Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Dodoma, SACP. Gilles Muroto akionyesha baadhi ya Dawa za Binadamu
zilizokamatwa zikisafirishwa kinyume na utaratibu wakati akizungumza na
waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Dodoma, SACP. Gilles Muroto akionyesha namna dawa za binadamu
zilizokamatwa zilivyokuwa zimefungwa na kusafirishwa kinyume na
yutaratibu wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Dodoma
Jeshi la Polisi
Mkoani Dodoma linamshikilia Fredrick Anaclet Maxmilian (38) mkazi wa
Mbagala Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma ya kusafirisha shehena ya madawa
ya binadamu, sambuli 149 baadhi yakiwa na nembo ya MSD.
Hayo
yamebainishwa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP.
Gilles Muroto wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini
Dodoma.
Aidha Muroto amesema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa mnamo tarehe 09/07/2020 majira ya saa moja jioni.
“Katika mahojiano ya awali mtuhumiwa amebainisha kuwa yeye sio daktarin wala siyo mfamasia wa dawa”, ameeleza Muroto.
Muroto amesema kuwa mtuhumiwa huyo anashirikiana na mfamasia ambaye ni mtumishi wa serikali huko mkoani Tabora.
Muroto amesema kuwa mtuhumiwa dawa hizo ameleta Dodoma kwa ajili ya kuuza katika maduka binafsi ya dawa.
Lakini pia Muroto ameongeza kuwa uchunguzi bado naendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
“Nitoe wito kwa
watanzania kuwa waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili
kutokomeza uharifu wowote katika nchi yetu, lakini pia tutumie miiko na
maadili ya taaluma zetu katika utendaji wa kuleta maendeleo na kujenga
taifa hili”, ametoa wito Muroto.
Naye Kaimu Mganga
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Samweli Seseja ameeleza kuwa katika
shehena hiyo dawa zilizo kamatwa na mtuhumiwa huyo ni dawa aina 8 zenye
nembo ya serikali na zilikuwa ziingie sokoni na kusababisha hasara kwa
serikali.
“Mtuhumiwa huyo
amekamatwa na dawa na baadhi ya vifaa tiba ambapo alikuwa akivisafirisha
kinyume na taratibu za usafirishaji wa dawa hizo kwani kila dawa zina
kipimo cha joto lake hivyo nyingine zahitaji kuwa katika jokofu ili
kulinda ubora wa dawa hizo”, amebainisha Dkt. Seseja.
Katika hatua
nyingine Dkt. Seseja ametoa wito kwa wafanya biashara wa maduka ya
madawa kununua dawa kutoka katika katika vyanzo sahihi na vilivyopewa
mamlaka na serikali ili kulinda afya za watanzania na taaluma ya afya
kwa ujumla.
No comments :
Post a Comment