Wednesday, June 3, 2020

Muuguzi mbaroni kwa tuhuma za kumdai rushwa mgonjwa


Na Joyce Kasiki,Dodoma
MUUGUZI wa Zahanati ya Chamwino, Zabron Richard (32) amefikishwa Mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya sh.100,000 ili amsafishe kizazi mwanamke mkazi wa
eneo hilo.
Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Dosoma amesema leo jijini Dodoma kuwa muuguzi huyo alifanikiwa kupewa sh. 60, 000 baada ya kumsafisha mwanamke huyo kizazi.
“Tumefanikiwa kumkamata Muuguzi huyu baada ya kupokea taarifa Mei 11, mwaka huu kutoka kwa mkazi wa Chamwino akihitaji huduma ya kusafishwa kizazi, lakini akawa amekataliwa hadi atoe sh 100, 000 kinyume na sheria,” amesema Kibwengo.
Amesema baada ya taarifa hizo TAKUKURU waliweka mtego na kumbaini muuguzi huyo. Katika hatua nyingine, TAKUKURU inatarajia kumfikisha mahakamani Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpamatwa iliopo Wilayani Bahi baada ya kukutwa na makosa manne ya rushwa.

Mkuu huyo wa TAKUKURU amesema uchunguzi unaonesha Juni, 2019 mtuhumiwa alighushi miniti za vikao viwili vya kamati ya shule na mkutano wa walimu kuonesha kwamba waliridhia kiasi cha sh 469, 500 kitolewe kwenye akaunti ya shule, huku akifahamu kwamba huo ulikuwa ni uongo na kwamba aliwasilisha miniti hizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi.

No comments :

Post a Comment