Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama ktk meza kuu) akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho leo na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro kwenye kikao cha menejimenti ya chuo.
Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akioneshwa mchoro wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia na meneja mradi Abdalla Khama.
Meneja mradi wa jengo jipya Abdalla Khama akimuelezea jambo Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro wakati alipotembelea eneo la mradi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akiongea na wanafunzi (hawapo pichani)
Sehemu ya wanafunzi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani).
******************************
Serikali imekiagiza Chuo cha
Diplomasia kujikita kuongeza tafiti pamoja na
machapisho mbalimbali kwa
lengo la kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kutoa mchango wao katika
Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya
Uchumi.
Maagizo hayo yametolewa leo jijini
Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho na
kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.
Dkt. Ndumbaro amesema ili chuo cha
diplomasia kiendelee kuheshimika zaidi duniani lazima kihakikishe kuwa
kinazalisha tafiti na machapisho ya kutosha.
“Utafiti na machapisho siyo suala
la wahadhiri peke yao…..siyo suala la wanafunzi peke yao ni suala la
wanachuo…… mawazo yenu lazima yafanyiwe utafiti kwa kushirikiana na
wahadiri wenu na ni lazima tuwe na machapisho zaidi,” Amesema DKt.
Ndumbaro
Naibu Waziri ameongeza kuwa moja
kati ya changamoto inayoikumba diplomasia hivi sasa ni mabadiliko ya
mifumo mbalimbali duniani ambapo wanadiplomasia wanapaswa kujua kuwa
dunia ipo katika mlengo upi, hivyo vyema mkajikita katika tafiti zenu
ili kuweza kusaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa
kimataifa yanayotokea duniani.
“Lakini pia niliagiza muongeze
lugha zaidi kwa sababu pia diplomasia pia ni mawasiliano na unawasiliana
na watu wa lugha tofauti tofauti, kwa hiyo tuongeze lugha mbalimbali
ili diplomasia iweze kufanya kazi yake,” Amesema DKt. Ndumbaro.
Aida, Naibu Waziri ameagiza pia
chuo hicho kuanzisha semina za kila mwezi ambapo zitajumuisha Wahadiri
na wanafunzi pamoja na mabalozi wastaafu kwa lengo la kujadili mambo
yanayohusu diplomasia na kuwapa uzoefu wa masuala ya kidiplomasia.
Wanafunzi kwa upande wao wamepata
fursa ya kumuelezea Naibu Waziri changamoto mbalimbali zinazo wakabili
zikiwemo za kupata asilimia ndogo za mkopo wa elimu ya juu, ukosefu wa
mafunzo kwa vitendo, ukosefu wa mabweni pamoja na mazingira ambayo siyo
wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Mkopo tunaopewa ni mdogo sana na
hautoshi hivyo tunaomba serikali itusaidie kutuongezea fedha za mkopo
ili tuweze kukidhi mahitaji yetu wakati tunapokuwa chuoni,”Amesema Isack
Sadock
Pia, Dkt. Ndumbaro baada ya
kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo, ameuagiza
uongozi wa chuo kuandaa na kuratibu mafunzo kwa vitendo badala ya
kufuatiliwa na wanafunzi, kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wenye
ulemavu/maitaji maalumu ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha
Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera amemhakikishia Naibu Waziri kuwa chuo
kitayafanyia kazi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
“Mhe. Naibu Waziri naomba
nikuhakikishie kuwa maagizo yako tumeyapokea……….mimi kwa kushirikiana na
menejimenti, wahadhiri na wafanyakazi tayafanyia kazi kwa wakati,”
Amesema Dkt. Ponera
Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia.
Katika hatua nyingine, ametoa
msimamo wa Serikali kuhusu changamoto zinazojitokeza mipakani hasa
katika mpaka wa Tanzania na Kenya na kusema kuwa Serikali ipo kwenye
mazungumzo na Kenya ili kuweza kubaini tatizo ni kitu gani.
“Kwa sasa tupo kwenye majadiliano
na wenzetu wa Kenya na kuona tatizo ni kitu gani je ni corona tu au ni
zaidi ya corona? Msimamo wa serikali yetu ni kuwa kila nchi ipime watu
wake…..na tunaamini huo ndiyo msimamo sahihi wa diplomasia ya uchumi,”
Amesema Dkt. Ndumbaro.
Chuo cha Diplomasia kilianzishwa
rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wa wakati huo, Mhe. Benjamini William
Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.
No comments :
Post a Comment