Waziri Ummy Mwalimu akiongea na mwananchi kupitia kituo cha afya cha huduma kwa wateja mara baada ya kukizindua
Waziri Ummy Mwalimu akiongea wakati wa uzinduzi huo
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiangalia namna watoa
huduma wanavyopokea simu kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kupata elimu
kuhusu ugonjwa wa Corona
Muonekano wa kituo cha afya cha huduma kwa wateja ambacho kitakua na wataalam 150 wa kutoa elimu na taarifa kwa wananchi
………………………………………………………………………….
Na. Catherine Sungura,WAMJW,Dar es Salaam.
Serikali itaendelea kutoa takwimu
za mwenendo kuhusu Ugonjwa wa Corona mara baada ya
kukamilika kwa
maboresho ya kiufundi ya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati
akizindua kituo cha Afya cha huduma kwa wateja (Afya call center)
kilichopo eneo la Chuo cha Afya ya Sayansi ya Jamii Muhimbili (MUHAS),
upanga Dar es Salaam.
“Takribani siku Saba sasa
hatukuweza kutoa taarifa za takwimu za maabara kuhusu mwenendo wa
Corona nchini kwa sababu sasa hivi tunafanya maboresho ya maabara ya
taifa ya afya ya jamii,hivyo niwatoe hofu wananchi kwamba ndani ya siku
chache zoezi litakamilika na tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa
mara”, alisema.
Waziri Ummy amesema kuwa Corona
ipo na itaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa,pia kumekuwepo na vifo
kutokana na ugonjwa huu, hivyo wananchi wanapaswa kujua namna ya kuishi
na ugonjwa huo kwa kujikinga na maambukizi.
“Ninawasihi wananchi muondoe hofu
na muendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga kwani ugonjwa wa Corona
bado upo Tanzania, wagonjwa wapo na vifo vinavyotakana na COVID-19
vipo, ni muhimu kutambua kuwa ugonjwa huu utaendelea kuwepo kwa miezi
kadhaa hivyo lazima mchukue tahadhari ya kujikinga kama magonjwa
mengine”Alisisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amewataka
wananchi kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa za kila siku
pamoja na kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima,
kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka, na kukaa umbali wa mita
moja kati ya mtu na mtu mwingine.
Kuhusu Uvaaji wa barakoa, Waziri
huyo amewataka wananchi kuendelea kuvaa barakoa za vitambaa ili
kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo na kuwa barakoa za viwandani
ziachwe zitumike kwa ajili ya watoa huduma za afya.
Amewashauri wananchi kufua na
kupiga pasi barakoa za vitambaa kabla ya kuzitumia na kusisitiza kuwa
zinapaswa kuwa safi kabla ya kuvaliwa.
MWISHO
No comments :
Post a Comment