Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Anthony
Mavunde,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa
taarifa kwa juu ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na
kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevye nchini,Kushoto kwake ni Kamishna
wa kinga na tiba Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya
Dk.Peter Mfisi.
Kamishna wa kinga na tiba Mamlaka
ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi,akisisitiza
jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma wakati
akitoa maelezo juu ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na
kudhibiti utumiaji wa dawa za kulevye nchini
……………………………………………………………………………….
Na. Alex Sonna, Dodoma
Naibu Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde
amesema kuwa Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na
Dawa za
Kulevya imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa
za kulevya hapa nchini kwa mwaka 2019.
Kauli hiyo
ameitoa leo jijini Dodoma wakati akziungumza na waandishi wa habari juu
ya mwenendo wa mafanikio makubwa ya kupambana na kudhibiti utumiaji wa
dawa za kulevye nchini.
Kwa mujibu wa
Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Duniani ya mwaka 2019 (Word Drug
Report 2019), takribani watu milioni 271 ambao ni asilimia 5.5 ya watu
wenye umri wa miaka 15 hadi 64 walitumia dawa za kulevya mwaka 2017.
Aidha Mhe.Mavunde
amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wa nje na ndani ya nchi
operesheni mbalimbali ndani ya nchi ikiwemo mipakani na katika ukanda
wa Pwani na Bahari ya Hindi na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza
uingizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Mhe. Mavunde
ameeleza kuwa kwa mwaka 2019, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa
za Kulevya ilikamata jumla ya kilogramu 55.35 za heroin, kilo 10.34 za
cocaine, tani 21.16 za bangi na tani 9.07 za mirungi ikiwahusisha
watuhumiwa wapatao 10,384 ambao kesi zao ziko katika hatua mbalimbali
mahakamani.
“Dawa za kulevya
zinazokamatwa huteketezwa kwa mujibu wa sheria kwa kushirikisha Mamlaka
mbalimbali za Serikali baada ya hukumu kutolewa, Mwaka 2019 tuliteketeza
kilo 122.55 za heroin na kilo 71.507 za cocaine katika viwanda vya
saruji Dar es Salaam na Mbeya” amebainisha Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde
ameongeza kuwa katika kukabiliana na madhara yatokanayo na matumizi ya
dawa za kulevyaSerikali imeendelea kuimarisha huduma za tiba kwa waraibu
wa dawa za kulevya ambao hadi mwezi Desemba mwaka 2019 serikali
imeanzisha vituo sita vya kutolea matibabu kwa waratibu wa dawa za
kulevya kwa kutumia Methadone.
Vituo hivyo vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, na Dodoma vilikuwa vimesajiri waraibu wapatao 7,600.
Aidha Mhe.
Mavunde amesema kuwa waathirika wa dawa za kulevya katika nyumba za
upataji nafuu (Sober houses) ambapo waraibu wapatao 3,600 waliweza
kuhudumiwa, hivyo kufanya idadi ya waraibu waliohudumiwa mwaka 2019
kufikia zaidi ya 11,100.
Pia Mhe. Mavunde
ameainisha kuwa matumizi ya dawa za kulevya kwa wajawazito husababisha
athari kwa watoto wao na wanapojifungua na huathiri familia zao kwa
kiwango kikubwa zaidi kwa kushindwa kuwapa malezi bora watoto wao.
“Hali hii
inatengeneza vizazi vya waraibu wa dawa za kulevya hivyo wanawake
walioathirika na dawa za kulevya kujitokeza ili wapatiwe matibabu katika
vituo vilivyoanzishwa na Serikali” amesema Mhe. Mavunde.
Mhe. Mavunde
ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitokeza pale ambapo kuna utoaji wa
Elimu juu ya dawa za kulevya inapotolewa katika maeneo yao kwa kupitia
njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, matukio ya kitaifa, semina,
makongamano na mitandao ya kijamii. Utoaji wa elimu ni mkakati muhimu wa
kupunguza matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa makundi tofauti ya
rika.
Kwa upande wa Kamishna wa kinga na
tiba Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter
Mfisi,amesema kuwa wanawake wanaotumia vilevi wanavitumia kwa haraka
zaidi kuliko wanaume na kuweza hupata uraibu wa madhara mengine kuliko
wanaume.
Hata hivyo Dk.Mfisi amesema kuwa
ipo sheria ambayo inampa mamlaka Kamishna anaweza kuruhusu kilimo cha
bangi au koki kwa ajili ya matumzi ya kisayansi kama tafiti au matumizi
ya kutengenezea dawa.
”Zipo njia ambazo lazima zifuatwe
ili mtu aweze kupatiwa kibali kutoka wizara ya kilimo na wizara ya mambo
ya ndani ya nchi na ijiridhishe kuwa mtu au mwananchi akilima zao la
bangi atatumia kwa ajili ya kutengenezea dawa na si kitu
chochote”amesisitiza Dk.Mfisi
No comments :
Post a Comment