*******************************
Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Dkt. Hasaan Abbasi ametoa saa 24 kwa Bodi na Menejimenti ya
Chama cha
Hakimiliki na Haki Shirikikishi Tanzania (COSOTA) kuwasilisha
mkakati wa namna Wasanii watakavyonufaika kupitia Taasisi hiyo.
Katibu Mkuu
ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya
makabidhiano ya chama hicho kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda
Wizara anayoisimamia.
“Tumshukuru Rais
John Magufuli kwa sababu mjadala wa kwa nini COSOTA ipo Wizara ya
Viwanda na Biashara umekuwa mrefu, lakini ndani ya saa 24 tangu Julai
12, 2020 Rais aliweza kusaini Waraka wa kuihamishia Wizarani kwetu”,
Dkt. Abbasi.
Aliongeza kuwa
taasisi hiyo inatakiwa kuhakikisha kuwa inawasaidia wasanii katika
kusimamia haki zao ili kuondokana na umaskini na kufikia malengo
waliyojiwekea katika kazi zao za Sanaa kwani ni jukumu la taasisi hiyo
kuhakikisha kuwa inamsaidia msanii kutoka kuwa msanii maarufu maskini na
kuwa msanii maarufu tajiri.
Aidha, Dkt.
Abbasi aliongeza kuwa taasisi hiyo kuhamia Wizara ya Habari ni jambo
jema katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Idara ya Maendeleo ya
Sanaa kwa kuhakikisha wasanii wanapata huduma kwa wakati na chini ya
mwamvuli mmoja.
Dkt. Abbasi
alieleza kuwa kwa sasa kuna mabadiliko na mafaniko mengi katika sekta ya
Sanaa ambapo Juni 26, 2020 Wizara ilifanikiwa kutangaza Kanuni za
Filamu na Michezo ya Kuigiza kupitia gazeti la Serikali namba 488 ambapo
kuna manufaa mengi kwa wasanii ikiwemo kupungua kwa tozo za filamu
kutoka shilingi 500,000/= hadi shilingi 50,000/= lengo ikiwa ni
kuwawezesha kutengeneza filamu zenye ubora.
Vile vile faida
nyingine ya kanuni hizo ni kuwepo kwa kamati ya kutetea haki za wasanii
ambapo Serikali imefanikiwa kurejesha kiasi cha milioni 200 ambapo kati
ya hizo, shilingi milioni 65 zilirejeshwa kwa familia ya marehemu Mzee
Majuto pamoja na kiasi cha milioni 20 zilirejeshwa kwa familia ya
marehemu Steven kanumba kutoka katika kampuni ambazo ziliingia mikataba
na Wasanii hao.
Naye Katibu Mkuu
kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe ameutaka
uongozi wa taasisi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Habari
katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wa
Afisa Mtendaji wa COSOTA, Doreen Sinare ameahidi kusimamia kwa ufanisi
majukumu ya taaasisi hiyo inayosimamia haki miliki pamoja na kusajili
wabunifu kukusanya na kugawa mirabaha na kusuluhisha mogogoro
inayohusiana na haki miliki pamoja na kutoa ushauri.
Nao baadhi ya
wasanii walitoa maoni yao kuhusiana na makabidhiano haya ambapo Msanii
wa Filamu na Michezo ya kuigiza, Vyonne Cherrie (Monalisa) ameeleza
kufurahishwa na uamuzi wa kuhamishwa kwa taasisi ya COSOTA kwenda Wizara
ya Habari kwani imeepusha milolongo mingi ya ufuatiliaji wa kazi za
filamu na sanaa.
Huku Msanii wa
Muziki wa kizazi kipya, Kala Jeremiah alisema kuwa ulinzi na ulezi wa
sanaa unatakiwa kwenda pamoja hivyo ni jambo jema kwa COSOTA kuhamia
Wizara ya Habari ili waweze kufanya kazi kwa ushrikiano na BASATA.
No comments :
Post a Comment