Saturday, July 18, 2020

HUDUMA CCBRT ZAMKOSHA MSAJILI WA NGOs


Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kulia) moja ya zao la kazi za mikono za wanufaika wa huduma zinazotolewa na Hospitali hiyo waliowezeshwa kutengeza bidhaa mbalimbali wakati wa ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kulia ni Msajili wa Mashirika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao.
 Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga (wa pili kushoto) Msajili wa Mashirika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao (wa tatu kushoto) na Maafisa wengine kutoka Ofisi ya Msajili wa NGOs wakati wa ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika yasiyo ya Kiserikali nchini.Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW.

Msajili wa Mashirika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini,Vickness Mayao ameeleza kuridhishwa na ubora na viwango vya huduma zinazotolewa na Hospitali ya CCBRT za kuwahudumia Watanzania wanaokabiiliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya.

Mayao ameyasema hayo jijini Dar Es Salaam alipofanya ziara katika Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali sambamba na uhakiki wa matumizi ya fedha ndani ya Mashirika hayo ili kuendana na mwongozo wa Mashirika unayosisitiza uhalisia wa fedha na matumizi yake.

“Hii ni ziara ya kujiridhisha na fedha zinazotumiwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kuhakikisha fedha zinazoingia kwa jina la Tanzania, zikilenga kuwanufaisha Watanzania zisitumike kinyume” alisisitiza

Aliongeza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatakiwa kuhakikisha fedha zinazotolewa na wafadhili kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali zinatumika kulingana na malengo yake na hivyo kuwanufaisha walengwa waliokusudiwa.

“Hapa nieleze tu kwamba CCBRT wanafanya kazi nzuri sana katika huduma zao kwa walengwa na hata katika miradi wanayoitekeleza, Mfano ni Jengo hili hapa kweli tunaona kwamba wamefanya vizuri sana” alisema.

Aidha, amesema kuwa baadhi ya Mashirika yaliyokaguliwa pamoja na kutekeleza majukumu yake, hayatekelezi miradi kwa ukamilifu wake na hivyo kusababisha maswali na hoja katika matumizi ya fedha zinazotolewa na wafadhili.

Akizungumzia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Dkt. Richard Sambaiga amesema CCBRT imekuwa mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma hasa za afya kwa watu ambao wengi wana kipato cha chini.

“Niseme ukweli, Kazi hii kubwa inayofanywa na CCBRT ilitakiwa kufanywa na Serikali, Lakini kwa kuwa Serikali imekasimu kazi hii kwa NGOs kwa utaratibu unaokubalika hivyo ni lazima lazima kazi hizo kufanyika kwa viwango vikubwa kama inavyofanya CCBRT”alisisitiza.

Pia amefafanua kuwa mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliotolewa na Serikali hivi karibuni hauna kusudio la kuyabana Mashirika hayo kama inavyodhaniwa na baadhi wadau bali umelenga kuweka uwazi katika matumizi ya fedha za miradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Brenda Msangi amesema Hospitali hiyo inafanya kazi ya kuwa kubwa ya kuwarejesha watu wenye matatizo mbalimbali ya kiafya katika mfumo wa kawaida ili waweze kufurahia maisha kama walivyo watu wengine.

Brenda amesema kuwa Hospitali ya CCBRT inatoa huduma mbalimbali za afya ikiwa ni pamoja na upasuaji kwa watu wenye miguu pinde na kuwapatia vifaa saidizi, upasuaji na urejeshaji wa katika hali ya kawaida kwa watoto wanaozaliwa wakiwa na midomo sungura, utoaji wa huduma kwa wanawake wenye ugonjwa wa fistula pamoja na kutoa huduma nyingine za Matibabu.

No comments :

Post a Comment