Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Dk. Edwin P. Mhede, akikabidhiwa
Tuzo ya Benki Bora na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB- Ruth
Zaipuna. Akishuhudia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB –
Filbert Mponzi
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB Dk.Edwin P. Mhede, Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB- Ruth Zaipuna na Afisa Mkuu wa
Wateja Binafsi na Biashara wa NMB – Filbert Mponzi wakiifurahia Tuzo
walioipokea kwa kuwa Benki Bora Tanzania.
*************************************
Benki ya NMB imekuwa benki bora nchini Tanzania kwa mara ya nane mfululizo baada ya
kuzibwaga benki zingine 40 nchini.
Tuzo hiyo imetolewa na
Euromoney, ambalo ni jarida la kimataifa la masuala ya kifedha
linaloongoza duniani lenye makao makuu yake jijini London, Uingereza.
Tuzo hii inaonesha kuwa Benki
ya NMB ni zaidi ya taasisi inayotoa huduma za kifedha na kuwa kichocheo
muhimu cha mabadiliko ya kiuchumi kupitia utoaji huduma za kibenki kwa
njia ya kidigitali.
Akiongea wakati wa kukabidhiwa
tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB – Dk.
Edwin Mhede alisema baada ya Tanzania kufikia uchumi wa kati, Benki ya
NMB inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuchangia zaidi
katika ukuaji wa uchumi kwenda katika hatua ya juu zaidi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna alisema: “Leo hii tunajulikana
kama benki imara zaidi, yenye huduma za ubunifu wa kiteknolojia.
Tumedhamiria kuwa zaidi ya taasisi ya huduma ya fedha kwa kuendelea
kuchochea mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yetu na kuboresha maisha ya
Watanzania wenzetu kwa kutoa huduma zinazowafaa na kukidhi mahitaji na
mipango yao.”
Tuzo hiyo hutolewa kwa kuzingatia
vigezo kadhaa kwa benki zilizopendekezwa ukiwamo ufanisi wa hesabu za
fedha na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma
jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na wajibu wa benki kwa
jamii inayoihudumia. Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki,
mapato yatokanayo na biashara ya hisa, mapato yatokanayo na mali za
kampuni, pato litokanalo na riba, uwiano wa fedha na gharama za
uendeshaji, kiwango cha amana za wateja, Kiwango cha Mikopo katika soko,
Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo chechefu,
uwiano wa hasara itokanayo na mikopo chechefu.
Akizungumzia mchakato wa
kumpata mshindi wa tuzo ya benki bora nchini, mhariri wa Jarida la
Euromoney, Clive Horwood alisema: “Tunaendelea kuzitambua taasisi bora
zaidi katika kila nchi zinazotoa huduma za fedha. Kwa kila mwaka, ukubwa
ni muhimu lakini sio kigezo muhimu zaidi. Faida ya benki husika ni
muhimu kama ilivyo uwezo wa kuthibitisha uwezo wa kukua, ufanisi wa
kiutendaji ikilinganishwa na washindani wake sokoni na uwezo wa kukabili
mazingira ya soko yanayobadilika pamoja na kukidhi mahitaji ya wateja.”
No comments :
Post a Comment