Maafisa usajili wa Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa nchini (NIDA) wakiendelea kutoa huduma za usajili
kwa wananchi katika ofisi za Wilaya za Mamlaka hiyo katika Wilaya za
Mkoa wa Dar es salaam huku tahadhari za maambukizi ya virusi vya Corona
ikiendelea kuzingatiwa kikamilifu.
……………………………………………………………………………
Na: Agnes Gerlad
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa
(NIDA) inaendelea na shughuli za Usajili na Utambuzi wa
Watu nchini kote
ambapo wananchi wanaendelea kupatiwa huduma katika ofisi za Usajili za
NIDA zilizoko katika kila wilaya nchini.
Kwa mujibu wa Msemaji wa NIDA,
Bw. Geofrey Tengeneza amesema, NIDA kwa kushirikiana na Idara ya
Uhamiaji, Uongozi wa Wilaya/Mkoa, Serikali za Mitaa na Wadau wengine
inaendelea kutoa huduma zote zinazohusiana na Usajili na Utambuzi wa
watu kama ilivyokuwa awali.
Ameongeza kusema kwamba,
Usajili wa awali kwa maana ya Mwombaji kujaza fomu ya Maombi ya
Utambulisho wa Taifa, kuchukuliwa alama za Kibaiolojia inayohusisha
mwombaji kupigwa picha, kuchukuliwa alama za vidole na kuweka saini ya
kielektroniki unaendelea kufanyika katika ofisi zote za Usajili za NIDA
zilizoko katika wilaya zote nchini kwa kuzingatia tahadhari na maelekezo
yaliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na changamoto ya janga
la Corona (COVID 19).
Aidha ametoa rai kwa wateja
waliokamilisha Usajili kuangalia Namba zao za Utambulisho wa Taifa
kupitia Kituo cha Huduma kwa Mteja, kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno
kwenda namba 15096 ama kupitia tovuti yetu www.nida.go.tz (https://services.nida.go.tz/nidportal/get nin.aspx)
bila kulazimika kufika kwenye ofisi za Usajili za wilaya jambo
linalowaokolea wananchi muda wao na kupunguza msongamano kwenye ofisi za
Usajili.
No comments :
Post a Comment