
…………………………………………………………………….
Na.Mwandishi Wetu- MAELEZO
Waziri wa Viwanda wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Amina Salum Ali amefunga rasmi
Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA),
yaliyokuwa yanafanyika katika viwanja vya Mwl.Julius Nyerere barabara ya
Kilwa Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Maonesho
hayo, Balozi Ali amesema kuwa Mamlaka ya Maendeleo ya
Biashara Tanzania,
(Tantrade) inatakiwa kuangalia namna ya kushusha huduma kwa wananchi
walioko katika maeneo mablimbali ya uzalishaji malighafi na bidhaa ili
waweze kujua changamoto za wafanyabiashara hao wa chini.
“Siri kubwa ya maendeleo
katika Sekta ya biashara ni kushusha huduma kwa wafanyabiashara wa chini
kule ambako uzalishaji wa vitu vingi upo yaani malighafi na bidhaa
ndogo ndogo huko ndiko kuna changamoto ambazo zikitatuliwa zitaleta
maendeleo makubwa kwa wafanyabiashara wa kati na wakubwa hatimaye
kukuza viwanda vitakavyoleta uhusiano mkubwa wa biashara”, Alisema
Balozi Amina Ali.
Balozi Amina Ali alisema kuwa
Tantrade ina jukumu kubwala kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kuwa
wakati na wakati kuwa wafanyabiashara wakubwa na hiyo itaondoa
changamoto na kukuza biashara katika maeneo mbalimbali nchini ambako
bidhaa zinazalishwa na kukosa soko mara kwa mara.
Alivitaka vyombo vinavyohusika na
biashara kwa Tanzania bara na Zanzibar kuwasikiliza wazalishaji wa
malighafi hizo ambazo zinatagemewa viwandani kutoa bidhaa kwa
wafanyabiashara wakubwa ni hii itasaidia kujua wakulima, wazalishaji wa
bidhaa ndogondogo wanataka nini ili kuendana na soko la kimataifa.
Aidha alivitaka vyombo hivyo
kushusha huduma za biashara ikiwemo utafutaji masoko na aliwapongeza TMX
ambao wanafanya minada kwa wananchi kwa kutumia mtandao na wananchi
ambao ni wazalishaji kupata bei iliyoko sokoni katika soko la kimataifa.
“Kushusha huduma hizo kwa wananchi
hususani wale wanaozalisha malighafi kutoka shambani ni moja ya
kuwapatia nguvu na kujua wapi wanaweza pata soko kwa faida Zaidi,
nawapongeza sana TMX ambao wanafanya biashara ya mnada ya kuwakutanisha
wafanyabiashara wakubwa nawananchi ana kwa ana na sehemu zingine kwa
njia ya mtandao kwa hiyo wananchi vyombo vyetu endeleeni kuwajali
wananchi kwa kuwatafutia masoko”, Alisisitiza Balozi Amina Ali.
Alibainisha kuwa viwanda vinafanya
vizuri kwa sasa kwani kila sehemu kuna kiwanda ambako mazao au
malighafi rasmi inazalishwa alitolea mfano kiwanda cha maparachichi,
viwanda vya mkonge, viwanda vya alizeti na viwanda vya nyama hiyo inatoa
fursa kubwa sana kwa wafanyabisahara wadogo wa mazao na bidhaa za
viwandani
Balozi ali aliwapongeza Tantrade
kuja na wazo la kulete banda la mazoa ya kimkakati ili kuwezesha
wananchi kujua namna ya kulima mazao hayo na kujipatia kipato kikubwa,
alitaja bodi hizo kuwa ni Bodi ya Mkonge, Bodi ya Korosho, Bodi ya
Pamba, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Pareto na Bodi ya Sukari ambazo
zilikuwepo katika maonesho ya 44 ya biashara ili kutoa elimu kwa
wananchi kuhusu kulima na kuuza mazao hayo.
Mwisho
No comments :
Post a Comment