Tuesday, May 12, 2020

TANESCO KUWEKEZA BILIONI 1.2 UMEME WA KIWANDA CHA SUKARI MTIBWA



…………………………………………………………………………………..
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema Serikali kupitia TANESCO imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya kikazi kukagua hali ya upatikanaji
wa umeme katika kiwanda cha Mtibwa kilichopo Mkoani Morogoro.
Aliongeza kuwa, njia ya umeme itakayojengwa ni ya umeme mkubwa yenye urefu wa takriban kilomita 100 na itakuwa maalum kwa ajili ya Kiwanda Sukari cha Mtibwa.
Aidha, ujenzi huo utaanza ndani ya siku mbili zijazo.
Alisema ujenzi wa njia hiyo ya umeme utakwenda sambamba na ongezeko la kiasi cha umeme ambacho kitafikishwa kiwandani hapo ikiwa ni megawati 27 hadi 40, ili kukidhi ongezeko la mahitaji yoyote ya umeme yatakayojitokeza kiwandani hapo kwa kipindi cha miaka mitano hadi kumi ijayo.
Dkt. Kalemani alitanabaisha kuwa, mahitaji ya umeme katika kiwanda hicho kwa sasa ni megawati 5 hadi 8 lakini kutokana na maboresho makubwa ambayo ameelezwa kuwa yatafanyika kiwandani hapo ndani ya kipindi cha miaka mitano unatarajiwa mahitaji ya umeme kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia takriban megawati 27 ifikapo mwaka 2025.

No comments :

Post a Comment