………………………………………………………………………………………
Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
SEKTA ya Kilimo
nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya uchumi wa
wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu tunapojizatiti
kufikia uchumi wa
viwanda.
Katika kipindi
cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa kutumia
bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Tsh. Trilioni
25.2 Mwaka 2015 hadi Tsh. Trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile, sekta
imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018 na
kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa huku sekta ndogo ya mazao
ikichangia asilimia 16.2 na hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo.
Ili kufikia
kiwango malengo makubwa ya uzalishaji wa mazao, Sera zinazoongoza
utafiti zina mchango mkubwa katika kupanga maendeleo ya sekta ya kilimo
ikiwa ni pamoja na ya kuboreshea viwango vya maisha ya wananchi kwa
kuchochea ukuaji na kuongeza tija katika sekta muhimu za uzalishaji za
uchumi wa taifa.
Historia
inaonyesha kuwa nchi zilizozingatia sera zenye mwelekeo wa utafiti
thabiti zimefanikiwa kujenga uchumi wenye ushindani kwa kutumia
rasilimali walizonazo, na kuziendeleza kwa ajili ya kuboresha maisha ya
wananchi wao.
Katika jitihada
hizo, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
imeendelea kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na
uvuvi katika eneo la Tafiti na Ushauri elekezi ili kutoa huduma ya elimu
ya ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema Serikali
kupitia SUA imeendelea na miradi mipya 13 ya utafiti yenye lengo la
kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ili
kuwezesha wananchi kuzalisha mali na malighafi za mazao ya kilimo kwa
ajili ya viwanda.
Prof. Ndalichako
anasema Chuo hicho pia kimeweza huduma ya elimu ya ushauri wa kitaalamu
kwa wakulima 9,500 kwa kutumia vituo atamizi, mashamba darasa, semina,
kozi fupi, runinga na redio kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija
na kupunguza umaskini kwa wananchi.
‘Mafunzo hayo
yametolewa kwa wakulima katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Iringa,
Dodoma, Tabora, Tanga, Pwani na Morogoro kwa lengo la kutoa elimu kuhusu
kilimo na ufugaji’’ anasema Prof. Ndalichako.
Aidha Prof.
Ndalichako anasema SUA pia ) imepima jumla ya sampuli 1,553 zikiwemo
sampuli za udongo 1,180, za mimea 297, za mbolea za viwandani 20, za
samadi tisa (9) na sampuli za maji 47 kutoka kwa watafiti mashirika ya
kilimo, Viwanda na Taasisi mbalimbali pamoja na wakulima binafsi.
Waziri Ndalichako
anasema kuwa Serikali imeingia mikataba mipya 13 ya mahusiano na
Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo
wafanyakazi na wanafunzi katika kufanya tafiti za kisayansi na kilimo
kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija katika shughuli mbalimbali
za maendeleo kwa wananchi.
Anazitaja taasisi
hizo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sophia kilichopo Japan; National
Institute of Health – Korea; Foundation Pierre Fabre – France; Kunming
Institute of Zoology, Chinese Academy of Science; Silverlands Tanzania
Limited – Iringa, Tanzania; College of Animal Science and Technology
Nanjing Agricultural University – China; Agronomos Sin Fronteras
Foundation (ASFF ) – Iringa Tanzania; University of Leeds – UK; na Wuhan
University (WHU) – China.
Akifafanua zaidi
Prof. Ndalichako anasema katika kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia Serikali imejenga jengo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi
2,400 kwa wakati mmoja litakalokuwa na maabara nane zenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi 100 kila moja.
Prof. Ndalichako
anasema Serikali pia imekamilisha ujenzi wa jengo la utafiti wa wanyama
na wadudu kwa ufadhili wa mradi wa Eastern and Southern Africa Centers
of Excellence for Innovative Rodent Pest Management and Biosensor
Technology Development (ACE II, IRPM and BTD) na kuendelea na ukarabati
wa madarasa likiwemo jengo la Hay Building kwa lengo la kuongeza nafasi
za kufundishia na kujifunzia.
Mazao ya Kilimo
ni malighafi muhimu sana katika viwanda, hivyo ni utafiti ni nguzo
muhimu sana inayoweza kuleta kuleta ubunifu wa bidhaa, uboreshaji wa
bidhaa, kuongeza ufanisi wa huduma, tija na ubora wa utendaji katika
soko.
No comments :
Post a Comment