Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipokea funguo, kutoka kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi, kama ishara ya kukabidhiwa nyumba 103, kwa
akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini,
zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akimkabidhi funguo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George
Simbachawene, kama ishara ya kukabidhi nyumba 103, kwa akijili ya Makazi
ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini, zilizojengwa na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
George Simbachawene, akimkabidhi funguo, Kamishina Jenerali wa Uhamiaji,
Dkt. Anna Makakala, kama ishara ya kukabidhiwa nyumba 103, kwa akijili
ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini,
zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020.
Kamishina Jenerali wa Uhamiaji,
Dkt. Anna Makakala, akionesha ishara ya funguo, baada ya kukabidhiwa
nyumba 103, kwa akijili ya Makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya
Uhamiaji nichini, zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Juni,
2, 2020.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akikata utepe, wakati akizindua nyumba 103 za Makazi ya Maafisa na
Askari wa Idara ya Uhamiaji nichini, zilizojengwa na Shirika la Nyumba
la Taifa (NHC) Juni, 2, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………..
*Ni utekelezaji wa uamuzi wa Rais Dkt. John Magufuli
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameikabidhi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nyumba 103
zenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni tano kwa ajili ya makazi ya
Maafisa na Askari wa
Idara ya Uhamiaji nchini zilizojengwa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ikiwa ni
utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Baada ya
kukabidhi nyumba hizo, Waziri Mkuu amesema kwamba makazi hayo yawe
chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini katika
kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya
wateja ambao ndiyo waajiri wao.
Akikabidhi nyumba
hizo leo (Jumanne, Juni 2, 2020), Waziri Mkuu amesema “Uamuzi huu wa
Mheshimiwa Rais ambao leo hii tunashuhudia utekelezaji wake kupitia
makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya Maafisa na Askari wa Uhamiaji
kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo waliishi
uraiani.”
Ameongeza kuwa
“Ni ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya Shirika
la Nyumba la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya vielelezo vya
utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya
kuwapatia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba 103.”
Pia, Waziri Mkuu
amesema “Nyote mtakubaliana nami kwamba leo ni siku muhimu kwa sekta ya
nyumba kwani ujenzi wa nyumba za namna hii ni muhimu katika kuimarisha
upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi za Serikali sambamba na
kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”
“Vilevile,
utekelezaji wa mradi huu umetoa ajira zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na
ajira 800 za mafundi na ajira 200 kwa watoa huduma za chakula yaani mama
lishe. Upatikanaji wa ajira hizo umechangia kuongeza kipato kwa
walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya umaskini.”
Amesema ujenzi wa
majengo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 inayosisitiza ujenzi wa majengo ya ofisi
na makazi kwa watumishi wa umma kwa lengo la kuipunguzia Serikali
gharama kubwa ya kodi ya pango pamoja na kuimarisha utendaji na
uwajibikaji wa watumishi wa umma katika kuwahudumia Watanzania.
Kadhalika, Waziri
Mkuu ametoa wito kwa Shirika la Nyumba la Taifa, kuendelea na kazi
nzuri ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na biashara kwani lengo la
Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ni kuliwezesha Shirika la Nyumba la
Taifa kuwa Mwendelezaji Miliki Mkuu.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema watendaji wa shirika hilo wanapaswa kuongeza kasi ya
ukusanyaji kodi ili kuongeza mapato ya shirika. “Serikali kwa upande
wake, itaendelea kutoa Ushirikiano wa karibu kwa Shirika katika kutatua
changamoto zinazokabili utekelezaji wa malengo ya shirika hili.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa
kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho
mbalimbali kama vile Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti,
vibali vya ukaazi, viza, usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa
njia ya kielektroniki. “Utekelezaji mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji
Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya ushindi wa pasipoti yenye
ubora duniani kwa mwaka 2019.”
Waziri Mkuu
amesema ushindi huo, umelipatia sifa na heshima kubwa Taifa Kimataifa.
“Halikadhalika, nimefurahishwa na taarifa kuwa ujenzi wa Makao Makuu ya
Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea vizuri. Ninawahimiza endeleeni
hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”
Awali, Kamishna
Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliishukuru Serikali ya Awamu ya
Tano kwa kuwezesha Idara ya Uhamiaji, kupata nyumba 103 za makazi kwa
ajili ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kwani hatua hiyo ni kielelezo cha
vipaumbele vya Serikali katika kuboresha makazi ya askari wa vyombo
vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.
“Aidha,
tunalipongeza pia Shirika la Nyumba la Taifa, kwa kubuni mradi mkubwa
kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi ya Wananchi kwa kujenga na
kuuza nyumba kwa bei nafuu, ambapo nasi tumekuwa wanufaika wa mradi huu.
Gharama za nyumba 103 za makaazi ya watumishi wa Idara ya Uhamiaji, ni
kiasi cha sh. 5,306,000,000.”
Alisema
upatikanaji wa nyumba hizo utasaidia Maafisa na Askari wa Idara ya
Uhamiaji kuishi katika maeneo yao maalum, badala ya ilivyokuwa hapo
awali ambapo walilazimika kutafuta nyumba za makazi uraiani. Sambamba na
hilo, itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, kwani
itakuwa ni rahisi kuwapata askari walio katika eneo moja mara
wanapohitajika.
Makabidhiano hayo
yameshuhudiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene,
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Nyumba la Taifa, Dkt. Maulid Banyani, Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo na Maafisa wengine
wa Serikali.
No comments :
Post a Comment