…………………………………………………………………..
Dar es Salaam,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
(TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa wa msimu wa kipupwe hapa
nchini, unaoanzia Mwezi Juni – Agosti 2020, taarifa hiyo imeelezea
athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri na tahadhari kwa wadau wa
sekta mbalimbali
wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji
wa majukumu yao.
Akizungumzia msimu huo,
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya
Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi kufuatilia
utabiri huo wa msimu wa kipupwe kwa kipindi cha Juni-Agosti (JJA) 2020,
ambapo mvua za msimu wa Machi hadi Mei ambazo zilileta athari hapa
nchini zimeisha.
“Msimu huu wa kipupwe
unatarajiwa kuwa na vipindi vifupi vya upepo mkali wa Kusi na hali ya
ukavu katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, vipindi vya baridi kali
vinatarajiwa katika maeneo ya miinuko ya nyanda za juu kusini-magharibi
hususan nyakati za usiku na asubuhi”. Alisema Dkt. Kijazi
“Vipindi vya baridi kali
vinatarajiwa hasa katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Juni na
kupungua kuelekea mwishoni mwa msimu yaani mwezi Agosti kwa maeneo ya
mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa pamoja na baadhi ya maeneo ya
mkoa wa Ruvuma, maeneo haya yanatarajiwa yatakuwa na joto la kawaida
kati ya nyuzi joto 6 na 12, hata hivyo baadhi ya maeneo hususan katika
mikoa ya Njombe na Mbeya yanatarajiwa kuwa na joto la chini ya nyuzi
joto 6”. Aliongezea Dkt. Kijazi
“Nawakumbusha wananchi kuchukua
tahadhari na kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama
unavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania”, alisisitiza Dkt.
Kijazi
Akitoa ufafanuzi zaidi, Dkt.
Kijazi alielezea hali ya joto katika maeneo mengi hapa nchini, huku
akibainisha kuwa joto la kawaida linatarajiwa katika maeneo mengi ya
ukanda wa Pwani na kuashiria uwepo wa vipindi vichache vya baridi
ikilinganishwa na hali ya wastani wa muda mrefu (1981-2010) kwa miezi ya
Juni-Agosti katika maeneo hayo.
Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo unaovuma kutoka mashariki na kusini mashariki (Matlai)
vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na
kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi
katika maeneo machache.
Akizungumzia athari zinazoweza
kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema, hali ya ukavu na upepo inaweza
kuongeza upotevu wa maji kwa njia ya mvukizo na kuathiri upatikanaji wa
maji kwa mazao, mifugo na matumizi mengine. Jamii inashauriwa kuzingatia
matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
“Jamii inashauriwa kuzingatia
matumizi endelevu ya maji ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza,
wakati huohuo wakizingatia tahadhari za upepo mkali ambazo zitaendelea
kutolewa na TMA kila upepo mkali utakapojitokeza”. Alimalizia Dkt.
Kijazi
No comments :
Post a Comment