Friday, July 10, 2020

KUSAYA AIPONGEZA CPB KWA KUPATA SOKO LA UNGA SUDAN KUSINI



Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa anakagua mfuko wa unga bora wa mahindi unaozalishwa na kiwanda cha kusagisha  nafaka CPB Tawi la Iringa leo. Kushoto ni Meneja  wa CPB Tawi la Iringa Kalungi Titina.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama maghala ya kuhifadhia nafaka wakati alipotembelea kukagua utendaji kazi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchangannyiko tawi  la Iringa leo. 
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( aliyea suti blu) akiwa katika picha ya pamoja viongozi wa mkoa wa Iringa leo alipoanza ziara ya kikazi. Kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Happiness Seneda.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika mtambo wa kusaga mahindi katika kiwanda cha usagishaji CPB Iringa.Kiwanda hicho kina uwezo wa kusaga tani 60 za unga wa mahindi kwa siku.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akikagua shehena ya unga bora wa mahindi unaosubiri kupelekwa sokoni baada ya kuzalishwa katika kinu cha usagishaji CPB Iringa.
Picha na habari na Wizara ya Kilimo.
………………………………………………………………………………………………
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ametoa pongezi kwa Bodi ya Nafaka na
Mazao Mchanganyiko ( CPB) kwa kazi nzuri ya kuzalisha unga bora wa mahindi unaokidhi viwango vya kimataifa.
Kusaya ametoa pongezi hizo leo wakati wa ziara yake mkoani Iringa leo alipokagua  kiwanda cha usagishaji nafaka cha CPB Tawi la Iringa na kufurahishwa kusikia kuwa wameanza kuuza unga wa mahindi nchini Sudan Kusini.
” Nimeridhishwa sana na utendaji kazi wa Bodi ya CPB .Tumeanza vizuri kuzalisha bidhaa kwenye kiwanda hiki na masoko tayari yapo.Onyesheni utofauti katika ubora na viwanda vingine binafsi.’ alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo amewaagiza watumishi na viongozi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuonyesha utofauti wa ubora na iliyokuwa NMC ambayo ilishindwa kuendeleza viwanda hivi .
” Mnatakiwa mfanye biashara ,tusipate hasara hivyo tuweke mikakati ya kupata mahindi ya kutosha na kutafuta masoko ndani na nje ili Bodi ijiendeshe kwa faida ” alisema Katibu Mkuu Kusaya.
Katibu Mkuu huyo ameahidi kuendelea kusaidia utatuzi wa changamoto za upatikanaji mitaji ili Bodi itekeleze mkakati wake wa kujiendesha kibiashara zaidi na kutimiza lengo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuona viwanda vya ndani vinafufuliwa  na kuzalisha ajira na masoko.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya CPB Dkt. Anselm Moshi alisema imefanikiwa kupata soko la unga tani 1000 kupeleka Sudan Kusini kutokana na kuzalisha bidhaa bora.
” Tayari hadi sasa tumefanikiwa kuuza unga bora wa sembe tani 600 kati ya tani 1000 zinazotakiwa Sudani Kusini katika tenda tuliyoipata” alisema Dkt.Moshi
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko hadi kufika mwezi Juni mwaka huu imetumia shilingi Bilioni 9.7 kununua mahindi  tani  13,606 katika kituo chake cha Iringa.
Kiwanda cha kusaga unga bora wa mahindi CPB Iringa kina uwezo wa kusaga tani 60 za unga kwa siku.
Dkt.Moshi ametaja mafanikio waliyopata katika mkoa wa Iringa kwa ni pamoja na kuuza tani 5000 za mahindi kwa East Africa Exchange ya Rwanda,tani 4000 kwa Shirika la Chakula (WFP)  na tani 5,721 zimesagishwa na kuuza kama unga na pumba
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Happiness Seneda alimweleza Katibu Mkuu kuwa wakulima wa zao la chai hususan Wilaya ya Kilolo wanapaswa kusaidiwa ili kiwanda kifanye kazi.
Seneda aliongeza kusema Wizara ya Kilimo isaidie jitihada za kufufua kiwanda cha chai Kilolo kwani hakiajaanza kazi muda mrefu.
Katibu Tawala huyo waa mkoa aliomba Wizara ya  Kilimo kufanyia kazi mfumo wa stakabadhi ghalani ili wakulima wapate manufaa ya bei kwani uwepo wa kauli kuwa wanaweza uza mazao yao nje ya mfumo bado haijaeleweka vizuri kwa watendaji.

No comments :

Post a Comment