ya maji kwa asilimia 85 kwa upande wa wananchi.
No comments :
Post a Comment