Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Isihaka Shariff akimuelimisha
Mfanyabiashara wa maduka ya Ikupa Market katika eneo la Tabata Kinyerezi
jijini Dar es Salaam kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati
wa Kampeni endelevu ya Elimu kwa Mlipakodi iliyoanza tangu tarehe 8
Juni, 2020.
Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Catherine Mwakilagala akimuelimisha
Mfanyabiashara wa eneo la Tabata Segerea jijini Dar es Salaam kuhusu
masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa Kampeni endelevu ya Elimu
kwa Mlipakodi iliyoanza tangu tarehe 8 Juni, 2020.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Lameck Ndinda akimuelimisha
Mfanyabiashara wa eneo la Tabata Kisukulu jijini Dar es Salaam kuhusu
masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa Kampeni endelevu ya Elimu
kwa Mlipakodi iliyoanza tangu tarehe 8 Juni, 2020.
PICHA ZOTE NA TRA.
*************************
Na Veronica Kazimoto
Dar es Salaam
11 Juni, 2020
Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) imewaelimisha wafanyabiashara wa maeneo ya Tabata jijini Dar es
Salaam kuhusu Kodi ya Zuio na kutoa wito kwa wamiliki wa majengo, fremu
na
ardhi kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi hiyo ambayo ni asilimia
10 ya kiasi cha malipo walichokubaliana katika mkataba wa upangishaji
ili waiwasilishe TRA.
Akizungumza wakati wa
kampeni endelevu ya elimu kwa mlipakodi ambayo kwa awamu hii itamalizika
kesho jijini hapa, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka hiyo Bw.
Stephen Kauzeni alisema kuwa, kodi ya zuio inatozwa kwa mujibu wa
Sheria ya Kodi ya Mapato na inasimamiwa na TRA hivyo amewataka
wapangishaji kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi hiyo wakati
wanapolipwa kodi ya pango.
“Tangu tumeanza zoezi hili la
elimu kwa mlipakodi tumefanikiwa kupita karibu maeneo yote ya Tabata
ikiwa ni pamoja na Relini, Bima, Barakuda, Kimanga, Kisukulu na
Kinyerezi. Katika maeneo yote haya tumegundua kwamba, baadhi ya wamiliki
wa nyumba za biashara hawaruhusu wapangaji wao kukata kodi ya zuio
ambayo inapaswa kuwasilishwa TRA kwa mujibu wa sheria.
“Tulichokifanya ni kuwaelimisha
wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kodi hiyo na napenda kuchukua fursa
hii kutoa wito kwa wenye nyumba na fremu mbalimbali kuwaruhusu wapangaji
wao kuzuia asilimia 10 ya kiasi cha malipo walichokubaliana kwenye
mkataba wa upangishaji ili wapangaji hao wakiwasilishe Mamlaka ya Mapato
Tanzania,” alisema Bw. Kauzeni.
Bw. Rashid Omary ni mmiliki wa
fremu za biashara wa Tabata Kimanga jijini hapa ambaye amesema kuwa,
amefurahishwa na elimu ya kodi ya zuio aliyoipata kutoka kwa maafisa wa
TRA na amewaomba wamiliki wenzake kuhakikisha wanawaruhusu wapangaji wao
kuzuia asilimia 10 ya kodi ya pango ili fedha hizo ziwasilishwe TRA
kama sheria inavyoelekeza.
“Kama mimi ni mmiliki lakini
nilikuwa sielewi kama wapangaji wangu wanatakiwa kunikata asilimia 10 ya
kodi ya pango tuliyokubaliana kwenye mkataba ili waipeleke TRA. Hivyo
elimu hii imenifungua sana na hivyo napenda kuwashauri wamiliki wenzangu
wawaruhusu wapangaji wao kukata hiyo asilimia 10 kwa sababu kodi hii
itarudi kwetu kupitia maendeleo yanayoletwa na Serikali katika maeneo
yetu tunayoishi, alisema Bw. Omary.
Naye, mmiliki wa maduka ya Ikupa
Market Bi. Hortensia Kimaro ameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania
iwasajili wenye majengo ya biashara ili walipe kodi ya zuio wao wenyewe
kwa sababu baadhi yao ni wagumu kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi
hiyo.
Kodi ya zuio hutozwa katika maeneo
tofauti ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara, mirabaha, hisa,
upangishaji na gawio mbalimbali ambapo kila eneo limepangiwa kiwango cha
asilimia kinachotakiwa kulipwa.
No comments :
Post a Comment