Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati na waandishi wa habari.
……………………………………………………………………………….
TAASISI ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa nchini, (TAKUKURU) Mkoani Manyara, inawashikilia
maofisa wawili wa mamlaka ya mapato nchini (TRA) kwa kudaiwa kupokea
rushwa ya shilingi milioni 10.
Mkuu wa TAKUKURU
Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati alisema
maofisa hao TRA wanadaiwa kufanya kosa hilo kinyume cha kifungu cha 15
cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Makungu aliwataja
majina yao maofisa hao wa TRA wanaodaiwa kupokea rushwa ya shilingi
milioni 10 kuwa ni Subilaga Mwangama na Ojungu Mollel.
Alisema washtakiwa
hao wanatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa wilaya ya
Babati na kusomewa mashtaka na waendesha mashtaka wa TAKUKURU, Isdory
Kyando akisaidiana na wakili Martin Makani.
Alisema maofisa hao
wa TRA wanadaiwa kupokea rushwa hiyo baada ya kumuomba mfanyabiashara wa
mjini Mbulu, (jina linahifadhiwa) ambaye ni mlipa kodi mzuri kwenye
ofisi za TRA Mbulu.
“Mfanyabiashara huyo
alilipa kodi ya shilingi milioni tisa mwaka, 2018 hata hivyo Machi mwaka
huu akapigiwa simu na watuhumiwa akitakiwa kufika ofisi za TRA mjini
Babati,” alisema Makungu.
Alisema
mfanyabiashara huyo alipofika mjini Babati watuhumiwa hao wawili
walimwambia wamefanya uchunguzi na kugundua kuwa alikadiriwa vibaya
hivyo alipe ongezeko la shilingi milioni tano.
Alisema hata hivyo
mfanyabiashara huyo alikubali na kuanza kulipa ongezeko hilo kwa awamu
baada ya kuruhusiwa na meneja wa TRA wilayani Mbulu.
“Mfanyabiashara huyo
baada ya kulipa awamu ya kwanza ya fedha hizo alipigiwa simu tena na
watuhumiwa hao na kutakiwa kuonana nao Babati juu ya ulipaji wa kodi wa
mwaka 2018 waliomaliza kujadili,” alisema Makungu.
Alisema alipofika
mjini Babati maofisa hao wa TRA walimwambia kuna ongezeko la kodi ya
shilingi milioni 45 kwenye biashara yake.
Alisema ongezeko hilo
lilimweka mfanyabiashara huyo kwenye wakati mgumu ndipo wakampoza kuwa
watampunguzia hadi shilingi milioni tisa endapo angekubali kuwapa
rushwa.
“Walijadiliana kiasi
cha kutoa rushwa ili apunguziwe ndipo akaelezwa atoe shilingi milioni 10
akaelekezwa kuzipeleka kwa mawakala waliopo mjini Babati ndipo TAKUKURU
wakaweka mtego na kuwakamata watuhumiwa,” alisema Makungu.
Alitoa wito kwa TRA
kuangalia upya mfumo wa ulipaji kodi ili kuondoa mianya ya maofisa wake
kuwabambikia wafanyabiashara kodi kisha kuwatishia kwa rushwa kama
watuhumiwa hao walivyofanya.
No comments :
Post a Comment