Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof.
Kitila Mkumbo (kushoto) akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kyaka,
Lubale na Katuntu Wilayani Missenyi (hawapo pichani) wakati wa kukabidhi
kwa Mkandarasi eneo la mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi. Kulia ni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na Diwani wa Kata ya
Kyaka, Projestus Tegamaisho
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof.
Kitila Mkumbo (mbele katikati) alipowasili katika Kijiji cha Kyaka
kwenye eneo litalojengwa chanzo cha Maji cha Mradi wa Kyaka Bunazi
wakati wa hafla ya uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof.
Kitila Mkumbo (katikati) akielekea kwenye eneo litalojengwa chanzo cha
mradi wa Maji Kyaka Bunazi wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele ambaye ni msimamizi wa utekelezaji
wa mradi wa Maji wa kyaka Bunazi kwa niaba ya Wizara ya Maji
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wake kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji,
Prof. kitila Mkumbo (hayupo pichani)
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof.
Kitila Mkumbo (katikati) akiwasili katika Kijiji cha Kyaka wakati wa
uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kyaka Bunazi. Kutoka kushoto
Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele na Meneja wa RUWASA
Mkoa wa Kagera, Mhandisi Warioba Sanya.
Mkurugenzi, Idara ya Usambazaji
Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Nadhifa Kemikimba (aliyesimama)
akizungumza na wananchi wa vijiji vya Kyaka, Lubale na Katuntu Wilayani
Missenyi (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa maji
wa Kyaka Bunazi.
……………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu
Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amezindua na kukabidhi rasmi
ujenzi wa mradi wa kwanza nchini utakaotumia maji kutoka Mto Kagera
maarufu kama Mradi wa
Maji wa Kyaka Bunazi utakaogharimu kiasi cha
Shilingi Bilioni 15.1.
Uzinduzi kwa
ajili ya kuanza kwa utekelezwaji wa ujenzi wa mradi umefanyika Juni 1,
2020 Wilayani Missenyi Mkoani Kagera na kushuhudiwa na wananchi kutoka
vijiji mbalimbali wilayani humo ambapo Mkandarasi Kampuni ya China Civil
Engineering and Construction Corporation (CCECC) alikabidhiwa rasmi
eneo la mradi kwa ajili ya kuanza mara moja utekelezaji wake.
Profesa
Mkumbo alipongeza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kutumia Mto Kagera kuwapatia wananchi
maji safi na salama na huku akibainisha kwamba mradi wa Maji wa Kyaka
Bunazi ni wa kwanza nchini utakaotumia Mto Kagera kama chanzo chake cha
maji kwa wanachi wanaouzunguka.
“Mradi huu ni
wa kwanza kutumia maji ya Mto Kagera kupelekea huduma ya maji kwa
wananchi, kwani hatukuwahi kuwa na mradi wa namna hii ila kwa Awamu hii
ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli hili limewezekana,” alibainisha
Profesa Mkumbo.
Akielezea
namna ambavyo mradi huo ulivyopatikana, Profesa Mkumbo alisema ni
utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Julai
11, 2019 la kuhakikisha wananchi wa Mji wa Kyaka wanapata huduma ya
majisafi kutoka Mto Kagera baada ya kujionea kero ya maji waliyokuwa
nayo.
“Rais Dkt.
Magufuli alimuelekeza Waziri wetu wa Maji, Profesa Makame Mbarawa
kuhakikisha anafika hapa ili kuhakikisha tatizo la Maji linatatuliwa
haraka na kesho yake Waziri alifika na alituelekeza sisi wasaidizi wake
tuanze utekelezaji wa mradi mara moja,” alisema Profesa Mkumbo.
Kwa mujibu wa
Profesa Mkumbo, utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika sehemu
mbili ambapo moja itatekelezwa na Kampuni ya CCECC kwa gharama ya
shilingi bilioni 9.4 na nyingine itatekelezwa na wataalam wa ndani kwa
gharama ya shilingi bilioni 5.7.
Alifafanua
kuwa utaratibu wa kutekeleza baadhi ya miradi kwa kutumia wataalam wa
ndani ulianzishwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa na
umeonyesha mafanikio makubwa kwani umewezesha kupatikana kwa miradi
mizuri na kwa gharama nafuu ikilinganishwa na utumiaji wa wakandarasi.
“Mheshimiwa
Waziri alianzisha mfumo huu unaitwa force account kabla ya hapo ilikua
hata shughuli ndogo anatafutwa mkandarasi lakini sasa shughuli nyingi za
kawaida zinatekelezwa na wataalam wetu wa ndani na imetusaidia kuokoa
fedha nyingi,” alisema Profesa Mkumbo.
Aidha,
alibainisha kuwa mradi unatekelezwa kwa fedha za ndani na kwamba tayari
fedha zimetengwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati huku akiweka
wazi kwamba shilingi milioni 650 ilikwishatolewa kwa ajili ya
utekelezaji wake.
Profesa
Mkumbo alielekeza mradi ukamilike kwa wakati kwani hakuna kikwazo cha
fedha kwenye utekelezaji wake na pia wahakikishe shughuli zinazoweza
kufanywa na wananchi wa maeneo ya mradi zifanywe na wananchi hao.
“Sisi kama
Wizara tumejipanga; fedha ipo Mkandarasi hata akileta kesho maombi yake
ya awali analipwa, hakuna kikwazo cha fedha kwenye kutekeleza mradi
huu,” alisisitiza.
Akizungumzia
hali ya utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini, Profesa Mkumbo
alibainisha kwamba Mradi wa Maji wa Kyaka Bunazi unakuwa ni mradi wa
1,425 miongoni mwa miradi inayotekelezwa kwenye Serikali ya Awamu ya
Tano.
Aliongeza
kuwa hadi hivi sasa miradi 792 imekamilika na kwamba miradi 633
inaendelea kutekelezwa huku miradi 41 ikitekelezwa kwa fedha za nje na
mingine yote iliyobakia ikiwa inatekelezwa kwa fedha za ndani.
Kwa upande wake
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele ambaye
ndiyo msimamizi wa utekelezaji wa mradi kwa niaba ya Wizara ya Maji
alisema sehemu itakayotekelezwa na Mkandarasi CCECC itahusisha ujenzi wa
chanzo cha maji, ujenzi wa kituo cha tiba ya maji, ulazaji wa bomba kuu
la kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye kituo cha tiba ya
maji lenye urefu wa kilomita 1.5 na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji
yaliyotibiwa la lita milioni mbili.
Aliongeza
kuwa sehemu ya pili ya mradi itahusisha ulazaji wa bomba kuu la
usambazaji kutoka kwenye tenki lenye urefu wa kilomita 14 na ulazaji wa
mtandao wa bomba za kusambaza maji kwa wananchi ambayo itatekelezwa na
wataalam wa ndani kutoka Wizara ya Maji, Mamlaka ya Maji Mwanza
(MWAUWASA), Mamlaka ya Maji Bukoba (BUWASA) na Wakala wa Maji Vijijini
(RUWASA).
Mhandisi
Msenyele alisema mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai,
2021 na kwamba kukamilika kwake kutawezesha upatikanaji wa maji kwa
wakazi wa Kyaka, Bunazi pamoja na maeneo jirani kwa asilimia mia moja na
hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji inayowakabili
wananchi wa maeneo hayo.
No comments :
Post a Comment