**********************************
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali leo
ametembelea kuona maendeleo ya ujenzi wa meli mpya, chelezo na
ukarabati
wa meli mbili za New Victoria na MV Mwanza (zamani Butiama) na
kuwahakikishia watanzania miradi yote hii itakamilika kwa wakati.
Akiwa kwenye maeneo ya ujenzi
jijini Mwanza leo (tarehe 8.06.2020) Dkt. Abbasi amesema ujenzi wa meli
hizo na Chelezo ni uthibitisho kuwa Serikali imetimiza wajibu wake bila
kuchelewa ambapo imeshatoa zaidi ya Shilingi Bilioni ya 100 katika
miradi hiyo minne kati ya TZS Bilioni 153.
“Hapa tulipo ni uthibitisho wa
dhana kwamba si tu angani, wodini, relini au madarajani kazi kubwa
zinafanyika lakini hata majini nako mnajionea Rais Magufuli anatekeleza
maono yake na ndoto za Watanzania kila eneo,” alisema na kufafanua kuwa
miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa Chelezo kubwa kuliko zote katika
ukanda wa Ziwa Victoria, ukarabati wa meli ya New Victoria na ukarabati
wa meli ya MV Mwanza kila kimoja kimefikia asilimia 98.
Kuhusu mradi wa nne wa uundaji wa
meli mpya na ya kisasa na itakayokuwa kubwa kuliko zote zilizowahi
kufanyakazi katika Ziwa Victoria itakayobeba abiria 1,200 na tani 400 za
mizigo, Dkt Abbasi alisema ujenzi wake sasa umefikia asilimia 60.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa
Kampuni ya Marine Services, Eric Hammis, alisema kuwa miradi
iliyofikisha asilimia 98 kimsingi ilikuwa tayari lakini inasubiri
wataalamu kutoka Korea wafikie kwa ajili ya majaribio.
“Wataalamu hao wamechelewa kuja
kutokana na zuio la Corona lakini sasa tayari wamethibitisha kuwasili
hapa nchini katikati ya mwezi Juni, 2020 ili kufanya majaribio na kisha
kuruhusu chelezo na meli za New Victoria na MV Mwanza ziweze kuanza kazi
wakati wowote mwezi huu,” alisema Eric
No comments :
Post a Comment