……………………………………………………………………
Na Masanja Mabula,Pemba.
WANAVIKUNDI vya
ujasiriamali Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wamekishukuru
Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar kwa juhudi
zake za
kuwawezesha wanawake kujiinua kiuchumi kupitia vikundi hivyo.
Wakizungumza na
Mwandishi wa habari hizi wamesema kupitia vikundi hivyo vinavyosimamiwa
na TAMWA Zanzibar kupitia mradi wa kuwawezesha Wanawake kiuchumi,
vimewasaidia kuongeza mashirikiano katika shughuli za uzalishaji na
kuongeza hamasa kwa wanawake wengine katika jamii.
Bijuma Hamis Kombo
mwanachama wa kikundi cha Safinia kilichopo Shehia ya Majenzi Micheweni
amesema vikundi hivyo vimekuwa ni mkombozi kwa wanawake wengi kutokana
wengi wao huvitumia kama sehemu ya kujikwamua kiuchumi.
“Vikundi hivi
vimetusaidia kupata sehemu ya kujikwamua kiuchumi kwani kupitia Hisa
tunazoziweka, mwanachama anaweza kukopa kwenye kikundi na kuendeleza
shughuli zake mwenyewe,” alisema Bijuma.
Aidha amesema kupitia vikundi hivyo vimemsaidia kuongeza kipato kwa familia yake kupitia mikopo hiyo.
“Mwanzo kabisa
nilikopa Shilingi laki Moja, nikapasisha leseni ya pikipiki yangu (boda
boda) ili kupata pesa za kuweka hisa na nashukuru Mungu saizi naendelea
na biashara yangu na Hisa naendelea kuweka bila shida yoyote,” alisema.
Nae Asha Moh’d Said
kwa upande wake amesema kupitia vikundi hivyo vimemuwezesha kuongeza
mtaji wa shughuli zake za ufumaji na ushonaji ikiwa ni sambamba na
kuongeza soko lake zaidi.
“Mimi nilikopa
Shilingi Laki Tatu kwenye kikundi changu nikaongezea mtaji wa biashara
ya Vitambaa na Mashuka. Tunashukuru sana vikundi vimetusaidia sisi
Wanawake kukwamuana sisi kwa sisi,” alisema Asha.
Kwa upande wake
Ramla Suleiman Khamis kutoka kikundi cha Tuko Pamoja, amesema licha ya
mafanikio hayo lakini vikundi hivyo vinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa
soko la uhakika wa bidhaa zao jambo linalochelewesha kasi ya maendeleo
yao.
“Tunashukuru sana
TAMWA Zanzibar wametusaidia, sasa umasikini unapungua taratibu kwetu
lakini changamoto yetu kubwa ni Masoko. Tunazalisha Sabuni, Mafuta na
kushona Mashuka lakini sehemu ya kuuza ni kikwazo kikubwa jambo
linalopelekea wengine kutaka kukata tamaa,” alisema.
Aidha wameomba
kupatiwa msaada wa utaftaji wa Masoko ili kuwawezesha Bidhaa zao kuuzika
na kuendelea kuzalisha kwa wingi kwa lengo la kuwainua wanawake
kiuchumi.
Afisa Mradi wa
kuwawezesha Wanawake Kiuchumi TAMWA Zanzibar Ofisi ya Pemba, Asha Mussa
Omar amesema chama hicho kinaendelea kufanyia kazi changamoto
zinazowakabili wanavikundi hao ili lengo la kuwainua kiuchumi liweze
kukamilika.
“Tusikatishwe tamaa
na changamoto zinazotukabili katika vikundi vyetu kwani changamoto ya
upatikanaji wa Soko tunaendelea kulitatua. Lengo la TAMWA Zanzibar ni
kuhakikisha Wanawake wanaondokana na umasikini kupitia shughuli zetu
hizi za vikundi,” alisema Asha.
No comments :
Post a Comment