Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Maonyesho ya 44 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam , Barabara ya Kilwa jijini Dar
es salaam, Julai 3, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,
amesema Serikali kupitia mpango wa maboresho ya
mazingira ya biashara
nchini (Blue Print) imeweza kufuta tozo 163 kati ya 173 zilizokuwa
zikisababisha kero na usumbufu kwa wafanyabiashara nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa
Maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DIFT) leo Ijumaa
(Julai 3, 2020), Waziri Mkuu Majaliwa alisema jitihada hizo za Serikali
zinalenga kukuza mchango wa sekta ya biashara katika pato la taifa
nchini.
Majaliwa alisema kupitia maboresho ya Blue Print,
kati ya tozo hizo tozo 114 ni za sekta ya kilimo na mifugo, tozo 5
kutoka Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) na tozo 44 kutoka Shirika
la Viwango Tanzania (TBS) ambazo zililalamikiwa na wafanyabiashara
kutokana na kutoza gharama kubwa wakati wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje
ya nchi.
‘’Kufutwa kwa tozo hizo
kumewezesha ongezeko la usajili wa taasisi ya OSHA kwa nafasi 16657
mwaka 2019 ikilinganishwa na nafasi 11663 mwaka 2018, hivyo Serikali
itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuchukua hatua
mbalimbali ikiwemo kutunga Sheria za Uwezeshaji Biashara’’ alisema
Majaliwa.
Kwa mujibu wa Majaliwa alisema
Serikali pia inaendelea kupitia majukumu ya mamlaka mbalimbali za
udhibiti ili kuhakikisha zinawawiana kimajukumu hatua inayolenga
kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara pindi wanapohitaji huduma
mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hizo.
Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa
Serikali pia itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara kwa kuweka
mazingira bora na rafiki ili kuziwezesha sekta za viwanda na biashara
kuendelea kuvutia wawekezaji na kuchangia katika ukuzaji wa uchumi wa
nchi.
Aliongeza kuwa maonesho ya mwaka
ya 2020, yamewekwa kimkakati ili kuwezesha shughuli za mazao, biashara
pamoja na huduma kuweza kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi,
hatua inayolenga kuziwesha sekta za kilimo, biashara kuweza
kujitosheleza na mahitaji ya bidhaa muhimu ikiwemo chakula.
Akizungumzia taarifa ya hivi
karibuni iliyotolewa na Benki ya Dunia, kuitangaza Tanzania kuingia
katika nchi ya kipato cha kati, Majaliwa alisema juhudi hizo zimetokana
na msukumo uliowekwa na Rais Dkt. John Magufuli wa kujenga sera imara za
uchumi usio na utegemezi.
‘Mafanikio haya yanaiweka Tanzania
katika ramani ya dunia, jambo kubwa ni kuwa tumeingia katika nchi ya
kipato cha kati miaka 5 kabla ya malengo tuliyojiwekea katika kuifikia
hatua hiyo mwaka 2025’’ alisema Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda
na Biashara, Innocent Bashungwa alisema maonyesho ya mwaka 2020 yamepata
mafanikio makubwa licha ya kuwepo tishio kwa tishio la ugonjwa wa COVID
19 kwani jumla ya washiriki 2880 wameshiriki maonyesho hayo wakiwemo
washiriki wa ndani 2837 na washiriki 43 kutoka nje ya nchi.
Bashungwa alisema katika kuwezesha
sekta za viwanda na biashara zinaendelea kupiga hatua nchini, Serikali
imeendelea kuzihamasisha taasisi za kifedha ikiwemo mabenki na kutoa
mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanaojitokeza kwa ajili ya
ujenzi wa viwanda vidogo katika maeneo mbalimbali nchini.
‘Tuna mkakati tuliojiwekea baina
ya taasisi yetu ya SIDO na Benki ya Azania ya kupeleka mitaa ya SIDO
Mikoani kwa ajili na taasisi zote za kifedha zikiiga mfano huu itakuwa
rahisi kuwatambua wajasiriamali hao na kuweza kuwapa mikopo
inayostahili’’ alisema Bashungwa.
Aidha Bashungwa alisema katika
kipindi cha miaka mitano ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano jumla
ya 8477, vilimeanzishwa ambapo jumla ya ajira 482,601 zimeweza kutolewa
kwa watu mbalimbali.
‘’Wakati wa Janga la COVID, Sisi
Tanzania kupitia viwanda vyetu vya ndani tuliweza kuzalisha barakoa na
vitakasa mikono kwa kuwa kwani kila nchi ilizalisha bidhaa hizo kwa
mahitaji yake, tunampongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa maono ya ujenzi
wa viwanda ambapo leo yametuvusha katika janga la COVID-19 kupitia vifaa
vilivyozalishwa na viwanda vyetu’’ alisema Bashungwa.
Kauli mbiu ya Maonyesho ya 44 ni ‘Uchumi wa Viwanda kwa Ajira na Biashara Endelevu’’.
No comments :
Post a Comment