NA WAJMW-DODOMA
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
ameziagiza Hospitali zote nchini za Serikali na binafsi, Zahanati na
Vituo vya Afya kuacha kuwadai damu wagonjwa kabla ya kuwapa huduma.
Waziri
Ummy amesema hayo jana wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya
wachangia damu duniani yenye kauli mbiu “Damu Salama inaokoa maisha”
ambayo kitaifa yamefanyika katika kituo cha kidogo cha damu salama
kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma.
“Nazitaka
Hospitali zote za Serikali na binafsi kuacha tabia ya kuwadai damu
wagonjwa na ndugu kabla ya kumpatia mgonjwa huduma, mnatakiwa kutoa
huduma kwanza na masuala ya wanandugu kuambiwa walete watu wa kuchangia
damu kabla ya huduma ni kinyume na taratibu na kanuni za utoaji wa
huduma za afya”. Amesisitiza Waziri Ummy.
Waziri
Ummy amezitaka Hospitali zote za Serikali na binafsi na vituo vya Afya
nchini kushirikiana na Mpango wa taifa wa damu salama katika kukusanya
damu na wasibaki wao kuwa watumiaji wa damu bila kuweka fedha au
jitihada zozote za ukusanyaji.
Waziri
Ummy amesema takwimu zinaonyesha kuwa, wakati Serikali ya awamu ya tano
inaingia madarakani mwaka 2015 jumla ya chupa za damu 104,632
zilikusanywa, kupimwa na kusambazwa. Idadi hii imeongezeka hadi kufikia
chupa 309,376 ziizokusanywa mwaka 2019 ambayo ni ongezeko la chupa
204,744 ambayo ni sawa na asilimia 195 ikilinganishwa na chupa za damu
zilizokusanywa mwaka 2015.
“Tumeboresha
huduma kwenye Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa kuwapitia mashine za
kisasa za kupimia damu ambapo uwekezaji huo umegharimu karibu Bilioni
13. Kwa kutumia mashine hizi Mpango una uwezo wa kufanya vipimo 4000 kwa
masaa 6 kutoka vipimo 1404 kwa mashine zilizokuwepo awali kabla
Serikali ya Awamu ya Tano haijaingia madarakani”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha,
Waziri Ummy amesema tendo la kuchangia damu ni jema na linalojenga utu
hivyo amewashukuru wachangia damu wote nchini hususani wale wanaochangia
mara kwa mara. Pia amewahamasisha wananchi ambao hawajawahi kuchangia
waweze kuchangia damu angalau mara moja kwa mwaka.
Waziri
Ummy ametaka Mpango wa damu salama nchini kuweka utaratibu wa kufikia
kaya zote nchini na kuhamasisha angalau awepo mtu mmoja kwa kila kaya
ambae atakua anachangia damu mara kwa mara ili kuweza kukidhi mahitaji
ya kitaifa ya damu salama.
Mwisho
Waziri Ummy ameipongeza mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kuweka mikakati
mizuri ya uchangiaji damu ambapo mgonjwa mwenye uhitaji wa damu
anahudumiwa kwanza kabla ya kutafuta ndugu wa kuchangia damu.
No comments :
Post a Comment