Mwenyekiti wa
Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu ya
Jaji Mkuu ,Mhe. Shaaban Lila (katikati) ambaye ni Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, akizungumza jambo jana wakati akifungua kikao cha
kamati hiyo kwenye ukumbi wa mkutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Divisheni ya Ardhi uliopo Jijini Dar es Salaam.
Katibu Kamati ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu, ambaye pia ni
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Enock Kalege
akitoa taarifa ya maendeleo ya teknolojia hiyo.
……………………………………………………………………………..
Na Magreth Kinabo – Mahakama
Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Takwimu ya
Jaji Mkuu, Mhe.
Shaaban Lila amewataka wajumbe wa kamati hiyo kutoa uzoefu wao kuhusu
matumizi ya teknolojia na kuzitafutia ufumbuzi changamoto
mbalimbali wanazokabiliana nazo katika eneo hilo.
Akizungumza jana wakati akifungua
kikao cha kamati hiyo cha siku mbili kilichofanyika kwenye ukumbi wa
mkutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi uliopo Jijini
Dar es Salaam, Jaji Lila, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika mahakamani na wana
majukumu tisa ya kuyafanyia kazi.
‘‘Tutumie kikao hiki kubadilishana
uzoefu na kuzitafutia ufumbuzi changamoto tunazokabiliana nazo katika
matumizi ya TEHAMA ukitaka kutatua tatizo ni lazima uliweke bayana na
kulitafutia ufumbuzi, ’’ alisema Mwenyekiti huyo.
Lila aliongeza kwamba kamati hiyo
imepewa majukumu mbalimbali ya kuyatekeleza ili kuhakikisha eneo la
TEHAMA linatekelezwa ipasavyo, hivyo aliwataka wajumbe hao kutoa
ushauri wa kuendelea kuboresha eneo hilo.
Alifafanua kuwa mifumo ya TEHAMA
iendelee kuboreshwa iwe ya manufaa kwa wananchi na Mahakama pia
kuwataka wajumbe wa kikao hicho kuyataja maeneo yanayotakiwa kuboreshwa.
Kwa upande wake Katibu wa kamati
hiyo, ambaye pia Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Enock Kalege akitoa taarifa ya maendeleo ya teknolojia hiyo, alisema
imeleta matokeo chanya katika shughuli mbalimbali za Mahakama licha
ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto kama vile rasilimali fedha na watu
kwa ajili ya kuendelea kulitekeleza jukumu husika.
Kalege alisema kwamba teknolojia
hiyo pia inasaidia kuwa na takwimu sahihi kama vile vifaa vya TEHAMA
ili kuweza kuboresha na kupanga mipango ya sasa na baadae kwa faida
ya Mahakama.
‘‘Tumefanikiwa kukamilisha jukumu
hili la TEHAMA kwa asilimia 71 kupitia miradi ya uwekezaji kwenye eneo
hili, na tunaendelea kutekeleza asilimia 29 iliyobakia,’’
alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu eneo hilo,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma alisema kwa
upande wa kufungua mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao limeendelea
kutekelezwa kama ilivyoagizwa na Jaji Mkuu wa Tanzania.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru alisema ili kuhakikisha teknolojia
hiyo inaendelea kurahisisha huduma ya utoaji haki na kupunguza gharama
za uendeshaji wa shughuli tofauti za Mahakama ni vema watumishi
wakaendelea kujengewa uwezo na kubadili mitazamo yao.
No comments :
Post a Comment