Sunday, July 5, 2020

KATIBU MKUU ASISITIZA UFUGAJI WENYE TIJA NCHINI.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel akizungumza mara baada kutembembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika maonesho ya biashara kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel  akiangalia ufugaji wa kuku namna wanavyofaata taratibu  za ufugaji
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa  Elisante Ole Gabriel akiwa katika Banda la  Bodi ya Nyama kuangalia utaratibu wa uandaaji nyama kisasa 
Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof.Elisante Ole Gabriel amewataka wafugaji nchini kuzingatia ubora wa mifugo yao na sio kuangalia zaidi wingi wa mifugo waliyonayo kwa kuwa ubora wa mifugo ndio utakaosaidia kupata mazao yaliyo bora yenye kuwanufaisha kiuchumi.

Alisema kuwa  mfugaji akiweza kubadilika na kufuga kisayansi kwa maana ya kufuga kwa tija na akaanza kupata mazao ya mifugo yaliyo bora, ndipo hapo atakapofaidika na kazi yake ya ufugaji.

Katibu Mkuu ametoa wito huo leo  wakati akiwakaribisha wawekezaji wa Kampuni ya kuchakata na kusambaza Nyama ya Tanfroz  Limited inayomilikiwa na wawekezaji kutoka nchini Ubelgiji na Ufaransa, walipofika Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) jijini  Dodoma kwa lengo la kutambulisha na kuomba ushirikiano katika mradi  huo hapa nchini.

Prof.Gabriel aliongeza kuwa azma ya serikali hii ya awamu ya tano chini ya Rais, Dk.John Pombe Joseph Magufuli, inayosisitiza uchumi wa viwanda, haiwezi kufanikiwa vizuri bila kuboresha mifugo ambayo mazao yake hutegemewa kama malighafi za viwandani.

Katibu Mkuu aliwaahidi ushirikiano kutoka kwake na wataalam wake katika hatua mbalimbali kwa lengo la kufanikisha mradi huo ambao ukishaanza rasmi utawanufaisha wawekezaji na wafugaji wa hapa nchini na kwa majaribio alisema mradi huo umeanzia mkoani Iringa katika maeneo ya Mgagao ambapo kuna shamba lenye ng,ombe zaidi ya mia mbili.

Akiongea kwa niaba ya Kampuni hiyo, Mkurugenzi wa kampuni ya Tanftoz Limited Bw.Luc Battel, alisema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya uwekezaji katika Sekta ya Mifugo kutokana na wingi wa mifugo iliyopo nchini, ila akasisitiza kuwa mifugo yenye manufaa ni ile yenye ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa Tanzania itafanikiwa kupata zaidi masoko ya nyama katika nchi za mashariki ya mbali na kwingineko duniani iwapo tu ng,ombe au mbuzi watafugwa katika mazingira bora na kuepushwa na maradhi yakiwemo magonjwa ya miguu na midomo.

Aidha aliongeza kuwa uboreshaji wa mbari ni muhimu katika kupata mazao bora  ya mifugo kwa maana ya nyama maziwa na ngozi ambayo hutumika kama malighafi katika viwanda mbalimbali  hapa nchini.

Akiongea katika kikao hicho meneja wa kampuni ya CRV Bw.Hielke Sportel naye alisema kuwa ili kufanikiwa katika uboreshaji wa mbari nchini, ni vema wafugaji wakawa na ushirikiano katika kubadilishana mbari na elimu mbalimbali za ufugaji bora wenye tija.

Aidha taasisi ya utafiti wa mifugo nchini (TALIRI) na vyuo vya mafunzo ya mifugo pia zimetakiwa zitumike kuwainua wafugaji kwa kuwapelekea taarifa za tafiti na elimu mbalimbali za kuboresha mifugo yao kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti nchini (TALIRI) Dk.Eligy Shirima aliwashukuru wawekezaji hao kwa kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya mifugo na kuahidi kuwapa ushirikiano kila panapostahili ili kuwainua wafugaji nchini na hatimaye kuweza kutoa mchango katika uchumi wa taifa.

No comments :

Post a Comment