Bi. Anna Henga
Freetown, Sierra Leone, Julai 13, 2020
Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika (African
NGO Council) imemteua Bi. Anna Henga (Wakili) kuwa mjumbe mpya wa bodi
hiyo. Wakili Anna Henga, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), atakuwa mjumbe wa bodi ya Baraza hilo
kwa muda wa miaka miwili, kuanzia Julai 2020.
Katika barua ya uteuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Asasi za
Kiraia Barani Afrika, Rebecca Paulson, amempongeza Anna Henga kwa uteuzi
huo na kumkaribisha katika bodi ya wakurugenzi ya Baraza hilo.
“Nina furaha sana kukukaribisha kuitumikia Bodi ya Wakurugenzi ya
Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika. Katika mkutano wa Kamati ya
Uteuzi ya Bodi hii, uliofanyika Julai 1, 2020, wajumbe waliafiki
kukuteua kuwa mjumbe mpya ya Bodi ya Wakurugenzi. Hivyo, kwa barua hii
umeteuliwa rasmi kuongoza na kutoa uelekeo wa kimkakati kwa Baraza la
Asasi za Kiraia Barani Afrika (African NGO Council) kwa kipinfdi cha
miaka miwili ijayo kuanzia Julai 2020”,amesema Rebecca katika barua ya uteuzi.
Kwa upande wake, Anna Henga ameonesha furaha yake kwa kupata nafasi hiyo
adhimu huku akiahidi kutoa mchango wake katika kufikia malengo ya
Baraza hilo.
“Nimefurahishwa sana kupata wito huu wa kuteuliwa. Ni heshima kubwa
kupata nafasi hii adhimu ya kulitumikia bara la Afrika kupitia Baraza la
Asasi za Kiraia (African NGO) Council). Baraza hili ni mwamvuli wa
asasi za kiraia kwa baraza la Afrika na ninatazamia kutoa mchango wangu
katika kufanikisha malengo ya Baraza hili”,amesema Henga.
Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Asasi za Kiraia Afrika inaundwa na
wajumbe sita, ambao hutumikia bodi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Moja ya kazi kuu ya bodi hiyo ni kuongoza Baraza la Asasi za Kiraia
Afrika katika kuweka mikakati na sera za zitakazowezesha kufikia malengo
ya Baraza hilo.
Kuhusu Baraza la Asasi za Kiraia Afrika (African NGO Council)
Baraza la Asasi za Kiraia Afrika (African NGO Council) ni taasisi ya
kikanda inayoundwa na mashirika ya kimataifa, kikanda na kitaifa
yanayofanya kazi kwa lengo la kufikia uendelevu wa mazingira, kudumisha
amani, kulinda haki za binadamu, utawala bora na maendeleo endelevu ya
binadamu katika bara la Afrika.
No comments :
Post a Comment