Mtaalam wa maabara kutoka Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jesca Mlay akimweleza Bilionea Saniniu
Laizer namna ambavyo maabara ndogo iliyopo katika banda la JKCI
inavyofanya kazi ya huduma za vipimo vya damu vilivyotolewa kwa wananchi
wanaotembelea banda hilo alipotembelea banda la JKCI wakati wa Maonesho
ya 44 ya Biashara ya Kimataifa leo Jijini Dar es Salaam
Daktari kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo akimwelezea Bilionea Saniniu
Laizer mwitikio wa wananchi kufanya uchunguzi wa afya ya moyo katika
banda la JKCI alipotembelea banda hilo kuona huduma zinazotolewa wakati
wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa leo Jijini Dar es Salaam.
………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum
Bilionea Saniniu Laizer aipongeza
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma za
ushauri na upimaji
wa magonjwa ya moyo wanazozitoa kwa wananchi wanaotembelea banda la
Taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya
Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo amezitoa leo
alipotembelea banda la JKCI kwa ajili ya kuona huduma wanazozitoa pamoja
na kupata elimu ya lishe na magonjwa ya moyo.
Lazier alisema huduma zinazotolewa
ni nzuri kwani zinaokoa maisha ya watu wenye matatizo ya moyo ambao
baada ya afya zao kuimarika watakua sehemu ya kukuza uchumi wa nchi
yetu.
Kwa upande wake Daktari wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alimshukuru bilionea
Laizer kwa kutembelea katika banda lao na kujionea huduma mbalimbali za
upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo zinazotolewa.
Dkt. Pedro ambaye pia ni mtafiti
wa magonjwa ya moyo alisema ugeni wa Bilionea Laizer katika banda la
hilo utawavutia wananchi wengi kufanya vipimo vinavyotolewa na Taasisi
hiyo.
Dkt. Pedro alisema mwitikio wa
wananchi katika banda la JKCI kwa ajili ya kufanya uchunguzi umekua
ukiongezeka mwaka hadi mwaka kwa miaka minne ambayo taasisi hiyo
imeshiriki maonyesho Sabasaba.
Mbali na huduma za upimaji wa afya
ya moyo na magonjwa mengine sugu, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete pia
imejikita kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa jamii ili iweze
kufahamu sababu hatarishi za magonjwa ya moyo na magonjwa mengine sugu.
“Tulichojifunza katika ushiriki
wetu kwenye maonyesho haya ni kuwa wananchi wengi wana shauku ya kujua
afya zao ila wengi hawajui ni wapi na kwa namna gani wataweza kufika
sehemu stahiki kufanya uchunguzi.
“Uzito mkubwa na shinikizo la damu
yameonekana kuwa ni matatizo mawili makubwa ambayo yanakuwa kwa kasi
mwaka hadi mwaka katika jamii ya kitanzania.
Ni rai yetu kwa taifa zima kuwa
kinga ni bora kuliko tiba hivyo jamii nzima ivalie njuga sababu
hatarishi za magonjwa sugu ikihusisha uzito sahihi, ulaji unaofaa,
mazoezi ya mara kwa mara, kunywa pombe kwa kiasi au kuacha kabisa, na
kutovuta sigara,”. alisema Dkt. Pedro.
Hadi sasa jumla ya watu 1940
wamefanyiwa vipimo katika banda hilo ambapo vipimo vya viashiria vya
magonjwa ya moyo ambavyo ni uzito, urefu, sukari mwilini na shinikizo la
damu (BP) vimefanyika bila malipo na vipimo vya damu, ECG na ECHO
wananchi wanachangia kiasi kidogo cha fedha.
No comments :
Post a Comment