Afisa Muuguzi wa chumba cha upasuaji kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aimana John akiwaelekeza wauguzi wenzake namna sahihi ya kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni wakati wa mafunzo ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aimana John akiwaelekeza wauguzi wenzake namna sahihi ya kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni wakati wa mafunzo ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Wauguzi wa Taasisi hiyo walioshiriki mafunzo ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo. Lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuufahamu vizuri ugonjwa wa Corona na kufahamu njia za kuzifuata ili wasipate maambukizi na wasiwaambukize wengine.
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na Wauguzi wa Taasisi hiyo walioshiriki mafunzo ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) yanayotolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo. Lengo la mafunzo hayo ni kuwafanya wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuufahamu vizuri ugonjwa wa Corona na kufahamu njia za kuzifuata ili wasipate maambukizi na wasiwaambukize wengine.
Picha na JKCI
********************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
01/05/2020
Utoaji wa mafunzo ya mara kwa mara ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa
Corona (COVID-19) kwa wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) umewasaidia kuelewa namna ya kujikinga na ugonjwa huo na
kuwahudumia wagonjwa bila ya kupata maambukizi.
Mafunzo hayo
ambayo yamekuwa yanatolewa kwa wafanyakazi wa Taasisi hiyo tangu
ugonjwa huo ulipotangazwa hapa nchini mwanzoni mwa mwezi wa tatu mwaka
huu yamewasaidia kutokuwa na hofu na kuendelea kutoa huduma ya matibabu
kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kiufanisi zaidi.
Hayo yamesemwa
jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof.
Mohamed Janabi wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi
hiyo waliohudhuria mafunzo hayo.
Prof. Janabi
alisema baada ya wafanyakazi wa JKCI kupewa mafunzo wameweza kuufahamu
vizuri ugonjwa wa Corona, kufahamu njia za kuzifuata ili wasipate
maambukizi na wasiwaambukize wengine na kuondoa unyanyapaa kati yao na
wagonjwa kwani ugonjwa wa Corona hauchagui unaweza kumpata mtu yeyote.
“Katika mafunzo
tunayoyatoa kwa wafanyakazi wetu tunawafundisha jinsi ya kuwahudumia
wagonjwa kipindi hiki Kkigumu ambacho Dunia inapambana na janga la
ugonjwa wa Corona. Kwani baadhi ya dalili za ugonjwa huu zinafanana na
magonjwa ya moyo ambazo ni kushindwa kupumua na kukohoa hivyo basi
wakifahamu jinsi ya kujikinga kutawasaidia kuepuka kupata maambukizi’’,
alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi huyo
Mtendaji alisema ili kuwalinda wafanyakazi wa Taasisi hiyo wasipate
maambukizi wamefunga mashine ya kutakasa mwili, wametoa vitakasa mikono
pamoja na barakoa kwa wafanyakazi wote pamoja na kuwapima joto la
mwili .
Aidha kwa
wataalamu wa afya ambao wanawahudumia wagonjwa wanaohisiwa kuwa na
ugonjwa wa Corona wanavaa vifaa kinga na kufuata mwongozo wa kuzuia
maambukizi wa mwaka 2018 na wa uzuaiaji wa maambukizi ya Virusi
vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa mwezi wa kwanza mwaka
2020 wakati wanawahudumia wagonjwa hao.
Prof. Janabi
alisema, “Wagonjwa wanaofika kutibiwa katika Taasisi yetu wanapimwa
joto la mwili kabla ya kuanza kupata huduma ya matibabu pia tumefunga
mabomba ya maji pamoja na kuweka vitakasa mikono katika maeneo
mbalimbali ya Taasisi yetu hii inawafanya kupata nafasi ya kunawa mikono
mara kwa mara”,.
“Tunatoa elimu
ya ugonjwa huu kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kupitia vipindi
mbalimbali vinavyorushwa katika Televisheni zilizopo katika Taasisi yetu
pia wataalamu wetu wanatoa elimu kila siku kabla ya kuanza kwa
kliniki zetu’’,.
Prof.Janabi
aliongeza kuwa Taasisi hiyo imetenga wodi maalum kwa wagonjwa
wanaohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ambao baada ya majibu ya
vipimo kutoka na kubainika kuwa na ugonjwa huo wanapelekwa katika kituo
cha Amana na kuendelea kupewa huduma za matibabu ya moyo wakiwa huko.
Kwa upande wake
mratibu wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha utafiti na
mafunzo Dkt. Naiz Majani alisema kuwepo kwa mafunzo hayo kumesaidia kwa
kiasi kikubwa kuwaondoa hofu wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuhusu ugonjwa
wa Corona.
Dkt. Naiz
ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema
mafunzo hayo yanatolewa katika vikundi vichache vya wafanyakazi kutokana
na kada zao hali ambayo inawasaidia kuelewa zaidi.
“Katika Taasisi
yetu tuna wafanyakazi wa kada ya afya na ambao siyo wa kada ya afya,
hata mafunzo tunayoyatoa tumewagawa kutokana na kada zao na lugha
tunayotumia kufundishia ni tofauti hii yote tunataka wauelewe kwa undani
zaidi ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga wao na kuwakinga wengine
wanaowazunguka”, alisema Dkt.Naiz.
Daktari huyo
bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliwaomba washiriki wa mafunzo
hayo kutoa elimu waliyoipata kwa watu wengine ili wajikinge na ugonjwa
huo. Pia wafuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ambayo ni
kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayotiririka
na sabuni , kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kukaa umbali wa zaidi
ya mita moja kati ya mtu na mtu.
No comments :
Post a Comment