UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Taarifa ya Hali
ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa
Mwaka 2020/21. Pamoja na hotuba hii ninawasilisha vitabu vya Taarifa ya
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa
wa Mwaka 2020/21. Taarifa hizi ndiyo msingi wa bajeti ya Serikali kwa
mwaka 2020/21 nitakayowasilisha hapa Bungeni leo jioni.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote nichukue
fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia afya njema.
Aidha, naendelea kumshukuru kwa kulijalia Taifa letu amani, utulivu na
mshikamano na kutuwezesha kukutana katika mkutano huu wa 19 na wa mwisho
wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kujadili namna ya
kuharakisha maendeleo ya Taifa letu.
3. Mheshimiwa Spika,
naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoendelea
kuliongoza vema Taifa letu. Kwa kipindi hiki cha miaka minne na nusu ya
utawala wake tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi, mfumuko wa bei
umedhibitiwa, miradi mikubwa ya maendeleo inatekelezwa, uwajibikaji
katika utumishi wa umma umeimarika na kero za wananchi wanyonge
zinatatuliwa. Kipekee napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniamini
kuongoza Wizara ya Fedha na Mipango tangu mwanzo wa uongozi wake hadi
sasa.
4. Mheshimiwa Spika, vile
vile, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa
uongozi wao mahiri wameendelea kumshauri vema Mheshimiwa Rais katika
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.
5. Mheshimiwa Spika,Napenda
pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na
Mheshimiwa Dkt. Godwin Aloyce Mollel (Mb), kwa kuteuliwa na Mheshimiwa
Rais kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto.
6. Mheshimiwa Spika, napenda
pia nitumie nafasi hii kutoa salamu za pole kwako, Waheshimiwa Wabunge
na Wananchi wote kwa ujumla kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rashid Ajali
Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini (CCM), Mheshimiwa
Mchungaji Dkt. Getrude
Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mheshimiwa
Richard Mganga Ndassa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve (CCM), na
Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Mbunge wa kuteuliwa
(CCM) aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Mwenyezi Mungu azilaze roho
za marehemu mahali pema peponi. Amina!
7. Mheshimiwa Spika, nchi
yetu imepata mvua nyingi zilizo juu ya wastani hali iliyopelekea
kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali. Mafuriko haya
yamesababisha uharibifu mkubwa wa mazao ya wakulima, mali na miundombinu
hususan barabara, reli na madaraja. Mafuriko hayo yameathiri
utelekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za ukarabati wa
miundombinu iliyoharibika. Kwa msingi huo, katika mwaka 2020/21
kipaumbele ni kukarabati miundombinu iliyoharibika.
8. Mheshimiwa Spika, kama
unavyofahamu, nchi yetu na dunia kwa ujumla ilikabiliwa na mlipuko wa
ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaojulikana kama COVID - 19
inayosababishwa na virusi vya Corona. Ni dhahiri kuwa ugonjwa huu
umeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani kutokana na vifo, kuongezeka kwa
gharama za utoaji huduma katika sekta ya afya na kuathiri shughuli za
biashara na uzalishaji hususan kwa nchi zinazotegemea utalii.
9. Mheshimiwa Spika, jambo
jema ni kuwa nchi yetu haikuathirika sana na ugonjwa huu kutokana na
hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
uongozi imara wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama Taifa tuliendelea kumtegemea
Mwenyezi Mungu, kuchukua tahadhari za kiafya kama inavyoshauriwa na
wataalam pamoja na kufanya kazi kwa bidii. Aidha, Serikali imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huu ambapo hadi sasa
Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 15.49 kwa
ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kinga. Hatua nyingine ni pamoja na:
kutolewa msamaha wa kodi kwa aina 15 za vifaa vya kupambana na COVID –
19; kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na maambukizi; kutenga maeneo
maalum kwa ajili ya uangalizi kwa wasafiri wanaoingia nchini na
wanaobainika kuwa na dalili za ugonjwa huu; na kuanzishwa kwa huduma ya
namba maalum ya kupiga simu bila malipo kwa ajili ya msaada wa kiafya.
Vile vile, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua
mbalimbali za Sera ya Fedha ili kulinda na kuimarisha uchumi
zikijumuisha: kushusha kiwango cha chini cha kisheria cha sehemu ya
amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania kutoka asilimia 7 hadi
6; kushusha kiwango cha riba kinachotozwa kwa benki kukopa Benki Kuu
kutoka asilimia 7 hadi 5; kupunguza kiwango cha dhamana za Serikali
kutoka asilimia 10 hadi 5 kwa dhamana za muda mfupi na kutoka asilimia
40 hadi 20 kwa hati fungani; na kuzielekeza kampuni zinazotoa huduma za
fedha kwa njia ya mtandao kuongeza kiwango cha miamala kwa siku kwa
mteja kutoka shilingi milioni 3 hadi 5 na kiwango cha akiba kwa siku kwa
wateja kutoka shilingi milioni 5 hadi 10.
10. Mheshimiwa Spika, kutokana
na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali, hivi sasa hali
imeimarika ambapo shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kufanyika
kama awali. Serikali imeruhusu vyuo vikuu vimefunguliwa, wanafunzi wa
kidato cha sita wamerudi shuleni kujiandaa na mitihani, shughuli za
michezo yote zimeruhusiwa, anga
limefunguliwa ambapo ndege za mizigo na abiria zinaendelea kuingia
nchini na hivyo kupokelewa kwa watalii kutoka nchi mbalimbali. Hii ni
ishara dhahiri ya uongozi imara wa Mheshimiwa Rais kwa Taifa hususan
katika kipindi cha majanga na misukosuko mikubwa kwa dunia kama ugonjwa
huu.
11. Mheshimiwa Spika, Taarifa
ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Mwaka 2020/21 zimezingatia dhana ya ushirikishwaji mpana wa
wadau katika hatua za uandaaji na maamuzi katika ngazi zote Serikalini.
Nitambue mchango mkubwa wa Bunge
lako Tukufu chini ya uongozi wako Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Spika
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt.
Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, napenda kumshukuru Mheshimiwa
Mashimba Mashauri Ndaki (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Bajeti na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa ushauri makini
waliotupatia. Ushauri wao umezingatiwa kikamilifu katika uandaaji wa
taarifa nilizowasilisha mbele ya Bunge hili.
12. Mheshimiwa Spika, maandalizi
ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 yamezingatia
vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano vilivyoainishwa katika Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21, Ilani ya CCM ya
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na ahadi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizotoa wakati
akifungua rasmi Bunge la Kumi na Moja. Aidha, katika mwaka 2020/21
msukumo mkubwa utawekwa katika kukamilisha utekelezaji wa miradi
inayoendelea ili kupata matokeo tarajiwa.
MWENENDO WA HALI YA UCHUMI 2019
Uchumi wa Dunia
13. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Aprili 2020, uchumiwa dunia ulikua kwa asilimia 2.9 mwaka 2019. Aidha,
uchumi wa dunia unakadiriwa kuporomoka na kufikia ukuaji wa asilimia
hasi 3.0 mwaka 2020 ambao kwa kiasi kikubwa utachangiwa na athari za
mlipuko wa ugonjwa wa COVID - 19. Katika mwaka 2021 uchumi wa dunia
unatarajiwa kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 5.8 kutokana na
matarajio ya kutoweka kwa virusi vya Corona katika nusu ya pili ya mwaka
2020 na hatimaye, kuimarika kwa shughuli za kiuchumi duniani
ikijumuisha biashara na uzalishaji viwandani na utekelezaji wa sera za
kuongeza ukwasi katika nchi mbalimbali.
Uchumi wa Afrika na Kikanda
14. Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kasi ya ukuaji wa
uchumi ilifikia asilimia 3.1 mwaka 2019. Matarajio ya ukuaji wa uchumi
ni kupungua na kufikia wastani wa asilimia hasi 1.6 mwaka 2020 kutokana na athari za mlipuko wa ugonjwa wa COVID – 19. Aidha, ukuaji wa uchumi katika nchi za ukanda huo, unatarajiwa
kuimarika na kufikia wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2021. Ongezeko hilo
litatokana na jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID – 19, matarajio
ya kuongezeka kwa misaada kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya
kupambana na ugonjwa huo na matarajio ya utulivu wa bei ya nishati ya
mafuta katika soko la Dunia.
15. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2019, uchumi wa nchi za ukanda wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki uliendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa na ukuaji wa
asilimia 7.0, Rwanda asilimia 9.4, Uganda (asilimia 4.9) na Kenya
asilimia 5.4. Aidha, kutokana na athari za COVID-19, ukuaji wa uchumi wa
ukanda wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unatarajiwa kupungua
kidogo kwa mwaka 2020 na hatimaye kuanza kuimarika mwaka 2021 kutokana
na juhudi zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kupambana na athari
za COVID-19 zikiwemo hatua za kifedha na kibajeti pamoja na utekelezaji
wa miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta za uchukuzi (reli, barabara
na madaraja) maji, nishati, elimu na afya.
Uchumi wa Taifa
Pato la Taifa
16. Mheshimiwa Spika, mwaka
2019, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 kama ilivyokuwa mwaka
2018. Ukuaji huu ulitokana na uwekezaji hususan katika miundombinu
ikiwemo: ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege; kutengamaa kwa
upatikanaji wa nishati ya umeme; kuimarika kwa huduma za usafirishaji;
kuongezeka kwa uzalishaji wa madini hususan dhahabu na makaa ya mawe; na
kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo. Sekta zilizokua kwa
viwango vikubwa katika kipindi hicho ni pamoja na uchimbaji madini na
mawe (asilimia 17.7), ujenzi (asilimia 14.8), sanaa na burudani
(asilimia 11.2), na usafirishaji na uhifadhi mizigo (asilimia 8.7). Kwa mwaka
2020, ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kupungua kidogo kutoka maoteo
ya awali ya asilimia 6.9 hadi 5.5 kutokana na hatua madhubuti
zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania hususan kuhimiza wananchi waendelee kufanya kazi wakati
wanachukua tahadhari dhidi ya corona kama inavyoelekezwa na wataalam wa
afya pamoja na matarajio ya kuimarika kwa uchumi wa kikanda na dunia.
17. Mheshimiwa Spika, mwaka
2019, Pato la wastani la kila mtu lilikuwa shilingi 2,577,967
ikilinganishwa na shilingi 2,452,406 mwaka 2018, sawa na ongezeko la
asilimia 5.1. Vile vile, Pato la wastani kwa kila mtu katika dola za
Marekani liliongezeka hadi kufikia dola za Marekani 1,121 mwaka 2019
kutoka dola za Marekani 1,078 mwaka 2018.
Mwenendo wa Bei
18. Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, mwenendo wa mfumuko wa bei uliendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo ulifikia wastani wa asilimia 3.4 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.5 mwaka 2018. Mfumuko
wa bei za nishati umeendelea kupungua na kufikia asilimia 4.1 Aprili
2020 kutoka asilimia 13.3 Aprili 2019 kutokana na kupungua kwa bei za
nishati ya mafuta katika soko la dunia.
Utekelezaji wa Sera ya Fedha 2019/20
19. Mheshimiwa Spika, Serikali
kupitia Benki Kuu imeendelea kutekeleza sera ya fedha ya kuongeza
ukwasi kwenye uchumi ambayo imesaidia kupunguza viwango vya riba katika
masoko ya fedha hususan riba za mikopo na amana.
Wastani wa riba za mikopo ya benki kwa ujumla katika kipindi cha Julai
2019 hadi Aprili 2020 ulipungua hadi asilimia 16.85 ikilinganishwa na
wastani wa asilimia 17.16 katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19, na
riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja zimepungua na kufikia wastani
wa asilimia 16.24 kutoka asilimia 17.79. Vile vile, wastani wa riba za
amana kwa ujumla ulikuwa asilimia 7.02 katika kipindi cha Julai 2019
hadi Aprili 2020, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 7.62 katika
kipindi kama hicho mwaka 2018/19. Aidha, riba za amana za kipindi cha
mwaka mmoja ziliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 8.77 katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020 kutoka wastani wa asilimia 8.21
katika kipindi kama hicho mwaka 2018/19.
Ujazi wa Fedha na Karadha
20. Mheshimiwa Spika, Katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa ujazi wa
fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliongezeka kwa asilimia 9.9 na
kufikia shilingi trilioni 28.8 mwezi Aprili 2020 kutoka shilingi
trilioni 25.6 mwezi Aprili 2019. Ongezeko hili la ujazi wa fedha ni
matokeo ya utekelezaji thabiti wa sera ya fedha, ongezeko la mikopo kwa
sekta binafsi pamoja na rasilimali fedha za kigeni katika sekta ya
benki.
Mwenendo wa Mikopo kwa Sekta Binafsi
21. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, wastani wa ukuaji wa mikopo
kwa sekta binafsi ulikuwa asilimia 8.7 kufikia shilingi trilioni 19.7
ikilinganishwa na shilingi trilioni 18.6 Aprili 2019. Sehemu kubwa ya mikopo
ilielekezwa kwenye shughuli binafsi (asilimia 31.1) ikifuatiwa na
shughuli za biashara asilimia 17.6, uzalishaji viwandani asilimia 11.0
na kilimo asilimia 7.7.
Sekta ya Nje
22. Mheshimiwa Spika, hadi
Aprili 2020, urari wa jumla wa malipo ulikuwa na ziada ya dola za
Marekani milioni 897.1 ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani
bilioni 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Hii ilichangiwa na
kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho
wa mali nchi za nje kulikotokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje
ya nchi.
23. Mheshimiwa Spika, nakisi
kwenye urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje
ulipungua hadi kufikia dola za Marekani milioni 333.3 mwezi Aprili
2020, ikilinganishwa na nakisi ya dola za Marekani bilioni 1.6 katika
kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua huku kulitokana na kuongezeka
kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususa katika bidhaa asilia na zisizo
asilia kama vile dhahabu.
24. Mheshimiwa Spika, hadi
Aprili 2020, mauzo ya bidhaa na huduma nje yaliongezeka kufikia dola za
Marekani bilioni 8.6 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 7.3
Aprili 2019. Hii ilichangiwa na kuanzishwa kwa masoko ya madini nchini
kulikopelekea kuongezeka kwa mauzo ya dhahabu sanjari na ongezeko la bei
katika soko la dunia. Thamani ya uagizaji bidhaa na huduma kutoka nje
ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 8.6, ikilinganishwa na dola za
Marekani bilioni 8.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Sehemu kubwa
ilitumika katika uagizaji mafuta na bidhaa za mitaji ikiwemo mitambo na
mashine inayotumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu
ya reli, barabara, madaraja na uzalishaji umeme.
Akiba ya Fedha za Kigeni
25. Mheshimiwa Spika, hadi
Aprili 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni
5.3, kiasi kinachotosheleza kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka
nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.1. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo
la nchi la miezi 4.0, ambayo ni juu ya lengo la nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki la miezi isiyopungua 4.5 na Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika la miezi isiyopungua 6.0.
Mwenendo wa Thamani ya Shilingi
26. Mheshimiwa Spika, thamani
ya shilingi ya Tanzania dhidi ya sarafu nyingine kubwa duniani
imeendelea kuwa tulivu kwa kipindi chote cha mwaka 2019/20. Katika
kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020, dola moja ya Marekani
ilibadilishwa kwa wastani wa kati ya shilingi 2,299.3 na shilingi
2,302.7 katika soko la fedha la jumla ikilinganishwa na wastani wa kati
ya shilingi 2,276.4 na shilingi 2,300.9 kwa dola moja ya Marekani katika
kipindi kama hicho mwaka 2018/19.
Deni la Serikali
27. Mheshimiwa Spika, hadi Aprili 2020, deni
la Serikali lilifikia shilingi trilioni 55.43. Kati ya kiasi hicho,
deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 40.57 na deni la ndani shilingi
trilioni 14.85. Deni la Serikali lilichangiwa na kupokelewa kwa mikopo
mipya kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo
inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi. Matokeo ya tathmini ya uhimilivu
wa deni iliyofanyika Desemba 2019, imeonesha kuwa deni la Serikali ni
himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.
Utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi
28. MheshimiwaSpika, mwaka
2019/20, Serikali ilifanya utafiti wa Sekta Isiyo Rasmi mkoani Dar es
Salaam kwa lengo la kubaini mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa
kwa kutumia makadirio ya mapato na ongezeko la thamani ya uzalishaji wa
bidhaa na huduma kutoka shughuli za kilimo na zisizo za kilimo; tija
katika uwekezaji; kiwango cha ukuzaji mtaji; kutambua mahali biashara
zilipo; thamani ya uzalishaji kwa kila mtu; ajira na mgawanyo wake; na
mahusiano kati ya Sekta Isiyo Rasmi na sekta nyingine za kiuchumi.
29. MheshimiwaSpika, matokeo
ya utafiti huo yanaonesha kuwa: Mkoa wa Dar es Salaam una wamiliki wa
shughuli za Sekta Isiyo Rasmi wapatao 1,023,520 ambapo asilimia 47.6
wanajihusisha na biashara ya jumla na rejareja pamoja na matengenezo ya
magari na pikipiki; uwekezaji wa mitaji katika sekta isiyo rasmi ni shilingi bilioni 901.5 kwa mwaka 2019; jumla
ya ongezeko la thamani kwa mwaka katika bidhaa na huduma zinazozalishwa
katika sekta isiyo rasmi ni shilingi trilioni 6.2; na ajira
katika sekta isiyo rasmi kwa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi
imepungua kutoka watu 1,208,250 (asilimia 61.5) mwaka 2014 hadi
1,154,336 (asilimia 55.2) mwaka 2019. Hii inatokana na juhudi kubwa za
Serikali ya Awamu ya Tano katika kupanua wigo wa kujenga uchumi wa
viwanda ambao matokeo yake ni kukuza upatikanaji wa kazi zenye staha (decent work) na kuongezeka kwa ajira katika sekta rasmi.
30. Mheshimiwa Spika, maelezo
ya kina kuhusu hali ya uchumi yapo katika Aya ya 9 hadi 26 ya hotuba
yangu na kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019.
MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO KWA KIPINDI CHA 2016/17 – 2019/20
31. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha miaka minne na nusu ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano
(2016/17 – 2019/20), yamepatikana mafanikio mbalimbali katika
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo yakiwemo:
(i) Ukuaji wa Uchumi: uchumi
wa Taifa uliendelea kuimarika ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 6.9
na mfumuko wa bei kuendelea kupungua na kubaki katika wigo wa tarakimu
moja, chini ya wastani wa asilimia 5.0;
(iii) Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere – MW 2,115: Kazi zilizokamilika ni
pamoja na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya mradi (njia ya kusafirisha
umeme, barabara kwa kiwango cha changarawe, mfumo wa maji, mawasiliano
ya simu na nyumba za makandarasi); ujenzi wa daraja la muda namba 2;
utafiti wa miamba na udongo; na uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini (adit tunnel)
wenye urefu wa mita 147.6 na mtambo wa kuchakata kokoto namba moja
ambapo utekelezaji wa mradi wote umefikia asilimia 10.74. Aidha, jumla
ya shilingi trilioni 1.42 zimetumika kugharamia mradi na ajira zipatazo
3,897 zimezalishwa;
(iv) Nishati:
kukamilika kwa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220
kutoka Makambako – Songea ambapo shilingi bilioni 160.1 zimetumika;
kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka
Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 67 na
shilingi bilioni 219.4 zimetumika; kuendelea na utekelezaji wa miradi ya
usambazaji umeme vijijini kupitia REA ambapo shilingi trilioni 2.27
zimetumika jumla ya vijiji 9,112 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara
vimeunganishwa umeme, sawa na asilimia 74.3. Hadi Mei 2020, kiwango cha
upatikanaji wa umeme (overall electricity access rate) kimefikia asilimia 84.6 kutoka asilimia 67.8 mwaka 2016;
(v) Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania: Serikali
imeendelea kuboresha Shirika la Ndege kwa kununua ndege mpya 11. Kati
ya hizo, ndege nane (8) zenye thamani ya shilingi trilioni 1.27
zimepokelewa na malipo ya awali ya shilingi bilioni 85.7 kwa ajili ya
ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu (3) yamefanyika ambapo ndege mbili
(2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni aina ya De Havilland Dash
8-400;
(vi) Viwanja vya Ndege: kukamilika
kwa ujenzi na ukarabati wa viwanja vya Ndege vya Mwanza awamu ya
kwanza, Nachingwea na Kilimanjaro (KIA); kuendelea na ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya Geita (asilimia 78) na Songea (asilimia 34).
Aidha, ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere umekamilika na kuanza kutumika ambapo kiasi
cha Euro milioni 276 sawa na takribani shilingi bilioni 722.1
zilitumika;
(vii) Bandari: kukamilika
kwa ujenzi wa Gati Na.1, 2, 3, 4 na Gati la kupakia na kupakua magari
(Ro-Ro) katika bandari ya Dar es Salaam; ujenzi wa gati lenye urefu wa
mita 300 katika bandari ya Mtwara umefikia asilimia 61; na kukamilika
kwa uongezaji wa kina cha bandari ya Tanga na ujenzi wa Gati namba 2
umefikia asilimia 60. Aidha, kwa upande wa Bandari za Maziwa Makuu: katikaZiwa Victoria - ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama,
Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi Mwigobero umekamilika;
kununuliwa kwa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; na ukarabati wa
majengo na ofisi za bandari. Ziwa Tanganyika - uboreshaji wa Gati
la Kagunga umekamilika; ujenzi wa Gati la Sibwesa umefikia asilimia 98;
ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Kabwe umefikia asilimia 56; na ujenzi wa miundombinu na Gati la Bandari ya Lagosa umefikia asilimia 53. Ziwa Nyasa - ujenzi wa sakafu ngumu kwa ajili ya maegesho katika bandari ya Kiwira; na ujenzi wa Gati la Ndumbi umekamilika;
(viii) Ujenzi na Ukarabati wa Meli katika Maziwa Makuu: kukamilika
kwa ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo
tani 200 katika Ziwa Nyasa, ukarabati wa meli ya MV Victoria katika
ziwa Victoria na meli ya mafuta ya MT. Sangara katika Ziwa Tanganyika;
kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi wa Chelezo na MV Butiama asilimia
98; na kuendelea na ujenzi wa meli mpya (MV Mwanza) yenye uwezo wa
kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo
utekelezaji umefikia asilimia 60;
(ix) Barabara na Madaraja: ujenzi wa Barabara:kukamilika
kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa jumla ya
kilometa 2,624.27 na kuendelea na ujenzi wa barabara kuu kwa kiwango cha
lami zenye urefu wa kilometa 1,298.44; barabara ya njia nane kutoka
Kimara hadi Kibaha (km 19.2) umefikia asilimia 80; na ujenzi wa Ubungo Interchange umefikia asilimia 77. Madaraja:
kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Mfugale (Dar es Salaam), Magufuli
katika mto Kilombero (Morogoro), Momba (Rukwa), Sibiti (Singida), Mara
(Mara), Lukuledi (Lindi), Mangara (Manyara) na Kavuu (Katavi); kuendelea
na ujenzi wa madaraja ya Kitengule (Kagera) asilimia 50, Ruhuhu
(Ruvuma) asilimia 86, Msingi (Singida) asilimia 40, New Wami
(Pwani) lenye urefu wa mita 513.5 na barabara unganishi zenye kilomita
4.3 umefikia asilimia 39 na daraja jipya la Selander lenye urefu wa
kilomita 1.03 na barabara unganishi zenye kilomita 5.2 umefikia asilimia
38.2; na kuanza kwa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye
urefu wa kilomita 3.2 ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 61.4 yamefanyika.
(x) Kilimo, Mifugo na Uvuvi: katika Kilimo,miche
bora ya korosho 12,252,197 imezalishwa na mbolea tani 519,813
imesambazwa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara; na kuongezeka kwa
upatikanaji wa mbegu bora za mahindi, ngano, maharage, mpunga, soya,
alizeti, mtama, ufuta, viazi mviringo na mazao ya bustani kufikia tani
49,040.66. Aidha, kupitia Mradi wa Kuongeza Uzalishaji wa Mpunga (ERPP),
shughuli zifuatazo zimetekelezwa: ukarabati wa miundombinu ya
umwagiliaji katika skimu za Kigugu -
Mvomero (hekta 200) asilimia 50, Mvumi - Kilosa (hekta 249) asilimia
84, Kilangali – Kilosa (hekta 600) asilimia 51, Msolwa Ujamaa -
Kilombero (hekta 675) asilimia 40 na Njage - Kilombero (hekta 325)
asilimia 84. Mifugo:
kuendelezwa kwa mashamba matano (5) ya kuzalisha mitamba; kuzalishwa na
kusambazwa kwa mitamba 15,097 ya ng’ombe wa maziwa; kununuliwa na
kusambazwa kwa lita 8,823.53 za dawa aina ya Paranex ya kuogesha mifugo; kukarabatiwa kwa majosho 1,129; na kutolewa kwa chanjo ya ndigana kali (east coast fever) kwa ng’ombe 70,260. Uvuvi: uzalishaji wa vifaranga 15,041,401 vya samaki; na kuongezeka kwa uvunaji wa samaki (maji ya asili) kufikia tani 470,309.23;
(xi) Miradi ya Afya: ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya
kutolea huduma za afya ya msingi nchini ikijumuisha vituo vya afya 487,
hospitali za wilaya 71, hospitali za rufaa za mikoa 10 na zahanati
1,198; kuongezeka kwa bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 269 mwaka
2019/20; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za
Njombe, Simiyu, Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza),
Burigi - Geita, Mwananyamala – Dar es Salaam na hospitali za rufaa za
kanda ya kusini Mtwara, kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya, hospitali
ya Kibong’oto na ujenzi wa Kituo Maalum cha kutenga wagonjwa wa magonjwa
yanayoambukiza (Isolation Centre)
katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Temeke, na Maabara ya Taifa
Mabibo; na ununuzi wa dawa, chanjo, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi
ikijumuisha vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete.
(xii) Miradi ya Elimu: kukamilika
na kuanza kutumika kwa Maktaba ya Kimataifa yenye uwezo wa kuhudumia
wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
kuendelea na ujenzi wa maabara ya masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (Kampasi ya Solomon Mahlangu), ujenzi wa hosteli
za Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
hosteli za wanafunzi na Maktaba katika Chuo Kikuu Mzumbe (kampasi ya
Mbeya); utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi
bilioni 365 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 450 mwaka 2019/20;
uimarishaji wa vyuo vya VETA na kukuza ujuzi kwa vijana nchini; na
ukamilishaji wa maboma 364 ya nyumba za walimu wa shule za msingi kwenye
maeneo yenye mazingira magumu na kuendelea kugharamia elimumsingi bila
ada ambapo shilingi trilioni 1.03 zimetumika kuanzia mwaka 2015 hadi Mei
2020.
(xiii) Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: Serikali
imeendelea kuboresha huduma za maji safi na salama vijijini na mijini
ambapo miradi 1,423 (vijijini 1,268 na mijini 155) imetekelezwa na
kukamilika kati ya mwaka 2015 na 2019. Miradi hiyo inajumuisha: mradi wa
kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa,
Tabora, Igunga, Uyui na Nzega ambapo ujenzi wa matanki 17 na ulazaji wa
mabomba makubwa ya kusafirisha maji kutoka kijiji cha Solwa – Nzega –
Tabora – Igunga (km 290.7) umekamilika. Utekelezaji wa miradi ya maji
umewezesha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 70.1
vijijini na asilimia 84 mijini;
(xiv) Madini: Mafanikio
yaliyopatikana ni pamoja na marekebisho ya sheria na mikataba ya
uwekezaji katika sekta ya madini na hivyo kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya
Twiga Minerals Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya
Serikali (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84); na
kufanyika kwa malipo ya fidia ya dola za Marekani milioni 100 kutoka
Kampuni ya Barrick ikiwa ni sehemu ya kwanza ya kiasi cha makubaliano
ya awali ya kulipa fidia ya dola za Marekani milioni 300. Aidha,
marekebisho ya Sheria yamewezesha kuanza kwa majadiliano baina ya
Serikali na Makampuni yote makubwa ya madini kwa lengo la kupata
asilimia 16 ya hisa kwa Serikali. Mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa
masoko 28 na vituo 25 vya ununuzi wa madini nchini; kukamilika kwa
ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bukoba, Handeni,
Bariadi na Musoma; kukamilika kwa ujenzi wa viwanda viwili (2) vya mfano
vya kuchenjua dhahabu vya Lwamgasa na Katente; kukamilika kwa ujenzi wa
one stop center Mirerani, kuimarika kwa udhibiti wa madini ikijumuisha ujenzi wa ukuta wa Mirerani uliowezesha kupungua kwa utoroshaji madini;
na kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali kutoka shilingi bilioni 196
mwaka 2015/16 hadi zaidi ya shilingi bilioni 470 mwaka 2019/20; na
(xv) Uendelezaji wa Viwanda: kufanikisha
ujenzi wa viwanda vipya 8,477 ambapo viwanda vikubwa ni 201, vya kati
460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Mafanikio mengine ni pamoja na
upanuzi wa Kiwanda cha Ngozi na Bidhaa za Ngozi cha Karanga (Moshi) na
kuimarisha Shirika la Nyumbu (Pwani).
32. Mheshimiwa Spika, maelezo
ya kina kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa Mpango yapo katika Aya ya 32
na 33 ya hotuba yangu na Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo
kwa Kipindi cha Mwaka 2016/17 hadi 2019/20.
MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21
Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa Mwaka 2020/21
33. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 umezingatia shabaha kuu za uchumi jumla zifuatazo:
(a) Ukuaji
wa Pato Halisi la Taifa unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya
asilimia 6.9 na kufikia asilimia 5.5 mwaka 2020 ikilinganishwa na
asilimia 7.0 mwaka 2019. Hii ni kutokana na athari za ugonjwa wa COVID-19 ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa kibiashara;
(b) Kuendelea
kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki katika
wigo wa tarakimu moja kati ya wastani wa asilimia 3 hadi 5 kwa mwaka
2020/21;
(c) Mapato ya ndani kufikia asilimia 14.7 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 14.0 mwaka 2019/20;
(d) Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.1 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21;
(e) Nakisi
ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa asilimia 2.6 mwaka 2020/21 ikiwa
ni chini ya asilimia 3.0 kuendana na makubaliano ya nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(f) Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi
4.0.
Miradi ya Kipaumbele 2020/21
34. Mheshimiwa Spika, mwaka
huu nchi yetu imepata mvua nyingi zilizosababisha uharibifu mkubwa wa
miundombinu. Katika mwaka 2020/21, Serikali itaweka kipaumbele katika
ukarabati wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii iliyoharibiwa na mvua
ikijumuisha barababara na madaraja, reli, nguzo za umeme, mabwawa ya
maji na majengo ya taasisi za afya na elimu;
35. Mheshimiwa Spika, miradi na shughuli za kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo:
(a) Viwanda vya Kukuza Uchumi na Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: Katika
eneo hili mkazo utawekwa kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia
malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini. Miradi mahsusi katika eneo
hili ni pamoja na:
(i) Uendelezaji wa Viwanda ikijumuisha
kuendeleza vituo vya utafiti wa teknolojia na bidhaa za viwandani vya
CAMARTEC, TIRDO, TEMDO na SIDO; kuboresha Shirika la Nyumbu; na
uendelezaji wa maeneo maalumu ya uwekezaji ya Bunda, Manyoni, Tanga,
Mtwara, Dodoma, Bagamoyo na Benjamin William Mkapa;
(ii) Kilimo: kuboresha
utafiti na miundombinu ya utafiti katika kilimo; kuongeza tija katika
uzalishaji kwa kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora na pembejeo, huduma
za ugani, maghala na masoko kwa mazao ya kimkakati ya michikichi,
kahawa, pamba, chai, tumbaku na miwa; kujenga na kukarabati miundombinu
ya skimu za umwagiliaji; na kuboresha huduma za ushauri kuhusu utafiti,
mafunzo na usambazaji wa taarifa za kilimo;
(iii) Mifugo: kuimarisha tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo; ujenzi
wa majosho; kuboresha miundombinu ya uhifadhi wa chanjo; kuimarisha
vituo vya uhimilishaji Kitaifa na Kikanda; na kuboresha mazingira ya
biashara ya mifugo;
(iv) Uvuvi: kujenga
na kukarabati miundombinu ya ufugaji wa viumbe maji; kuboresha Shirika
la Uvuvi Tanzania (TAFICO); kujenga na kukarabati miundombinu ya mialo
na masoko ya uvuvi; na ujenzi wa bandari ya uvuvi; na
(v) Madini: kujenga ofisi nane (8) za maafisa madini na kituo cha umahiri; kujenga ghala la kuhifadhi sampuli za miamba choronge (core shed); kununua vitendea kazi kwa ajili ya shughuli za utafiti wa ikolojia; na kununua vifaa vya maabara na utafiti;
(b) Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi ya kipaumbele itakayotekelezwa katika mwaka 2020/21 itajielekeza katika maeneo yafuatayo:
(i) Elimu: kuendelea
kusomesha kwa wingi wataalamu kwenye fani na ujuzi adimu kama vile
udaktari, mafuta na gesi, Jiolojia, Jemolojia na Uhandisi migodi;
kuendelea kugharamia utoaji wa elimumsingi bila ada; ujenzi na ukarabati
wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika shule na vyuo vya
ualimu na vya Elimu ya Juu; ujenzi wa nyumba 122 za walimu katika shule
10 za msingi na shule 20 za sekondari katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi; na kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu;
(ii) Afya: kuendelea na ujenzi wa hospitali 71 za wilaya; kuboresha
miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za
mikoa, kanda na Taifa; kuimarisha usambazaji wa dawa, chanjo, vifaa,
vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya;
kuimarisha huduma katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Tiba
ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI); kujenga
na kukarabati vyuo vya Maendeleo ya Jamii; kuboresha uhai na Maendeleo
ya Awali ya Mtoto; na kuboresha huduma za Ustawi wa Jamii;
(iii) Maji: kuendelea
na ukamilishaji na upanuzi wa miradi ya maji katika miji mikuu ya Mikoa
na Wilaya ikijumuisha Mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Njombe, Katavi na
Songwe; kuendelea na ujenzi wa miradi ya maji ya Masasi – Nachingwea,
Same – Mwanga – Korogwe, ziwa Victoria – Igunga, Nzega na Tabora, ziwa
Victoria – Kahama – Shinyanga; na kusimamia na kuendeleza rasilimali za
maji nchini.
(c) Uboreshaji wa Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara na Uwekezaji: Miradi
itakayotekelezwa katika eneo hili italenga kuendeleza ujenzi na
ukarabati wa miundombinu wezeshi ili kurahisisha uendeshaji biashara na
uwekezaji nchini. Miradi hiyo ni pamoja na: kuendelea na ujenzi wa Reli
ya Kati ya standard gauge;
mradi wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115; na
kuboresha Shirika la Ndege Tanzania. Miradi mingine inajumuisha:
(i) Barabara na Madaraja: kuendelea na ujenzi wa barabara ya Tabora - Ipole - Koga - Mpanda (km 370); Barabara ya Mbeya - Makongolosi - Rungwa – Itigi - Mkiwa (km 577.9);
Kigoma - Kidahwe - Uvinza – Kaliua - Tabora (km 389.7); Kabingo –
Kasulu – Manyovu (km 260); Mtwara – Mingoyo – Masasi – Songea – Mbamba
Bay (km 1,470.9); Bagamoyo – Makurunge – Saadani - Tanga (km 246); Sumbawanga - Mpanda – Nyakanazi (km 517.4); Usagara – Geita – Buzirayombo – Kyamyorwa (km 388); ujenzi wa barabara za mzunguko Dodoma (km 112.3); na upanuzi wa Barabara ya njia nane (8) Kimara – Kibaha (km 25.7);
kuendelea na ujenzi wa madaraja ya Kigongo – Busisi (Mwanza), daraja
jipya la Selander, Mangara (Manyara), New Wami (Pwani) na Kitengule
(Kagera);
(ii) Reli: kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha kimataifa cha standard gauge, kuendelea na ukarabati wa vichwa vya treni, mabehewa ya mizigo na abiria pamoja na njia za reli ya kati na TAZARA;
(iii) Nishati: kuendelea na ujenzi wa bwawa la kuzalisha Umeme katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere Rufiji – MW 2,115,
kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 -
North – West Phase I, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa
kV 400 kutoka Singida - Arusha – Namanga, Mradi wa Kusafirisha Umeme wa
Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Kinyerezi, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 kutoka Chalinze - Dodoma, Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Rusumo – Nyakanazi na kuendelea na usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA; na
(iv) Bandari: kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na bandari za maziwa makuu; na
(v) Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Viwanja vya Ndege: kuendelea
kuboresha Shirika la Ndege Tanzania, uendelezaji wa viwanja vya ndege
ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja kipya cha Ndege cha Kimataifa cha
Msalato – Dodoma.
(d) Kuimarisha Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango: Miradi
itakayotekelezwa inalenga kuimarisha mifumo na taasisi za utekelezaji
na usimamizi wa Mpango, kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za
kutekeleza mpango na kuweka vigezo vya upimaji
wa matokeo ya utekelezaji. Miradi hii itajumuisha maeneo ya Utawala
Bora hususan utoaji haki na huduma za kisheria, kuimarisha miundombinu
ya Mahakama na Bunge na kuimarisha vyombo vya ulinzi na usalama.
36. Mheshimiwa Spika, Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 utaendelea kuzingatia umuhimu wa
kuimarisha Muungano wetu. Miradi itakayotekelezwa kwa pamoja Tanzania
bara na Zanzibar ni pamoja na:
(i) Mradi wa Kikanda wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) kwa lengo la kuimarisha uvuvi wa bahari kuu;
(ii) programu ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kulinda mazingira ya fukwe katika ukanda wa bahari kuu;
(iii) Mpango
wa Kunusuru Kaya Masikini katika Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF III) ambapo shughuli zilizopangwa ni kuendelea kuongeza
maeneo ya utekelezaji kutoka 161 ya sasa hadi maeneo 187 katika
Halmashauri zote Tanzania Bara na Wilaya zote Zanzibar ambapo shughuli
za miradi 2,505 ya kutoa ajira za muda na kuendeleza miundombinu
zitatekelezwa Tanzania Bara na miradi 204 zitatekelezwa Zanzibar; na
(iv) Mradi
wa Kupitia Mifumo ya Ikolojia kwa lengo la kuongeza uvumilivu wa
kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha
mifumo ikolojia katika Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro
(Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) na Kaskazini A,
(Kaskazini Unguja). Shehia
zitakazonufaika na mradi kutoka Kaskazini A ni pamoja na Shehia ya
Matemwe Kijini, Matemwe Jugakuu na Matemwe Mbuyutende.
37. Mheshimiwa Spika, maelezo
ya kina kuhusu vipaumbele vya Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya
ya 35 na 36 ya hotuba yangu na Sura ya Nne ya Kitabu cha Mpango.
Ugharamiaji wa Mpango 2020/21
38. Mheshimiwa Spika,
Serikali imetenga shilingi trilioni 12.90, kwa ajili ya kugharamia
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, sawa na
asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2020/21. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 10.16 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.74 ni fedha za nje. Kiwango kilichotengwa kinaendana na lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano la kutenga kati ya asilimia 30 na 40 ya bajeti yote kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
39. Mheshimiwa Spika, maelezo
ya kina kuhusu ugharamiaji wa Mpango kwa Mwaka 2020/21 yapo katika Aya
ya 40 na 41 ya hotuba yangu na Sura ya Tano ya Kitabu cha Mpango.
Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa za Utekelezaji
40. Mheshimiwa Spika,
moja ya nyenzo muhimu ya kufikia malengo ya mipango ni kuwa na mfumo
madhubuti wa kufuatilia utekelezaji na matumizi ya fedha zilizopangwa.
Kwa kutambua hilo, Serikali imejipanga kufanya ufuatiliaji wa karibu wa
matumizi sahihi ya fedha za miradi na kukagua maendeleo ya shughuli zote
za utekelezaji wa miradi kwa lengo la kujiridhisha iwapo utekelezaji
unaendana na matarajio na kuhakikisha matokeo yaliyokusudiwa yanafikiwa
kwa manufaa ya Taifa. Katika kuboresha utekelezaji wa miradi ya
maendeleo, Serikali itaandaa Mwongozo wa Kisera wa kusimamia shughuli za
ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
41. Mheshimiwa Spika, katika
kufanikisha Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango, Serikali inazielekeza
Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali kuimarisha
mifumo ya ndani ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo;
kutafsiri malengo na viashiria vya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 - 2020/21 katika Mipango na Bajeti za
kisekta kwa mwaka 2020/21; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya
maendeleo kila robo mwaka; kuwajengea uwezo watumishi katika tasnia ya
ufuatiliaji na tathmini; na kuandaa taarifa za ufuatiliaji na tathmini
ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na programu, na
kuziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI itaratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo
inayotekelezwa katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za
Serikali za Mitaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji Wizara ya Fedha
na Mipango.
MAJUMUISHO
42. Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa Mpango huu utakuwa ni wa mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Pili
wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wenye dhima ya kujenga uchumi wa
viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.
Mafanikio yanayotarajiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango ni pamoja na: kuongeza
kasi ya ukuaji wa uchumi na utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla;
kuimarisha utoaji wa huduma za jamii zikijumuisha maji, elimu, afya na
umeme vijijini; kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji; na
kuongezeka kwa ajira na kipato cha wananchi na hatimaye kupungua kwa
kiwango cha umaskini nchini.
HITIMISHO
43. Mheshimiwa Spika, kwa
niaba ya Serikali napenda kuwashukuru wadau mbalimbali wakiwemo
Waheshimiwa Wabunge, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo na Wananchi
kwa ujumla kwa michango yao katika utekelezaji wa Mpango na kujenga
uchumi. Michango hiyo imewezesha kupatikana kwa mafanikio mkubwa katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
44. Mheshimiwa Spika, naomba
nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu
Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara Zinazojitegemea na Wakala, Taasisi
na Mashirika ya Umma kwa ushirikiano wao katika
kutayarisha taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2019 na Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21. Kipekee ninamshukuru Mheshimiwa
Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mipango kwa kunisaidia kuboresha hotuba hii. Aidha, ninawashukuru watendaji
wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto
M. James kwa kusimamia kikamilifu maandalizi ya hotuba hii.
45. Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii
na vitabu vya Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 vinapatikana katika tovuti
ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni www.mof.go.tz.
46. Mheshimiwa Spika, baada
ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2019 na Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Mwaka 2020/21.
47. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527
Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
Umezisoma hizi?
- FULL POWER, ZATI 50 NI KIBOKO YA TATIZO LA UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME NA UUME MDOGO
- SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA TAIFA WAUENDESHAJI WA SHUGHULI ZA UTALII NCHINI TANZANIA WAKATI HUU WA JANGA LA CORONA
- RAIS MAGUFULI AMSAMEHE ALIYEKUWA KAMISHNA MKUU WA JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI, THOBIAS ANDENGENYE
- ASKARI POLISI WA FFU AFARIKI DUNIA KWA KUGONGWA GARI SHINYANGA...UZEMBE WATAJWA
- AJALI YA LORI,TREKTA, HIACE YAUA WATU 8,KUJERUHI WATANO IHAYABUYAGA MWANZA
- WAFANYABIASHARA DAR WAELIMISHWA KUHUSU KODI YA ZUIO